Benki ya Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KCBL) inakusudiwa kushitakiwa mahakamani kujibu tuhuma za kumdanganya mwanachama wa Benki ya Kijamii Vijijini (VICOBA) kuwa benki hiyo ingempatia mkopo wa Sh milioni 50.
Mwanachama huyo, Vicent Mulamba, ameipa KCBL hati ya kusudio la kuifikisha mahakamani kwa kile anachodai ilimdanganya mkopo licha ya kutimiza masharti.
Nakala ya barua hiyo ya Machi 4, mwaka huu, ambayo JAMHURI ina nakala yake imepelekwa kwa Mkurugenzi wa Shirika la Hifadhi la Taifa (NSSF) kupitia kwa Meneja wake Mkoa wa Kilimanjaro, Angela Mollel.
Mollel ni mmoja wa viongozi wa Vicoba Endelevu; pamoja na Kampuni ya H. M. Associates iliyojihusisha na michanganuo ya mikopo.
Vikundi zaidi ya 140 vya wajasiriamali (wana-Vicoba) katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha viliahidiwa mikopo ya kati ya Sh milioni 50 na Sh milioni 60 kupitia KCBL kwa sharti la kujiunga NSSF. Hata hivyo, mpango huo umeyeyuka na kuzua sintofahamu kutoka wa wana-Vicoba hao.
Inadaiwa kuwa mmoja wa maofisa wa idara ya mikopo katika KCBL alipokea Sh 100,000 kutoka kwa kila mwanachama wa Vicoba kama ‘kilainishi’ cha upatikanaji mikopo haraka.
“Bila halali yoyote, mlinidanganya ya kwamba sina sifa za kukopesheka hadi pale nitakapojiunga na Vicoba Endelevu, niwe mwanachama wa NSSF, nifungue amana au niwe mteja wa KCBL, lakini pia niwe na mchanganuo wa biashara.
“Bila halali yoyote mlinidanganya kwamba maendeleo yangu yataendelea kudorora ikiwa sitachukua uamuzi wa haraka wa kuchangamkia fursa ya mkopo mnono kwa kutii masharti katika muda mfupi,” inasema sehemu ya barua ya kusudio la kuishitaki KCBL.
Mwanachama huyo anasema kutokana na ushawishi wa maofisa wa KCBL aliamua kuacha kazi zilizokuwa zikimwingizia kipato na kuelekeza nguvu zote kwenye mkopo.
Miongoni mwa masharti anayosema alipewa na kuyatekeleza ni pamoja na kujiunga kwenye Vicoba Endelevu na kutoa kiingilio cha Sh 120,000; kugharimia uzinduzi wa Vicoba Endelevu kwa kutoa Sh 20,000 na kununua fulana kwa Sh 8,000 ambayo angeivaa wakati wa uzinduzi.
Masharti mengine ni kujiunga na NSSF kwa kulipa ada ya miezi sita kwa kiwango cha Sh 20,000 kila mwezi na kufungua akaunti KCBL kwa kima cha Sh 30,000.
Pia anasema alipewa sharti la kuandikiwa mchanganuo wa biashara na kuelekezwa mchanganuo huo ufanywe na kampuni ya H. M. Associates ambako kila mwanachama alitozwa Sh 250,000.
Amelalamika kuwa pamoja na kukamilisha masharti yote aliyopewa, uongozi wa KCBL umekataa kumkopesha Sh milioni 50.
“Mtandao wenu wa kunilaghai umeniathiri, kwa sababu hiyo ninataka mnilipe fidia ya madhara ya kiasi cha Sh milioni 30 ili akili yangu itulie na kufanya biashara mliyonichochea kuifanya,” inasema barua hiyo.
Meneja wa KCBL, Elizabeth Makwabe, amekiri kupokea hati hiyo ya kusudio la kufikishwa mahakamani, lakini akagoma kuingia kwenye undani wa suala hilo.
Sakata latinga TAKUKURU
Taasisi ya Kuzia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeamua kuingilia kati mgogoro wa mikopo kwa wanachama zaidi ya 4,000 wa Vicoba katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.
Taasisi hiyo inachunguza majalada 56 yanayotokana na tuhuma 126 zilizofikishwa katika ofisi hiyo mkoani Kilimanjaro. Taarifa za awali zinasema Takukuru imejiridhisha majalada hayo yameiweza kuwa na msingi wa uchunguzi.
Miongoni mwa tuhuma zinazochunguzwa zinagusa ufisadi, rushwa na matumizi mabaya ya madaraka katika kipindi cha Januari hadi Machi, mwaka huu.
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Alexander Kuhanda, amesema tuhuma 126 zilipokewa na kuzipitia, ofisi yake imefungua majalada 56 huku maeneo yaliyoonekana kulalamikiwa zaidi ni rushwa katika vyama vya ushirika vya msingi.
Maeneo mengine ni idara za ununuzi katika ofisi mbalimbali za Serikali na mfumo unaosimamia Vicoba katika Mkoa wa Kilimanjaro. Amesema wana-Vicoba zaidi ya 4,000 wanahangaikia mikopo katika KCBL.
Maofisa watatu wa benki hiyo wamehojiwa kuhusu mikopo ya wanachama wa Vicoba Endelevu.
Baadhi ya watumishi wa umma wameshafikishwa mahakamani wakituhumiwa kufuja mali za umma, kughushi na matumizi mabaya ya madaraka.
Takukuru imesema kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro, imeokoa Sh milioni 33 kutoka kwa mfanyabiashara mmoja aliyekuwa anakwepa kodi kwa kutumia namba feki ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN). Jina lake halikutajwa.
Takukuru imesema mafanikio iliyopata katika kipindi cha miezi mitatu, yametokana na mwitikio wa jamii katika kutoa taarifa na utayari wa kuipa taasisi yake ushirikiano.