Ukosefu wa ukwasi wa kutosha uliokuwa unaikabili Benki M umesababisha mali na madeni yake kuhamishiwa katika Benki ya Azania Ltd, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya BoT kubaini kuwa benki hiyo imetetereka na kujikuta ikiwa chini ya kiwango cha ukwasi unaohitajika kwa mujibu wa sheria za benki wa Sh bilioni 15, kiwango ambacho kinatakiwa kulinda amana ya benki husika.
Kutokana na hali hiyo, inaelezwa kuwa Benki M ilikuwa imefikia hatua ya kushindwa kulipa madeni yake.
Naibu Gavana wa Benki Kuu, Bernard Kibese, amewaambia wanahabari kwamba kabla ya kufikia uamuzi huo wamefanya mikutano ya mara kwa mara na uongozi wa Benki M ili kupata ufumbuzi lakini jitihada hizo hazikuzaa matunda.
Kibese amesema Benki M ilipewa muda wa kutosha ili kurekebisha hali hiyo na kwamba Agosti 2, mwaka jana baada ya hali ya ukwasi wake kuzidi kushuka, BoT iliamua kuiweka benki hiyo chini ya uangalizi kwa siku 90.
Hata hivyo muda huo haukutosha na kwamba Novemba 2, mwaka jana waliiongeza muda mwingine wa siku 60 lakini ndani ya kipindi hicho suluhisho halikupatikana.
“Kama mnavyojua, sheria ya fedha imeipa Benki Kuu ya Tanzania mamlaka ya kusimamia shughuli zote za fedha nchini. Kutoa leseni kwa benki na taasisi za fedha hilo ni jukumu letu, hivyo tunautangazia umma wa Watanzania kuwa mchakato wa kupata ufumbuzi juu ya Benki M umekamilika,” amesema Kibese.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba Benki M, ilipewa leseni ya kutoa huduma za kibenki mwaka 2008, ikiwa na jumla ya matawi matano na mtaji wa Sh trilioni 1.
Matawi hayo yakiwa matatu Dar es Salaam, Mwanza na Arusha.
Kutokana na tatizo la ukwasi linaloikabili benki hiyo, BoT imeamua kuhamisha mali na madeni yake kwenda Benki ya Azania.
Kinachoandaliwa kwa sasa ni taratibu za kisheria za kuhamisha mali na madeni hayo kwenda Benki ya Azania.
Amesema wateja wenye amana na wadaiwa wa Benki M watapewa taarifa kuhusu kuanza kupata huduma kupitia Benki ya Azania.
Kibese amesisitiza kwamba wale wenye mikopo wanatakiwa kuendelea kulipa mikopo yao kulingana na mikataba yao, na kwamba BoT wanalisimamia hilo kwa ukaribu.
Kwa mujibu wa BoT, baada ya uamuzi huo, mtaji wa Azania unatarajiwa kukua na kufikia kiasi cha Sh bilioni 164, kiwango ambacho ni cha juu kwa mujibu wa sheria za mitaji ya kibenki ambacho ni Sh bilioni 15.
Hata hivyo, Naibu Gavana Kibese, amesema pamoja na baadhi ya benki kushindwa kutoa huduma, kitendo hicho hakiathiri uchumi, kwani uchumi wa nchi unaimarika na kwamba zinazofanya uchumi huo kuimarika ni taasisi za kifedha ambazo wanazipigania ili zizidi kuimarika.
“Ndiyo maana Benki Kuu ipo pale kuvisimamia hivi vyombo vya fedha. Benki inapoonekana kutetereka, Benki Kuu inaingilia kati kulinda amana za wateja,” amesema.
Pamoja na Benki M kuonekana kumiliki mali zenye thamani ya Sh trilioni 1, kwa miaka 10 iliyopita, alisema kiasi hicho kilikuwa ni mali peke yake ‘asset’ na si ukwasi ‘liquidity’.
Hivyo, kinachoifanya benki yoyote kukua si mali ‘asset’ bali ni ukwasi ambao hutumika kwenye ukopeshaji, kutokana na hali hiyo, Benki M haikuwa na uwezo wa kulipa madeni kwa sababu ilikuwa haina uwezo wa kuzalisha fedha zake kupitia mikopo.
Ukwasi wa benki unaweza ukatetereka ndani ya siku moja, hivyo Benki Kuu huwa inafanya juhudi mbalimbali ili kuzinusuru benki zisikumbwe na tatizo la kuishiwa ukwasi.
“Benki Kuu inaingilia kati kumnusuru mteja ili benki za biashara wasitumie fedha za wateja kulipa madeni, yaani tusipoingilia, wanaweza kutumia kile kilichowekwa benki kama amana. Ili benki isifike hapo, ndiyo maana Benki Kuu tunaingilia kati,” amesema.
Hata hivyo, wamiliki wa Benki M, ‘shareholders’ wamepewa siku 7 kufika BoT ili wafanye makubaliano na kujieleza namna gani watalipa madeni wanayodaiwa.
Kwa mujibu wa Naibu Gavana Kibese, wamiliki wenye mali katika benki yoyote wanaweza kukopeshana mle mle ndani ya benki, hivyo kwa utaratibu huo wamiliki wote wa Benki M wanatakiwa kueleza ni kwa namna gani watalipa madeni hayo.
Amebainisha kuwa wakati Benki M, mali na mtaji wake vinapata uamuzi wa kuhamishiwa Benki ya Azania, imehama na madeni ya Sh. bilioni 618, lakini Naibu Gavana huyo anabainisha kwamba hilo halina madhara kwa benki hiyo kwa sababu ni lazima yalipwe.
Amewaondoa shaka wananchi wote na kuwasihi waziamini shughuli za kifedha zitakazofanywa na Benki ya Azania na kwamba mkurugenzi mkuu wa benki hiyo atakapokuwa amekamilisha makabidhiano atafungua milango kwa wateja wote wa Benki M kuanza kuhudumiwa. Amesema lengo la kufanya hayo yote ni kutaka kumlinda mteja.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Posta Tanzania (TPB), Sabasaba Moshingi, ambaye benki yake ilipata fursa kama hiyo iliyotolewa kwa Benki ya Azania, amesema ni jambo jema lililofanywa na BoT la kuhamisha mali na mtaji wa Benki M kwenda Benki ya Azania.
Amesema uamuzi huo una faida kwa uchumi wa nchi kuliko ambavyo benki hiyo ingeachwa ifilisike na kuwekwa chini ya mfilisi.
Moshingi amesema uamuzi huo utakuwa na changamoto zake, na kwamba Benki ya Azania itaweza kuzimudu kwa sababu kinachoangaliwa zaidi ni imani ya wateja wa Benki M kuiamini na kuendelea kuweka amana zao.
Hata hivyo, haoni kama kuna kikwazo chochote ambacho kitasababisha shughuli za kibenki za Benki M kukwama wakati zikifanywa na Benki ya Azania, kwani uzoefu wa TPB baada ya kupokea shughuli za Benki ya Wanawake (TWB) na Benki ya Twiga (Twiga Bancorp) zilizokumbwa na hali kama ya Benki M, unaonyesha bado benki hizo zinafanya vizuri katika biashara.
“Sisi TPB baada ya kuzipokea Benki ya Wanawake na Benki ya Twiga, ule mtiririko wa kuingiza na kutoa amana katika benki yetu umekuwa mkubwa.
“Kwa mantiki hiyo, ‘inflow’ na ‘outflow’ ya biashara yetu inaendelea kuwa nzuri na kukua,” amesema Moshingi.
Kuhusu mtaji wa Benki M kuwa mkubwa kuliko uwezo wa Benki ya Azania, amesema kinachoangaliwa ni uwezo wa benki kuendesha shughuli zake bila kuathiri amana za wateja wake.
Amesema kwa sababu Benki M inamiliki mtaji mkubwa, kitendo cha kuhamishia shughuli zake katika Benki ya Azania kitasababisha Benki ya Azania ikue kwa kasi na kuwa miongoni mwa benki kubwa hapa nchini.