Mshambuliaji wa Ubelgiji Romelu Lukaku anatarajiwa kuikosa mechi muhimu katika Kombe la Dunia dhidi ya England Alhamisi.
Mechi hiyo itakayochezewa mjini Kaliningrad inatarajiwa kuamua nani atamalizakileleni katika Kundi G.
Mchezo huo utaanza saa tatu saa za Afrika Mashariki.
Mshambuliaji huyo wa Manchester United mwenye umri wa miaka 25 aliumia kwenye kifundo cha mguu wakati wa mechi ya Jumamosi dhidi ya Tunisia ambayo walishinda 5-2.
Kocha wa Ubelgiji Roberto Martinez amesema Lukaku alipimwa na ikabainika kwamba hawezi kucheza dhidi ya England.
“Nafikiri itamchukua muda zaidi,” amesema Martinez.
Lukaku amefunga mabao manne Kombe la Dunia Urusi kufikia sasa, bao moja nyuma ya Harry Kane wa England.
Mataifa yote mawili tayari yamejihakikishia nafasi ya kucheza hatua ya 16 bora na yanatarajiwa kufanya mabadiliko kadha kwenye vikosi vyao.
Ikizingatiwa kwamba mataifa yote mawili yamefuzu, na yanaoshana nguvu kwa alama, tofauti ya mabao na mabao ambayo wamefunga pia, nidhamu ya wachezaji uwanjani huenda ikaamua nani atamaliza kileleni Kaliningrad iwapo watatoka sare tena. Aliyepata kadi nyingine ndiye atakayekuwa wa pili.
Iwapo watatoshana pia kwa kadi, huenda wakalazimika kuchagua kwa kuokota karatasi kutoka kwenye kasha kuamua nani atakuwa wa kwanza.
Mshindi wa kundi G atakutana na atakayemaliza wa pili Kundi H, na atakayemaliza wa pili akutane na mshindi Kundi H.