Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, ameingia katika mgogoro na wanachama wa Chama cha Ushirika wa Wakulima wa Chai Lupembe kutokana na hatua yake ya kuvunja bodi ya chama hicho na kuteua watu wa kusimamia uendeshaji wa shamba la chai la ushirika huo. 

Wanaushirika huo wameliambia JAMHURI kuwa kitendo cha Naibu Waziri Bashe kuivunja bodi hiyo ni kinyume cha sheria, bali kuna hisia kuwa hatua hiyo inalenga kukwamisha juhudi za ushirika huo kuhakikisha serikali inarejesha hisa zake ndani ya chama hicho ambazo ziliuzwa miaka kadhaa iliyopita bila kufuata utaratibu kwa kampuni binafsi.

Aidha, Bashe aliagiza kuwekwa ndani kwa viongozi kadhaa wa ushirika huo ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili. Watu 11 walikamatwa na kuwekwa ndani kwa agizo hilo. Watano wameachiwa kwa dhamana.

Bashe alitoa maagizo hayo Januari 11, mwaka huu katika ukumbi wa kiwanda cha chai Lupembe akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher ole Sendeka, pamoja na Yusuph Mulla, ambaye ni Mkurugenzi wa Dhow Enterprises (EA). Dhow Enterprises inamiliki sehemu ya hisa katika ushirika huo. 

Kupitia kwa Wakili wao, Rugemeleza Nshala, wanachama hao wamemwandikia barua Naibu Waziri Bashe wakimtaka afute mara moja amri yake ya kuvunja bodi ya Lupembe Farmers Cooperative Joint Enterprises Limited pamoja na kuamuru kuachiwa mara moja kwa viongozi wote wa bodi hiyo na wanachama wake waliowekwa ndani. 

Katika barua hiyo ya Januari 13, mwaka huu ambayo JAMHURI limeiona, wanachama hao wanamtaka Bashe awaondoe mara moja watumishi aliowapa mamlaka ya kuendesha shamba la chai la Lupembe, pia aache ‘kuipendelea’ Kampuni ya Dhow Mercantile (EA) Limited na kuwasafisha viongozi wa Lupembe Farmers Cooperative Joint Enterprises Limited.

Wanachama hao wanasema iwapo Bashe atashindwa kufanya hivyo watalazimika kuchukua hatua zipasazo za kisheria ikiwa ni pamoja na kumburuza mahakamani kudai nafuu ya stahili. 

Pamoja na hayo, barua hiyo inamtaka Bashe kulipa fidia ya jumla ya Sh bilioni 1.35, ikiwa ni Sh milioni 150 kwa kila mmoja kwa watu tisa ambao walikamatwa na kuwekwa ndani kwa maagizo ya naibu waziri huyo. Hata hivyo Mwanasheria wa wanachama wa Lupembe, Nshala, anasema wamemshitaki Bashe binafsi, si serikali, kwa kuwa wanaamini serikali haikumtuma kuvunja sheria. 

Waliokamatwa na kuwekwa ndani ni: Andrew Ulungi, ambaye ni mwenyekiti wa bodi, pamoja na wajumbe wa bodi Obali Mhonda, Lason Malekela, Pius Mnyalape, Yoram Ligungwine na Gloria Ulime. Pia wamo Bossy Mbanga ambaye ni mwanachama wa Ushirika wa AMCOS, Henrick Lupembe, mjumbe wa mkutano mkuu na mjumbe mwingine wa bodi, Jachindus Mgodamkali.

Watu hao wanadai fidia kwa kuwadhalilisha na kuwaweka ndani, jambo lililosababisha kupoteza uhuru wao wa kikatiba.  

JAMHURI limeambiwa baada ya kuivunja bodi hiyo ya chama cha ushirika, Bashe akapeleka watumishi wawili wa serikali kusimamia shamba la chai la Lupembe ambalo ni mali ya ushirika huo. 

Naibu Waziri Bashe kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Ole Sendeka, wamemteua Simon Chatanda, ambaye ni mfanyakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kuwa meneja wa shamba la chai la ushirika huo akisaidiana na mtu mwingine ambaye ni mtumishi wa Tanzania Small Holders Tea Development Agency (TSHTDA).

Gazeti la JAMHURI limemtafuta Bashe kwa njia zote za mawasiliano, hata hivyo hakupatikana ili kutoa ufafanuzi wa uamuzi wake huo. Kama ilivyokuwa kwa naibu waziri, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Ole Sendeka hakupatikana pia kutoa ufafanuzi. 

Hata hivyo, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, ameliambia JAMHURI kwamba yeye ndiye alimtuma Bashe kwenda Njombe kufuatilia mgogoro uliokigubika chama hicho kwa muda mrefu. 

“Juzi Naibu Waziri (Bashe) ameniambia kwamba ataniletea taarifa ya maandishi kuonyesha kile alichokiona kule,” anasema Hasunga. 

Alipoulizwa iwapo hatua zilizochukuliwa na Bashe kuivunja bodi ni sahihi au la, Hasunga amesema hawezi kulizungumzia hilo kwa undani hadi pale atakapoisoma taarifa ya kina atakayopewa na Bashe.

“Kuhusu hizo hatua zilizochukuliwa inabidi nione ripoti ndipo nitajua kama ni sahihi au la. Lakini hivi unaweza kuacha kuchukua hatua hata kama chama kinaibiwa? Lakini ngoja nione ripoti kwanza ndipo nitajua iwapo hatua zilizochukuliwa ni sahihi au la,” anasema. 

Katika barua kupitia kwa mwanasheria wao, wanachama hao wanaeleza kuwa hatua ya Bashe kuivunja bodi yao ni kinyume cha sheria na ni batili kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika Namba 6 ya mwaka 2013. 

“Iwe wewe binafsi au kama Naibu Waziri wa Kilimo, hauna mamlaka ya kisheria kuvunja bodi ya chama cha ushirika chochote nchini. Aidha, hauna madaraka ya kuamuru kuwekwa ndani kwa viongozi na wanachama wa chama cha ushirika,” inasomeka sehemu ya barua hiyo. 

Kwa mujibu wa jedwali la tatu katika Sheria ya Vyama vya Ushirika Namba 6 ya mwaka 2013, ni wanachama wa ushirika tu ndio wenye uwezo wa kuivunja bodi yao. 

Mgogoro huo upo mbele ya Mahakama ya Rufaa ya Tanzania katika Rufani Namba 64 ya 2016.  

Hisa za Serikali

Bodi ya chama hicho cha ushirika iliyoondolewa na Bashe inasimamia rufani iliyokatwa na chama hicho inayotokana na kesi ya kuhoji umiliki wa hisa ndani ya chama hicho.

Historia inaonyesha kuwa wakati fulani hisa za chama hicho ziliuzwa na PSRC na hapo ndipo Dhow Mercantile (EA) ilipoingia kwenye umiliki kwa ahadi ya kununua asilimia 70 ya zilizokuwa hisa za serikali. 

Hata hivyo, mchakato wa uuzaji wa hisa hizo haukufuatwa, badala yake kampuni hiyo ikachukua hisa zote za serikali.

Katika rufani hiyo, Lupembe Farmers Joint Enterprises Limited inapinga hukumu ya Mahakama Kuu kuipa Kampuni ya Dhow Mercantile (EA) haki ya kuendelea kumiliki hisa katika ushirika huo. 

Rufani hiyo ilitakiwa isikilizwe na Mahakama ya Rufaa Novemba 6, 2019 lakini ililazimika kuahirishwa baada ya Wakili wa Dhow Mercantile (EA) Limited, Michael Ngalo, kuandika barua kuwa anaumwa.