Mshambuliaji wa Crystal Palace, Christian Benteke, ameweka historia mpya kwa kufunga bao sekunde ya 7, baada mchezo kuanza wakati Ubelgiji ikicheza dhidi ya Gibraltar, katika kuwania kushiriki fainali za Kombe la Dunia, Urusi 2018.
Wakati Benkete aliweka rekodi hiyo baada ya kuchukua nafasi ya mshambuliaji wa klabu ya Everton, Romelu Lukaku aliyekosekana kwenye mchezo huo kutokana na majeraha, ameweka rekodi yake kwa kuwa mchezaji aliyefunga bao la mapema zaidi kwenye historia ya hatua za kuwania kufuzu kwa Kombe la Dunia.
Rekodi hiyo ilikuwa inashikiliwa na mshambuliaji wa San Marino, Davide Gualtieri, ambaye amekuwa anashikilia rekodi hiyo tangu mwaka 1993, amekuwa anashikilia rekodi hiyo baada ya kufunga bao sekunde ya 8.3 dhidi ya England.
Benteke ambaye alishindwa kutamba kwenye kikosi cha Liverpool, aliinasa pasi ya mchezaji wa Gibraltar kisha kabla ya kufunga bao kwa mguu wa kushoto.
Klabu ya Crystal Palace ilimnunua Benteke kwa kiasi cha pauni milioni 27, kutoka Liverpool kwa kandarasi ya miaka minne, akiwa Liverpool alionekana kutokuwa kwenye mipango ya kocha Jürgen Klopp.
Awali mchezaji huyo alijiunga na Liverpool akitokea klabu ya Aston Villa kwa kiasi cha pauni milioni 32.5, kujikuta akimaliza msimu kwa kufunga mabao 10 kwa mechi 43 tofauti na alipokuwa katika Klabu ya Aston Villa alipofunga idadi ya mabao zaidi ya 50.
Katika mechi hiyo ya timu ya taifa, Benteke aliongeza bao jingine dakika mbili kabla ya mapumziko na kuifanya Ubelgiji kuwa mbele kwa magoli 3-0 hadi wakati wa mapumziko.
Benteke alikamilisha hat trick yake dakika ya 55, kipindi cha mchezo huo ambao Ubelgiji ilishinda kwa mabao 6-0.
Wafungaji wengine wa mabao ya Ubelgiji walikuwa ni Witsel (19’), Mertens (51’) na Hazard (79).