Benedict Mapunda (Rasha) ndiye aliyegundua kuungua moto kwa mgodi wa madini ya makaa ya mawe Ngaka uliopo Wilaya ya Mbinga Mkoa wa Ruvuma mwaka 2006.

Diwani wa Kata ya Raunda Edmund Nditi

Madini ya Makaa ya mawe Ngaka

Na Albano Midelo

Benedict Mapunda (Rasha) mwenye umri wa miaka 66 mkazi wa kijiji cha Ntunduwaro ndiye aliyegundua kuungua moto kwa mgodi wa madini ya makaa ya mawe Ngaka uliopo Wilaya ya Mbinga Mkoa wa Ruvuma mwaka 2006.
Inakadiriwa moto huo uliowaka kwenye mgodi huo mwaka 2006 uliteketeza
tani milioni sita za makaa ya mawe ndizo.Inaaminika Moto huo ulianza
kuwaka tangu Septemba mwaka 2003.
Inaaminika Moto huo usingezimwa mapema ungeweza kuvuka hadi Wilaya
jirani ya Makete Mkoa wa Njombe na kuunguza Madini ya Mchuchuma
ambayo yapo Kilomita 32 kutoka Moto ulipokuwa unawaka katika Wilaya
ya Mbinga.
Mgodi huo hivi sasa unaingiza mabilioni ya fedha kwa Kampuni binafsi ya
uchimbaji wa madini hayo ya TANCOAL na serikali inalipwa kodi na ushuru
kutokana na kazi ya uchimbaji na usafirishaji wa madini hayo ilioanza tangu
mwaka 2011.
Hata hivyo uchunguzi ambao umefanywa katika Kijiji cha Ntunduwaro
kilichopo ndani ya mgodi wa Ngaka,umebaini Mzee Rasha anaishi maisha
ambayo hayastahili kulingana na uzalendo wake wa kushiriki kuokoa
rasilimali adimu ya madini ya makaa ya mawe kwa nchi yake ambayo
yalikuwa yanateketea kwa moto ardhini kwa miaka kadhaa.
“Pengine kama sio ujasiri na uzalendo wa mzee huyo kugundua moto na
kutoa taarifa kwa vyombo vya serikali,madini hayo yangeendelea kuteketea
kwa miaka mingi’’,anasema Joseph Ngahy Afisa Mtendaji wa Kijiji cha
Ntunduwaro
Mzee Rasha anasema aligundua moto ambao ulikuwa umewaka kwa
miaka kadhaa,ukiteketeza madini ya makaa ya mawe chini ya ardhi katika

eneo hilo.Mzee huyo amepewa jina la GPS kutokana na utalaam wake wa
kutambua alama(becon) zilizowekwa katika eneo la mgodi.
Akizungumzia namna alivyogundua moto huo,Rasha anasema mwaka
2006 alikwenda kuchunga ng’ombe porini katika eneo la Ngaka ambapo
alipata harufu kali mbele yake ya kama mkaa unaungua lakini hakuweza
kuuona.
“Niliamua kusogea mbele zaidi nikaona udongo umegeuka rangi kama
tofali zinachomwa,nirudi kijijini ili kutoa taarifa kijijini,taarifa ikaenda katani,
tarafani, wilayani, mkoani hadi ngazi ya Taifa’’,anasema Rasha.
Anasema baada ya taarifa kutolewa watu wa wazima moto ngazi ya Mkoa
na Taifa walifika lakini kwa kuwa makaa hayo yalikuwa yamewaka miaka
mitatu mfululizo huku yakinyeshewa mvua,ilikuwa ni vigumu moto huo
kuzima.
Watalaam wa zimamoto kwa kushirikiana na Mzee Rasha waliamua
kutumia mbinu ya kitaalam kuchimba mashimo marefu ya meta kumi
kwenda chini kuzunguka eneo lote lililoungua,ili kutenganisha eneo ambalo
limeungua na ambalo bado moto haujafika.
“Wataalam hao walikodi mashine maalum ya kuchimba na kuweka
mchanga eneo hilo ambalo mimi nilikuwa nakagua kila siku hatimaye moto
ulifanikiwa kuzima baada ya miezi mitatu’’,anasisitiza Rasha.
Hata hivyo anasema katika kipindi chote cha miezi mitatu alikuwa
anasimamia kuhakikisha moto huo unazima kazi ambayo anasema
aliifanya kwa uzalendo bila kulipwa kitu chochote na kwamba watalaam
baada ya kuchimba na kuweka mchanga,walirudi na kazi ya uangalizi hadi
moto ulipozima aliachiwa pekee yake.
Anasema baada ya kuzima moto na kuanza kazi ya utafiti wa makaa ya
mawe mwaka 2008,Kampuni ya TANCOAL ilimchukua tena Rasha kama
kibarua kufanya utafiti kuanzia eneo ambalo liliwaka moto na maeneo
mengine ya mgodi kazi ambayo anasema aliifanya kwa uzalendo wa hali
ya juu hadi walipomaliza utafiti na kuanza rasmi uchimbaji wa madini hayo
mwaka 2011 na kwamba hadi sasa bado anaendelea kufanyakazi katika
kampuni hiyo.

“Changamoto nilionayo nimechelewa sana kuajiriwa na kampuni hii licha ya
kufanyakazi ngumu katika umri wa uzee,sasa wameniajiri wakati umri
umepita nina miaka 66 nilitakiwa kustaafu,lakini kampuni imeniachia
nifanyekazi walau nipate hela nzuri ya uzeeni’’,anasema Rasha.
Anasema mwanzoni wakati shughuli za kuzalisha makaa zinaanza na yeye
akifanyakazi ya kibarua kwenye mgodi alikuwa na matumaini kwamba
pengine watendaji wa mgodi watatambua mchango wake wa kushiriki
kuokoa rasilimali ambayo ilikuwa inaendelea kutekea kwa moto.
Akizungumza kwa masikitiko Rasha anasema Kampuni ya TANCOAL
inazalisha maelfu ya tani za makaa ya mawe kila mwaka na kuuza ndani
na nje ya nchi ambapo anadai hakuna anayemwangalia kama alifanya kitu
kwa ajili ya Tanzania na kwamba hata ajira aliyopewa na Kampuni
amepewa kitengo ambacho anafanyakazi juani licha ya kuwa na umri
mkubwa.
Kaimu Meneja Mgodi wa Makaa ya mawe Ngaka Edward Mwanga
alipohojiwa iwapo anatambua mchango wa Rasha katika Kampuni
hiyo,anasema Kampuni ya TANCOAL inatambua mchango wa Rasha
kuanzia alipogundua moto wakati unaunguza mgodi,mchango wake katika
utafiti na sasa uchimbaji wa makaa ya mawe ndiyo maana hadi sasa licha
ya kuwa na miaka 66 bado Kampuni imeamua kuendelea kumwajiri na
kumtumia.
“Tunatambua mchango wa Rasha ndiyo maana hadi sasa yupo kwenye
ajira,yeye ni mzee wa umri wa kustaafu lakini bado yupo na anaendelea
kufanyakazi hivyo tunatambua mchango wake ndiyo maana tunaendelea
kumtumia,ni hazina kwenye Kampuni yetu’’,anasisitiza Mwanga.

Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Mbinga Mashariki Gaudence Kayombo
ambaye wakati moto unaunguza madini hayo alikuwa Mbunge alikaririwa
na vyombo vya habari akieleza kuwa sababu ya kuungua kwa makaa ya
mawe kulitokana na wawindaji haramu ambao huchoma Moto hovyo kwa
ajili ya kuwinda.
Historia inaonesha kuwa eneo la Mgodi la Ngaka liliwahi kuchimbwa
Makaa ya Mawe na Wajerumani Mwaka 1945 na Uchimbaji huo ulikoma
Mwaka 1953.

Utafiti uliofanywa mwaka 1952 ulibaini kuwepo kwa madini ya makaa ya
mawe tani Milioni 79,ambapo utafiti uliofanywa Mwaka 2001 ulibaini
kuwepo kwa madini ya makaa ya mawe kati ya tani Milioni 200 hadi milioni
4000 na kwamba makaa hayo yanatarajiwa kuchimbwa kwa zaidi ya miaka
50.

John Haule Mkazi wa Kijiji cha Ntunduwaro anasema,walitegemea
Kampuni ya TANCOAL itampa tuzo mzee Rasha kwa kazi ya kugundua
moto uliokuwa unaunguza rasilimali hiyo muhimu kwa uchumi wa
Tanzania.
Diwani wa Kata ya Ruanda Edmund Nditi anashauri mchango wa mzee
Rasha katika kuokoa rasilimali adimu ya makaa ya mawe ,ulitakiwa
kutambuliwa na Kampuni ya TANCOAL kwa kumweka katika kitengo kizuri
badala ya kuendelea kufanyakazi katika mazingira magumu.
“Mzee Rasha hata kama hana ujuzi ambao Kampuni walihitaji wakati
wanampa ajira,busara ingetumika mzee huyu kufanyakazi kivulini badala
ya kuendelea kufanyakazi juani,hasa kutokana na uzee alionao’’,anasisitiza
Nditi.
Hata hivyo Mwenyekiti wa serikali ya Kijiji cha Ntunduwaro John Nyimbo
anasema kuna mambo mema ambayo yamefanywa Kampuni ya
TANCOAL katika kijiji hicho ikiwemo kusaidia madawati 80 yenye thamani
ya karibu sh. Milioni1.2,ujenzi wa choo cha kisasa cha wanafunzi,mipira na
jezi za michezo katika shule ya msingi Ntunduwaro.
Rasilimali adimu kama madini,gesi na mafuta zinatakiwa kuwanufaisha
wananchi wa maeneo husika na taifa kwa ujumla wake.Lakini pia Wazee
ambao wamelitumikia Taifa kwa uzalendo kama Mzee Benedict Mapunda
ni vema jamii kuwaenzi kwa kuthamini mchango wao katika ujenzi wa