Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Kiteto
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMIA), Innocent Bashungwa ameagiza watumishi watano kusimamishwa kazi na kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa tuhuma za kuisababishia hasara Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara.
Bashungwa ametoa maagizo hayo wakati wa kuhitimisha ziara yake wilayani Kiteto mkoani Manyara kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Watumishi alitoa agizo la kusimamishwa ni aliyekuwa mweka hazina Nassoro Mkwanda na mhasibu wa mapato, Christopher Mwigani, Kaimu mweka hazina, Hadija Boffu na kaimu mkuu wa kitengo cha manunuzi, Nakaji Mollel na kaimu mwanasheria wa halmashauri Joseph Hoza.
Kati ya hao Nassoro Mkwanda aliyehamishiwa Mafinga Mji, Khadija Bofu aliyehamishiwa Songea Manispaa na Christopher Mwigani ambaye amestaafu wote wanatuhumiwa kuhamisha fedha na kuweka kwenye akaunti ya amana isiyo na vifungu vya matumuzi na wanatakiwa kurejeshwa kwenye Halmashauri hiyo kujibu tuhuma hizo.
Pia, Kaimu Mkuu wa kitengo cha manunuzi Nakaji Melateki Mollel ambaye aliidhinisha Sh.milioni 191.9 kwa ajili ya kununua vifaa vya ujenzi bila kufuata taratibu sambamba na Sh.milioni 235.5 alizolipa mkandarasi wa kuchimbia visima bila kuzifanyiwa tathimini na Khalfan Hinga aliyetoa kazi hiyo bila kufanyika tathimini.
Amekemea tabia ya kuwahamisha watumishi waliofanya vibaya kwenye halmashauri na kusisitiza kuwa atawafuata popote walipo.