Na Mwandishi wetu, JAMHURI MEDIA
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amewakaribisha wawekezaji kutoka katika maeneo mbalimbali duniani kuja kuwekeza kwenye kilimo na kuahidi kuwa Serikali itatoa ardhi na kuweka mazigira bora.
Bashe ameyasema leo Machi 17, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na washiriki wa uzinduzi wa Jukwaa la Mfumo wa Chakula Afrika (AGRF), uliofaywa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Waziri Bashe amesema uzinduzi wa jukwaa hilo hapa nchini unaenda kufungua fursa kwenye sekta ya kilimo, hivyo ameomba wawekezaji kujitokeza ili tafsiri sahihi ya kufanyika kwa mkutano huo hapa nchini ikamilike.
Amesema Tanzania ina zaidi ya hekta milioni 29 zinazofaa kilimo cha umwagiliaji, hivyo mtu au taasisi inayotaka kuwekeza katika eneo hilo milango ipo wazi.
“Tunataka kilimo kiwe biashara, hivyo tunawaomba watu au taasisi ambazo zipo tayari kuja kuwekeza nchini, kwani kwa sasa tuna zaidi ya hekta milioni 29 zizonafaa kwa kilimo cha umwagiliaji,” amesema.
Bashe amesema lengo la Rais Samia na serikali yake ni kuona Tanzania inalisha dunia chakula safi na salama, hivyo lengo hilo linaweza kutumia kwa kuvutia wawekezaji.
Amesema mkutano wa Jukwaa la Mfumo wa Chakula Afrika unaotarajiwa kufanyika Septemba 5 hadi 9 mwaka huu nchini Tanzania utakuwa chachu kubwa ya kuhamasha kilimo.