Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (kulia), akisikiliza maelezo ya huduma za uwezeshaji na uwekezaji zinazotolewa na Benki ya NMB kutoka kwa Mkuu wa Idara ya Biashara za Serikali wa benki hiyo, Vicky Bishubo (wa pili kushoto), wakati kiongozi huyo alipotembelea banda la NMB kwenye Maonyesho ya Viwanda na Biashara na Kongamano la Uwekezaji mkoani Pwani hivi karibuni.

Benki kubwa mbili nchini zimetenga mabilioni ya shilingi kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano na zimesema zimejipanga vizuri kuchangia kikamilifu ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Moja ya benki hizo, NMB, imesema imetenga zaidi ya Sh bilioni 700 kwa ajili ya kusaidia miradi ya kimkakati inayoendeshwa na serikali. Benki nyingine iliyobainisha azima yake ya kusaidia miradi hiyo ni CRDB.

Wakizungumza hivi karibuni mkoani Pwani, viongozi waandamizi wa benki hizo walisema taasisi zao zina fedha za kutosha kushiriki katika mchakakato mzima wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Benki hizo tayari zinashiriki kikamilifu katika miradi kadhaa mikubwa ya kimkakati. Pia zimetoa mikopo na huduma nyingine za kifedha kwa wadau na sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi wa viwanda.

Miradi iliyonufaika na uwezeshwaji wa benki hizi ni pamoja na Mradi wa Umeme wa Nyerere, Mradi wa Treni ya Umeme (SGR), usambazaji wa umeme vijijini kupitia REA, Ubungo Interchange, ujenzi na upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam na ujenzi wa Uwanja mpya wa Ndege wa Kimataifa Dar es Salaam (Terminal 3).

Wakizungumza wakati wa Maonyesho ya Viwanda na Biashara na Kongamano la Uwekezaji mkoani Pwani hivi karibuni, viongozi wa benki hizo walisema taasisi zao ziko imara kifedha na zina uwezo mkubwa kulihudumia taifa na uchumi wake kwa ujumla.

Vicky Bishubo, Mkuu wa Idara ya Biashara za Serikali wa NMB, amesema tayari wametenga zaidi ya Sh bilioni 700 kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa miradi ya kimkakati. 

“Benki yetu iko tayari kuwahudumia wawekezaji wakati wowote na mahali popote kwa hiyo tunawakaribisha kuja kupata huduma zetu bora. Sisi tuko tayari kushirikiana na yeyote kujenga uchumi wa viwanda,” Bishubo alimwambia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipotembelea banda la benki hiyo.

“Tuna mtaji wa zaidi ya Sh bilioni 700 maalumu kwa ajili ya miradi mikubwa ya serikali na wawekezaji wengine ambayo inatuwezesha kama benki kutoa huduma za kifedha kulingana na mahitaji,” Bishubo alisema kwenye wasilisho lake kwenye kongamano la uwezeshaji na kuongeza:

“Benki ya NMB ina historia ya kuhudumia miradi mikubwa ya kimkakati ya serikali kama: REA – NMB imetoa dhamana zenye thamani ya Sh bilioni 44 pamoja na kutoa mikopo mbalimbali kwa makandarasi. Tumewezesha TANESCO kununua vifaa muhimu kama mita na nguzo za umeme kwa kutumia Letters of Credit (barua fungani) zenye thamani ya Sh bilioni 54.” 

Akiwa kwenye banda la Benki ya CRDB, waziri mkuu aliwahimiza wakopeshaji nchini kuhakikisha wanatoa mikopo kwa riba nafuu. Ofisa Mkuu wa Biashara wa benki hiyo, Dk. Joseph Witts, amesema tayari hilo linafanyika na kuongeza kwamba benki yao ina pesa za kutosha kuwakopesha wawekezaji wa aina zote.

Ameongeza kusema kwamba benki hiyo ilikuwepo kwenye maonyesho hayo ili kuonyesha inavyoshiriki kwenye uwekezaji na utekelezaji wa miradi ya kimkakati.

“Tunachangia kwa kiasi kikubwa kwenye uwekezaji hasa kwa kutoa mikopo na huduma nyingine za kifedha kwa wadau na sekta mbalimbali kama kilimo, biashara na madini. Tuko hapa kwa ajili ya wawekezaji na pesa za kuwakopesha zipo za kutosha,” Dk. Witts alimwambia waziri mkuu.

Katika hotuba aliyoisoma wakati wa Kongamano la Fursa za Uwekezaji mkoani Pwani kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela, Dk. Witts aliwahimiza wawekezaji na wafanyabiashara kwa ujumla kuitumia benki hiyo na huduma zake mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa taifa. 

Amesema tayari benki hiyo imekwisha kutoa mikopo yenye thamani ya Sh trilioni 3.18 zinazoifanya CRDB kuwa mojawapo ya wakopeshaji wakubwa nchini.