Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Rufiji

SERIKALI kupitia wizara ya Ujenzi imemuagiza Mkandarasi, Kampuni ya China Railways Seventh Group Ltd (CRSG) anaejenga ujenzi wa barabara ya Utete -Nyamwage yenye km.33.7, kuacha mzaha na kusuasua ambapo hadi sasa Ujenzi umefikia asilimia 7 tangu mwaka wa utekelezaji 2022/2023-2024/2025.

Aidha imemuagiza Mkandarasi huyo kuhakikisha anafikisha vifaa vya ujenzi kwa asilimia 107 kutoka asilimia 67 ili kuendelea na ujenzi kwa kiwango kinachotakiwa.

Akiongea na wananchi wa kata ya Chemchem, wilayani Rufiji Mkoani Pwani wakati wa muendelezo wa ziara yake maalum, Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa alimtaka mkandarasi CRSG kuacha mzaha katika tenda anazopatiwa na ahakikishe anatekeleza mradi kulingana na mkataba wake.

Vilevile Bashungwa amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania TANROADS Mkoani Pwani injinia Baraka Mwambage, kusimamia mikataba ya wakandarasi wa Ujenzi wa barabara bila kuwachekea.

“Taarifa ya utekelezaji wa mradi inaeleza mkandarasi ana vifaa asilimia 67 wakati anatakiwa vifaa site kwa asilimia 107 “‘nitahakikisha narudi hapa kufanya ukaguzi”

Aidha Bashungwa alifafanua, Serikali imemuamini mkandarasi CRSG kutekeleza miradi ya Ujenzi wa barabara Mara,Katavi,Pwani na Dar es salaam lakini amekuwa anasuasua suala ambalo anahitaji kubadilika.

Alieleza, Serikali imedhamiria kusimamia barabara ya Nyamwage hadi Utete ili kuleta mageuzi ya kiuchumi Utete na mkoa kijumla.

“RAIS Samia Suluhu Hassan ana mapenzi makubwa kuinyanyua, Rufiji ilikuwa nyuma lakini kwa kipindi cha miaka minne maendeleo makubwa yanaonekana”alisisitiza Bashungwa.

Pamoja na hayo Bashungwa, aliahidi kushughulikia suala la fidia kwa wananchi waliopisha sehemu ya Ujenzi wa barabara hiyo na atahakikisha analeta majibu juu ya uhakika wa fidia hizo.

Katika ziara hiyo Bashungwa alikagua ukarabati wa hospital ya Utete iliyojengwa tangu mwaka 1967 ,kuangalia utekelezaji wa fedha za Serikali zimavyofanyiwa kazi.

Awali Meneja wa Tanroads Pwani mhandisi Baraka Mwambage, alieleza barabara ya Utete -Nyamwage ina urefu wa km.33.7, mkandarasi anasuasua 2024 July mkandarasi kupitia wataalam wake walieleza wamefikia asilimia 7.

Alieleza kuanzia sasa Tanroads itamsimamia mkandarasi afikie asilimia 4.1 kwa mwezi ili kufidia muda alioupoteza.

Mwambage alimhakikishia Waziri Bashungwa kuwasimamia wakandarasi usiku na mchana ili kutekeleza miradi kwa wakati.

Mkuu wa mkoa wa Pwani alhaj Abubakar Kunenge, alieleza kutokana na jiografia km 354 inajengwa kuanzia Chalinze,Magindu hadi Utete.

Kunenge alimshukuru Rais Samia, kwa kupeleka mabilioni ya fedha kutekeleza miradi ya Ujenzi wa barabara na kuifungua Rufiji na mkoa huo.

Diwani wa kata ya Chemchem ,Masudi Ally Nanganje anasema barabara ya Nyamwage hadi Utete yenye km 33.7 eneo la kata hiyo inapitia km 22.

Aliomba Serikali kuharakisha kuleta majibu kwa wananchi waliofanyiwa tathmini ili kupata malipo yao kwa wakati.

Ujenzi wa barabara ya Nyamwage hadi Utete kwa kiwango cha lami na Daraja la Mbambe zitagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 bila VAT ili kuboresha sekta ya usafiri na usafirishaji.

Zabuni ya mradi huo ilitangazwa Sept mwaka 2022 na kufunguliwa November 2022 na baada ya tathmini kukamilika ilishinda Kampuni ya CRSG Bil 43.4 bila VAT na itajengwa kwa muda wa miaka miwili.