*Yajipanga kuipiga mnada ‘nyumba ya Serikali’
*Ni kinyume cha vipengele vilivyowekwa kisheria
*Mfanyabiashara adai mkopo wageuzwa ndoana
DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Wetu
Nyumba iliyokuwa ikimilikiwa na serikali imo hatarini kupigwa mnada kwa kile kinachodaiwa kuwa mmiliki wake kushindwa kulipa mkopo aliouchukua benki; JAMHURI limebaini.
Nyumba hiyo iliyopo katika Kitalu Na. 1829, Msasani Peninsula, Dar es Salaam, ni mali ya mume wa Happy Magulla anayefahamika kwa jina la Ephraim Magulla na wakati wowote huenda ikapigwa mnada na Dalali wa Mahakama kupitia Benki ya Exim Tanzania.
Happy ni mmiliki na Mkurugenzi wa Kampuni ya M/S Hedico ambayo mwaka 2013 ilichukua mkopo wa Sh milioni 400 kutoka Benki ya Exim kwa dhamana ya nyumba kupitia hati Na. 113294.
Awali, mwaka 2010, Magulla aliuziwa nyumba hiyo na serikali ambapo kwa sasa thamani yake inakadiriwa kuwa zaidi ya Sh bilioni 2.
Akizungumza na JAMHURI, Happy anasema kitendo anachofanyiwa na Exim Benki si cha kiutu, kinalenga kufanya dhuluma ya wazi na kumtosa kwenye lindi la umaskini.
“Niliomba mkopo wa Sh milioni 500 Exim kwa kuwapa nyaraka ikiwamo hati ya nyumba. Wakazikagua na kunipa mkopo wa Sh milioni 400 kwa makubaliano ya kurejesha Sh milioni 15 kila mwezi,” amesema Happy.
Hata hivyo, hati ya mauziano kati ya serikali na Magulla (nakala yake tunayo) inaonyesha kuwapo kwa kipengele kinachozuia nyumba hiyo ama kuuzwa, kuhamisha umiliki wake au kuwekwa rehani kwa kipindi cha miaka 25.
Kuhusu kipengele hicho, Happy anasema:
“Sikuwa na uelewa kama kuna zuio la kutoichukulia mkopo nyumba ya mume wangu. Benki walikuwa na wajibu wa kunieleza kuhusu hilo kabla ya kunipa mkopo. Wakanipa fedha wakisema kila kitu kipo sawa.”
Mwanzo wa matatizo
Happy anakiri kwamba kuna nyakati hakuweza kulipa Sh milioni 15 kwa mwezi kama makubaliano yalivyokuwa, na mwaka 2015, Benki ya Exim ikafungua shauri Na. 60/2015 katika Mahakama Kuu Dar es Salaam Kitengo cha Biashara, ikimshitaki yeye, mumewe na mtu anayefahamika kwa jina la Abdallah Wanzala kwa kushindwa kufanya marejesho kwa wakati.
Wakati huo mkopo na riba yake vilikuwa vimefika Sh milioni 685. Kesi hiyo ilisikilizwa hadi mwaka 2018 ambapo pande husika zikaafikiani kuingia makubaliano mapya nje ya mahakama.
Happy amesema makubaliano hayo yalikuwa ya kufanya marejesho ya Sh milioni 4 kila mwezi.
“Mara moja nikaanza kutekeleza makubaliano hayo,” amesema na kuongeza kuwa hadi wakati wa makubaliano hayo, tayari alikuwa amekwisha kurejesha benki Sh milioni 385 kupitia akaunti ya Benki ya Exim, Tawi la Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, ambapo salio la deni na riba lilikuwa ni Sh milioni 300.
“Lakini kutokana na makubaliano hayo mapya, Exim wakanijulisha kuwa sasa deni pamoja na riba ni Sh milioni 441 si Sh milioni 300 tena. Tukakubaliana kwamba nilipe kwa kipindi cha miezi 116 (sawa na miaka tisa na miezi minane).
“Ajabu ni kwamba hata kabla muda huo haujaisha, Exim wamefikia hatua ya kuuza nyumba kwa hoja kwamba sijafanya marejesho kwa kipindi kirefu,” amesema.
Nia ovu ya Exim
Katika makubaliano baina yake na Benki ya Exim ya mwaka 2018 (nakala tunayo), kuna kipengele kinachomtaka Happy kufanya marejesho kila mwezi bila kupitisha hata mwezi mmoja na kwamba hilo likitokea, dhamana yake (nyumba) itauzwa kufidia.
Na ni kwa kigezo hicho ndipo mahakama sasa imeamua kuruhusu nyumba kuuzwa huku Happy akidai kuwa:
“Exim wameidanganya Mahakama kuwa tangu mwaka 2018 nimerejesha Sh milioni 25 tu. Lakini si kweli, wao wamepeleka benki akaunti moja kama kielelezo wakati ni wao wenyewe walionibadilishia akaunti ya kufanyia marejesho mara mbili.
“Mwanzo akaunti niliyokuwa naingiza fedha ilikuwa Na. 019900007907 yenye majina yangu. Humo nilikuwa nimeweka Sh milioni 385 kama marejesho. Wakanibadilishia na kunipa nyingine Na. 184000110 iliyosoma jina la IBIT.
“Hiyo nayo baadaye waliibadili na kunipa yenye Na. 199000100; jina System Suspense. Mabadiliko yote hayo yalifanyika bila kunieleza sababu za msingi.”
Happy anadai kuwa benki wanasema hawaitambui akaunti ya IBIT ilhali jumla ya fedha alizoweka kwenye akaunti zote mbili ni Sh milioni 175.
“Kwa mujibu wa risiti za malipo nilizonazo za fedha nizoingiza kwenye akaunti walizonipa Exim, mpaka sasa nimekwishawapa Sh milioni 560, na muda wa kufanya marejesho bado upo!” amesema Happy huku akipinga hatua ya benki kulazimisha nyumba kuuzwa, akisema huo ni umumiani.
Amesema tangu mwaka 2015 Exim wameonyesha kuwa na nia ya kuuza nyumba tu, wala si kupokea fedha za marejesho, wala hawataki kumsikiliza, kumpa taarifa za kifedha (bank statement) za akaunti yake huku wakitumia taarifa za uongo kutoka kwenye akaunti ya mwanzo ambayo walikwisha kumzuia kupitishia marejesho.
“Japo mahakama imefanya uamuzi (Februari 22, 2022 kumpa dalali mamlaka ya kuuza nyumba), lakini uamuzi huu umeacha maswali mengi ambayo yalitakiwa kupatiwa majibu kabla ya hukumu.
“Mahakama ilipaswa kuhoji, nini kilifanyika kati ya benki na msajili wa hati akawakubalia wanipe mkopo? Hawakuona dosari ya kuwapo zuio kwenye hati?” amesema na kuhoji Happy.
Maofisa wa Exim wazungumza
Kwa upande mwingine, JAMHURI limewatafuta maofisa kadhaa wa Benki ya Exim kutaka kujua ukweli wa benki kutaka kuuza nyumba iliyokuwa ikimilikiwa na serikali kinyume cha utaratibu na sababu za kumbadilishia Happy akaunti za marejesho.
Ofisa Marejesho Mikopo (Recovery Officer) wa Benki ya Exim, Jacob Sanga, hakuwa na majibu ya moja kwa moja akisema:
“Siwezi kutoa ushirikiano kwenye masuala hayo, kwa kuwa mimi si mhusika. Anayeweza kukueleza kwa ufasaha ni msimamizi wa Kitengo cha Masoko.”
Ofisa Masoko wa Benki ya Exim ambaye hakutaka kutaja jina (namba yake ya simu tunayo), amekiri kufahamu habari za Happy na Kampuni ya Hedico, lakini hakutaka kufafanua chochote kuhusu ama sababu za kutoa mkopo kwa dhamana ya nyumba ya serikali au kubadili akaunti za marejesho mara kwa mara, akisema:
“Suala hili kwa sasa limo mikononi mwa Dalali wa Mahakama.”
JAMHURI limezungumza na dalali mhusika katika sakata hili, Kishe Auction Mart, ambapo Mkurugenzi wake, Benson Swai, naye hakutaka kutoa ushirikiano.