Na Mussa Augustine,JamhuriMedia
Benki ya Maendeleo Plc imepata faida ya shilingi Bilioni 1.3 mwaka 2022 ukilinganisha na faida ya shilingi milioni 587 ambapo ni sawa na ongezeko la zaidi ya mara mbili ya faida hiyo.
Hayo yamesemwa Jijini Dar es salaam Januari 30 ,2023 na Mkurugenzi wa Benki hiyo Dkt Ibrahim Mwangalaba wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuelezea ufanisi na utendaji kazi wa Benki hiyo Kwa mwaka 2022.
Dkt Mwangalaba amebainisha kuwa faida hiyo imetokana na ukuaji wa jumla wa mapato Kwa asilimia 22 mwaka hadi mwaka kutoka shilingi za kitanzania Bilioni 12.8 hadi shilingi za kitanzania Bilioni 15.6 mwaka 2022.
Amesema kuwa Mapato halisi yaliongezeka Kwa asilimia 31 kutoka shilingi za kitanzania Bilioni 7.6 mwaka 2021 hadi shilingi za kitanzania Bilioni 9.9 mwaka 2022,pamoja na biashara ya mikopo kutokana na kuimarika Kwa hali ya uchumi na kuboresha ubora wa vitabu vya mkopo kutoka mikopo chechefu asilimia 13 mwaka 2021 hadi asilimia 5.2 mwaka wa 2022.
“Amana za wateja ziliongezeka kwa asilimia 11 kutoka shilingi za kitanzania Bilioni 70 mwaka 2021 hadi shilingi za kitanzania 77 mwaka 2022 wakati mikopo na malipo ya awali kwa wateja yaliongezeka Kwa asilimia 5 kutoka shilingi za kitanzania Bilioni 57 Hadi shilingi za kitanzania Bilioni 60 mwaka 2022” amesema Dkt Mwangalaba.
Aidha Mkurugenzi huyo wa Benki ya Maendeleo Plc ameendelea kusema kwamba mwaka 2022 benki hiyo imewakopesha Wafanyabiashara ndogondogo wapatao 2500,ambapo kiasi cha shilingi Bilioni 3. zimetumika kwa ajili ya mikopo hiyo.
Dkt Mwangalaba amesema kwamba mwaka huu 2023 Benki hiyo inatarajia kuwafikia Wamachinga zaidi ya elfu tano,pamoja na makundi ya Wanawake na vijana kuwapatia Elimu ya biashara na kuwapatia mikopo yenye riba nafuu Kwa wale wanaokidhi vigezo ili kuweza kuwainua kiuchumi.
Hata hivyo amesema kwamba Benk hiyo inatarajia kufungua tawi jipya Mbagala Jijini Dar es salaam,kuanzisha huduma za mtandao( Internet Banking) na huduma ya ulipaji na upokeaji wa malipo ( Payment Collection System) itakayotumika Kwa ajili ya kulipa ada mashuleni pamoja na kulipa gharama za matibabu hospitalini.
” Mfumo huu unasaidia kulipa ada au malipo ya gharama za matibabu hospitalini,mfumo huu ukilipa tu taarifa zinafika sehemu husika hakuna haja ya kupeleka risiti ya malipo ,tunafanya hivi Ili kuwaondolea wazazi usumbufu wa kupeleka risiti shuleni au hospitalini” amesema Dkt Mwangalaba.