Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads), inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam Awamu ya Nne (BRT 4) kuanzia Daraja la Kijazi (Sam Nujoma) – Mwenge – Maktaba ya Taifa (Posta) yenye urefu wa kilometa 13.5.

Akizungumza na wakazi jijini Dar es Salaam, Waziri Bashungwa amesema ujenzi wa miundombinu ya mabasi hayo unaendelea kuanzia Mwenge – Tegeta (Dawasa) yenye urefu wa kilometa 15.63.

Ujenzi huo unatekelezwa na wakandarasi wawili M/s China Geo Engineering na M/s Shandog Group Co. Ltd.

“Tunao wakandarasi wanaojenga barabara ya mwendokasi kuanzia Serena Hoteli kuelekea Mwenge na kutoka Mwenge kuelekea Ubungo (Daraja ya Kijazi), wakandarasi wako kazini na fedha zipo,” alisema Bashungwa.

Alimuagiza mkandarasi Sinohydro Corporation anayetekeleza ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Tatu (BRT 3) katika barabara ya Tanganyika Motors – DIT, Uhuru (Buguruni – Msimbazi) Bibi Titi na Shaurimoyo (Karume – Bohari) afanye kazi usiku na mchana ili akamilishe mradi huo kwa wakati kwa kuzingatia mkataba.

Aidha, Bashungwa alisema Tanroads wapo katika hatua ya manunuzi ya kumpata mkandarasi atakayejenga daraja la Mzinga na kufanya upanuzi wa barabara kuanzia Mbagala Rangi Tatu hadi Vikindu ili kupunguza foleni ya magari na kuondoa adha ya watumiaji wa barabara hiyo kwa wananchi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Amesema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025, serikali imejipanga kufanya upanuzi wa njia nne barabara ya Mwaikibaki (Morocco – Africana) yenye urefu wa kilometa 11.7, itakayoanzia Morocco kuelekea Africana kupitia Kawe ya Chini, Kawe – Lugalo pamoja na kipande cha Mwalimu Nyerere cha kwenda Rose Garden.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameiomba serikali iingie ubia na sekta binafsi kwa ajili ya ujenzi wa barabara na madaraja ya kulipia tozo kama ilivyo katika Daraja la Nyerere ili fedha zinazopatikana zitumike katika ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara na madaraja.

Please follow and like us:
Pin Share