Na Immaculate Makilika – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na Vyama vya Wafanyakazi nchini imefanya jitihada mbalimbali ili kukuza uchumi wa nchi
Hayo ameyasema leo Mei 1, 2023 mkoani Morogoro wakati akihutubia katika Sherehe za Siku ya Wafanyakazi zilizofanyika kitaifa katika mkoa huo.
“Pongezi nyingi kwa wafanyakazi wa sekta ya umma na sekta binafsi kwa mchango wao mkubwa katika huduma za uzalishaji ambao unachangia katika ukuaji wa nchi yetu. Nadhani hivi karibuni wote mmesoma maelezo ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani kuipongeza Tanzania kwa kukua kwa uchumi wetu, lakini pia kuwa na mipango mizuri ya sera za fedha na matumizi, tulipongezwa mno na hapa kuna mkono mkubwa wa wafanyakazi”, alisema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia aliwataka wafanyakazi nchini kuendelea kujituma ili Taifa la Tanzania lizidi kukuwa kiuchumi.
Kuhusu mishahara ya wafanyakazi, Rais Samia alisema kuwa mwaka 2022 Serikali ilipandisha mishahara kwa asilimia 23 ambapo si kila mfanyakazi alinufaika nayo na hivyo lengo lilikuwa kuwainua wafanyakazi wa kima cha chini.
Vilevile, Serikali ilipandisha posho za wafanyakazi na walionuifaika ni wafanyakazi wenye mishahara mikubwa kwa kuwa hawakunufaika na ongezeko la mishahara la asilimia 23.
“Mwaka huu kuna upandisha wa viwango vya posho na Serikali imejiandaa kupandisha madaraja, vyeo, pamoja na vyeo vya mserereko vitakuwepo kwa ambao hawakupata mwaka jana. Lakini niseme pia kuna nyongeza za mishahara za mwaka ambazo kwa muda mrefu zilikuwa zimesitishwa nikaona mwaka huu nizuridishe, kwa hiyo wafanyakai wote mwaka huu mbali ya niliyoyasema kuna nyongeza za mishahara ya kila mwaka na tutaanza mwaka huu” Alisisitiza Rais Samia.