Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa ameishukuru Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa katoa zaidi ya shilingi bilioni 1.27 kujenga vyumba vya madarasa, vyoo na miundombinu mingine ya shule za msingi katika halmashauri ya wilaya Karagwe.

Bashungwa ameeleza hayo katika mwendelezo wa ziara ya jimboni ya Kuongea na Wananchi na kukagua miradi ya maendeleo katika Kata za Chonyonyo, Chanika, Rugera na Kihanga .

Amempongeza Rais Dkt. Samia kwa kuendelea kuboresha elimu nchini ambapo ameeleza kuwa katika mwaka huu wa 2023 amewezesha ujenzi wa vyumba vya madarasa, shule mpya, matundu ya vyoo, majengo ya utawala vyenye Jumla ya Shilingi Bilioni 1.27 katika elimu ya awli na msingi pekee.

Pia, Bashungwa amesema halmashauri ya wilaya Karagwe imepokea kiasi cha shilingi Bilioni 1.1 kwa ajili ya kukamilisha miundombinu iliyosalia katika ujenzi wa shule ya Wasichana ya Mkoa ambapo awali ilipokea kiasi cha shilingi bilioni 3.

“Serikali imejenga madarasa 11 Katika shule ya Sekondari Ruicho yaliyogharimu kiasi cha shilingi milioni 220 pamoja na ujenzi wa maabara mbili ambazo zimekamilika kwa gharama ya milioni 60” amesema Bashungwa

Aidha, Bashungwa amesema Katika Sekta ya Miundombinu ya Bararabara zaidi ya Shilingi Bilioni 1.5 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi na ukabarabari wa barabara pamoja na kurekebisha maeneo korofi ya barabara katika kata za chonyonyo na Chanika.

“barabara zitakazokarabatiwa ni barabara ya Nyakahita – Chanika, barabara ya Runyaga – Masheshe – Katwe, barabara ya Chanika – Rwakiro – Rwambaizi, barabara ya Chanika – Ahakayenje – Rukole, barabara ya Chonyonyo- Karushaja – Omurusimbi, barabara ya Rukole – Kigarama na Barabara ya Rukole – Ahakayenje – Chanika” amesema Bashungwa.

Kadhalika, Bashungwa ameeleza barabara barabara zilizokuwa korofi ambazo tayari zimekarabatiwa ni pamoja na barabara ya Kanyableza – Runyaga, barabara ya Runyaga – Masheshe – Katwe, barabara ya Kakiro – Katwe – Kibugu na barabara ya Chonyonyo – Omukimeya zilizogharimu Shilingi milioni 377.6.

Vile vile, Bashungwa amesema shilingi bilioni 6.7 zimetoalewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji vya Omukimeya, Omurulama, Ruzinga, Runyaga, Ruhanya na Chanika ambayo ikamilika itahudumia wananchi zaidi ya 12,989 katika kata za chanika na Chonyonyo.