BENKI ya NMB na timu ya Mpira wa miguu ya Azam FC wamekubaliana kuongeza mkataba wa udhamini kwa mwaka mmoja zaidi.
Mkataba mpya wa Udhamini ulianza mwezi septemba – 2017 na ni mkataba wenye thamani na manufaa zaidi katika historia ya udhamini wa klabu ya Azam kwa miaka 10 tangu kuanzishwa.
Utilianaji saini mkataba mpya ni muendelezo wa mkataba ambao ulisainiwa kwa mara ya kwanza mwaka 2014, ukaongezwa mwaka mmoja – mwaka 2016 na sasa inaongeza mwaka mmoja zaidi ya ushirikiano na udhamini kati ya Azam FC na NMB Bank.
Nembo ya mdhamini Mkuu wa Azam FC ambaye ni NMB Bank itakuwa inaonekana mbele ya jezi za wachezaji na benchi la ufundi kama ilivyozoeleka.
“Ushirikiano huu unazikutanisha benki kubwa na bora kuliko zote Tanzania na mojawapo ya timu kubwa za mpira wa miguu nchini na mabingwa wa kihistoria wa kombe la Mapinduzi,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa NMB Bank – Ineke Bussemaker.
Bi Bussemaker alisema “Hakuna mchezo wenye wapenzi wengi nchini kama mpira wa miguu. Timu ya Azam ina uwezo mkubwa wa kuwaunganisha watanzania wengi kupitia mpira wa miguu, Ndio maana benki ya NMB ambayo wateja wake ni sehemu ya mashabiki wa mpira wa miguu nchini imeamua kuendeleza msaada wake kwenye mpira wa miguu kupitia timu ya Azam.”
“Huu ni ushirikiano wa muda mrefu na wenye faida kwa pande zote mbili, tunaamini kuwa tutaendelea kujifunza kwa kila mmoja na kupata matokeo chanya pamoja,” alisisitiza Bi. Bussemaker
Mkurugenzi wa Azam FC– Abdul Mohamed alisema “tumefurahi sana kuongeza udhamini wetu na NMB Bank ambao ni wa kipekee katika historia ya timu yenye malengo ya kutengeneza muunganiko mzuri wa mashabiki wa mpira na benki ya NMB.
Bwana Mohamed aliongeza kuwa “Udhamini huu ni wa kipekee unaohusisha benki kubwa kuliko zote nchini ambayo imekuwa mstari wa mbele kusaidia mpira wa miguu kwa miaka mingi. Huu unaipeleka timu yetu ya Azam hatua moja zaidi katika maendeleo ndani na nje ya uwanja.
NMB ni benki inayoongoza nchini Tanzania kwa matawi, ikiwa na zaidi ya matawi 212, wateja zaidi ya milioni 3 na zaidi ya mashine 700 za kutolea fedha (ATM) nchi nzima. NMB imeasisi ubunifu mkubwa katika soko la Tanzania ikiwa ni pamoja na huduma za benki kwa njia ya simu yaani NMB mobile, Pesa Fasta na malipo kwa kutumia mashine za ATM.
NMB inaendelea kujikita katika kutoa huduma kwa makampuni makubwa, masoko ya kifedha pamoja na huduma za kusaidia makusanyo ya kifedha na biashara. Lakini Pia imekuwa mstari wa mbele katika maendeleo ya kilimo na imeanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani kupitia vyama vya ushirika nchini.
NMB imekuwa ikisaidia utoaji wa huduma za kifedha kwa Serikali kupitia matawi yote nchini ambapo asilimia 60 yapo maeneo ya vijijini.