BEI ya mafuta ilipanda baada ya Iran kurusha makombora ya balistiki dhidi ya Israel na kuzua hofu ya mzozo mkubwa katika eneo la Mashariki ya Kati ambao unaweza kuvuruga usambazaji wa mafuta.

Wakati wa biashara Jumanne, kigezo hicho kilipanda kwa zaidi ya asilimia 5. Iran ni nchi ya saba kwa uzalishaji wa mafuta duniani, kulingana na Utawala wa Taarifa za Nishati wa Marekani, na mwanachama wa tatu kwa ukubwa wa shirika la wazalishaji wa mafuta la Opec.

Wafanyabiashara pia wanahofia kuongezeka kwa mzozo wa kijeshi katika eneo hilo kunaweza kuathiri usafiri wa meli kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz.

Njia hiyo ya meli – ambayo iko kati ya Oman na Iran – ni muhimu kwa biashara ya kimataifa ya mafuta na asilimia 20 ya bidhaa za ulimwengu zinapitia humo.

Wanachama wengine wa OPEC Saudi Arabia, UAE, Kuwait na Iraq pia hutuma mafuta mengi wanayouza nje kupitia Mlango huo wa Bahari.