DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Wetu
Kauli iliyotolewa bungeni jijini Dodoma wiki iliyopita kuhusu kutaka kutazamwa upya kwa utaratibu wa uagizaji wa mafuta ili kuleta ushindani sokoni, imepokewa kwa mitazamo tofauti.
Akichangia Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby, ameishauri serikali iruhusu wafanyakazi binafsi kuingia katika biashara ya mafuta tofauti na ilivyo sasa.
Shabiby analaumu mfumo uliopo sasa wa ununuzi wa pamoja (bulk procurement), akisema unatengeneza uwepo wa mianya ya ulaji miongoni mwa wajumbe wa kamati husika huku pia ukiua ushindani, hivyo kusababisha kupanda kwa bei ya mafuta.
Anasema kuna uwezekano kamati zinazohusika na ununuzi wa mafuta zikawa zinajitengea kiasi fulani cha fedha katika kila kiwango cha mafuta watakayoagiza.
“Watu nchi hii wanakula pesa si mchezo! Nchi hii hutumia lita milioni 400 kwa mwezi. Sasa fanya hesabu kwenye ‘kikamati’ kinachotoa tenda ya kwenda kununua mafuta, wakiweka dola tano tano kwa mafuta watakayonunua watakuwa na shilingi ngapi?
“Hata wakisema waweke dola mbili mbili watakuwa na fedha nyingi,” anasema Shabiby, mwanasiasa mkongwe na mfanyabiashara mkubwa wa magari na hoteli.
Anasema kutokana na kila kitu sasa hivi kutazamwa katika sura ya fedha, wapo watu ambao kazi yao ni kupanga mipango ya kujipatia huku Bunge likielekezwa kupitisha sheria ambazo zinawanufaisha wachache.
Shabiby anaiomba serikali iruhusu kampuni binafsi ziagize mafuta ili kuleta ushindani wa bei sokoni kwa wafanyabiashara wa jumla na rejareja kuamua ama wanunue mafuta kutoka kwenye mfumo wa ‘bulk procurement’ au kuagiza wenyewe moja kwa moja kutoka nje ya nchi.
Shabiby anashauri kazi ya serikali kupitia taasisi kama EWURA na TBS kuwa waangalizi na wadhibiti wa viwango vya mafuta vinavyotakiwa pamoja na bei elekezi.
Amesema hoja kwamba serikali ikiruhusu mtu mmoja mmoja kuagiza mafuta kutakuwapo ukwepaji wa kodi hazina ukweli kwa sababu meli zote hushusha mafuta kwenye mita moja.
“Tangu mfumo wa ‘bulk procurement’ uanze kufanyakazi, mita inayopima kiwango cha mafuta kinachoingizwa nchini imekuwa ikifa mara nyingi toauti na awali. Hali hii hutengenezwa makusudi kuhalalisha wizi wa mafuta.
“Serikali inapaswa kuiamini TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) kwenye ukusanyaji wa kodi ya mafuta na endapo wafanyabiashara binafsi wakiruhusiwa kuagiza mafuta, bei zitashuka haraka,” amesema.
Shabiby anazilaumu kampuni za nje kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi kuhujumu soko la mafuta wakati lilipokuwa la ushindani, hasa kampuni za mafuta za Uarabuni na Urusi.
Anasema mgomo wa kampuni hizo ndio uliosababisha Bunge kusitisha watu binafsi kuagiza mafuta, badala yake ukapitisha mfumo wa ‘bulk procurement’.
Hoja yaungwa mkono
Ofisa mmoja mstaafu wa serikali mkazi wa Mapinga, Bagamoyo mkoani Pwani, Rafael Kalunguwala, anaunga mkono hoja ya Shabiby, akisema kuwa ‘ina mashiko’.
“Mfumo uliopo sasa ni kweli umeua upinzani kwa kuwa bei ya mafuta inabaki kuwa ile ile. Hii ni kwa sababu wafanyabiashara wote wananunua sehemu moja. Lakini kama kungekuwapo sehemu nyingine ya kununua, basi lazima bei zingetofautiana,” anasema.
Kalunguwala, mtaalamu wa takwimu, anasema serikali imekuwa haisikilizi ushauri inaopewa na wataalamu, akidai kuwa si sahihi kwa vyombo vinavyosimamia au kudhibiti biashara kutoza tozo kutokana na biashara husika.
“Hawa wanapaswa kulipwa kutoka kwenye mfuko mkuu wa serikali badala ya kutokana na vitu wanavyovidhibiti. Wakiachwa kujilipa kwa vitu wanavyovidhibiti watakuwa wakitamani bei iongezeke, kwa kuwa kiwango cha makusanyo yao pia kinaongezeka hata kama ni asilimia moja,” amesema.
Mwananchi huyo anashangaa mfumo kumtupa nje Kamishna wa Petroli na kumuacha bila kazi ya kufanya.
Hoja kinzani
Kwa upande mwingine, mfanyabiashara na mmiliki wa vituo vya mafuta wa Dar es Salaam, akiomba kutotajwa gazetini, anasema si vema uagizaji wa mafuta kuachwa mikononi mwa wafanyabiashara.
“Nishati hii ni muhimu sana. Ni nyeti na ni suala la usalama wa taifa. Ukiwaacha wafanyabiashara ndio wadhibiti, unaweza kujikuta unatumbukia hatarini kama wakiamua kugoma,” amesema.
Hata hivyo, ofisa mmoja wa wakala wa uagizaji mafuta kwa jumla, PBPA, aliyezungumza na JAMHURI, hakutaka kuzungumza kwa kina akiomba kupewa muda.
Mjadala huu unakuja wakati EWURA ikiwa imetangaza ongezeko la bei ya mafuta kwa mwezi Aprili, ikiwa ni ya juu kuwahi kutumika nchini.