Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, ameeleza Serikali itahakikisha inakamilisha na kusimamia ujenzi wa kipande kilichobaki cha barabara inayoelekea Msangani kwa kiwango cha lami, ili kurahisisha usafiri na usafirishaji.

Kutokana na hilo amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoani Pwani, injinia Baraka Mwambage kuainisha madeni yanayodaiwa na mkandarasi ili Serikali ishughulikie haraka.

Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa shule ya sekondari katika Kata ya Msangani, ambayo itagharimu sh. milioni 528, wilayani Kibaha, katika ziara yake ya siku tano mkoani Pwani, Bashungwa alisema inaendelea kuboresha na kusimamia miradi ya barabara ili kufungua milango ya kiuchumi na maendeleo.

Bashungwa alisisitiza kuwa ,serikali itahakikisha mkandarasi analipwa kwa wakati ili kazi ziendelee .

Kadhalika Waziri huyo alitoa agizo kwa wakandarasi wanaopewa kandarasi za miradi ya serikali kuhakikisha wanazingatia masuala ya usalama kazini kwa mafundi ujenzi ili kuepusha ajali na kuhakikisha wanakuwa salama.

Vilevile, alieleza kuwa serikali inaendelea na mchakato wa ujenzi wa barabara sita kuelekea Morogoro, huku ikiangalia namna ya kushirikiana na wadau na wawekezaji ili kuboresha miundombinu ya barabara hiyo.

Pia aliongeza kuwa haitakuwa matumizi mabaya ya fedha kuwekeza katika kuboresha barabara kuanzia Mbagala Rangi Tatu hadi Mwanambaya.

“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya kwa kutenga fedha nyingi kujenga miradi na miundombinu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Daraja la Wami ambalo limefungua milango ya kiuchumi na maendeleo,” alifafanua Bashungwa.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakar Kunenge, aliishukuru serikali kwa kupeleka kiasi cha shilingi trilioni 1.3 kwa ajili ya kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo.

Hata hivyo, alieleza kuwa maboresho ya barabara mkoani Pwani yatafungua uchumi, hasa barabara kubwa ya Morogoro, ambayo ni muhimu kwa uchumi wa taifa, lakini kipande cha Mlandizi – Chalinze ni changamoto hasa kero ya foleni.

“Barabara hii ni uti wa mgongo wa uchumi wetu, Tunaiomba serikali ifanye juhudi kulitatua tatizo la kipande cha Mlandizi – Chalinze,” na barabara ya Makofia – Mlandizi – Mloka na ujenzi wa kiwango cha lami barabara ya Kiluvya hadi Kisarawe”

Mkuu wa wilaya ya Kibaha,Nikkison Simon alieleza ,katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan shule 20 zimejengwa wilayani Kibaha ikiwemo shule za sekondari 10 na shule za msingi 10.

Katika ziara yake, Bashungwa pia alikagua na kuweka jiwe la msingi ujenzi wa mabweni,vyoo na madarasa manne ya Shule ya Sekondari ya Viziwaziwa Kibaha Mjini, kisha akakagua soko la Halmashauri na Hospitali ya Wilaya ya Kibaha.

Please follow and like us:
Pin Share