Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mtwara

WAZIRI wa Kilimo Hussein Bashe amesema hata sita kuendelea kuwafutia leseni wafanyabiashara wakubwa na wadogo wanaotumika na waleta janja janja katika ununuzi wa korosho na kunyonya wakulima.

Amesema hatua ya Serikali kuwapa kipaumbele wafanyabiashara wa ndani kununua korosho moja kwa moja kwa wakulima haikulenga kufungua mianya ya unyonyaji.

Akizungumza katika muendelezo wa zira yake mkoani Mtwara Waziri Bashe amesema amefanya ziara hiyo mapema kabla ya msimu kuanza ili kusiwepo na kutoelewana.

Amesema anatambua wanaosemea wakulima si wakulima, hivyo hatasita kufuta leseni ya biashara kwa wafanyabiashara wakubwa, wadogo, wakati na wenye viwanda wanaofanya ujanja ujanja na kunyonya wakulima.

Ameongeza kuwa, muhimu ni kila mmoja kufuata bei elekezi kwa kuwezesha sekta ya kilimo cha korosho kupiga hatua.

“Kuna mtu ana hangaika kuanzia Oktoba kwa mwaka mzima, anaenda mnadani kipato chake ni kimoja kwa mwaka halafu kuna mtu yupo katikati, anafanya ujanja ujanja wa kumnyonya huyu mkulima sitakubali”, amesema Bashe.

Bashe ameongeza kuwa Serikali imebadili mfumo wa awali kwa kuwa mkulima anapewa chini ya bei, wanunuzi ambao ni wabanguaji wamegeuka kangomba na viongozi wa Amcos wamegeuka mawakala wakupokea pesa, sasa mnada ukiisha mnunuzi atalipa Chama cha Ushirika na ushirika walipe moja kwa moja kwa mkulima

Pia amesisistiza kuwa Serikali imezindua mfumo mpya wa masoko, TMX, kwa mazao ya kilimo ili kuhakikisha wakulima wanapata faida stahiki kutokana na kilimo.

Waziri Bashe ameeleza kuwa mfumo wa TMX unalenga kusaidia wakulima kufikia masoko kwa urahisi na uwazi, huku wakipata bei halali inayolingana na bei za kimataifa.

“Tumeanza kutumia mfumo wa TMX kwa lengo la kusaidia wakulima kufikia masoko kwa urahisi, uwazi na kupata bei halali, inayolingana na bei ya mazao katika masoko mengine yote duniani,” alisema Waziri Bashe.

Pamoja na changamoto zilizopo, Waziri Bashe alisisitiza kuwa serikali itaendelea kuboresha na kutumia mfumo huu, huku ikiunga mkono wadau wote wanaounga mkono mfumo huo. Amepongeza benki zote nchini kwa kusaidia ukuaji wa sekta ya kilimo kupitia mikopo mbalimbali kwa wakulima.

Waziri Bashe pia alibainisha kuwa Serikali imepanga kuajiri maafisa ugani 400 ili kuhakikisha kila kijiji cha uzalishaji kinakuwa na afisa ugani. Hii itasaidia serikali kufanya mipango,kupata takwimu sahihi;na makadirio sahihi kuhusu mahitaji ya wakulima katika ngazi ya uzalishaji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, alisema kuwa Mkoa wa Mtwara unafanya vizuri katika uzalishaji wa mbaazi, korosho, na ufuta. Aliongeza kuwa uzalishaji wa korosho umeongezeka kwa asilimia 82 ikilinganishwa na mwaka uliopita, na kwamba Mkoa umefanikiwa kuzalisha tani 180,544 za korosho kwa msimu wa 2023/2024.

Mapinduzi yanayofanywa na Wizara ya Kilimo yamewezesha usambazaji wa pembejeo za kilimo kwa njia ya kielektroniki, ambapo wakulima wanahitajika kusajiliwa katika mfumo. Mfumo huu unalenga kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali zinazohusiana na kilimo, ikiwemo ruzuku ya mbolea, ambayo imechangia kuongezeka kwa uzalishaji katika Mkoa wa Mtwara.

Kanali Sawala amesema kuwa Mkoa wa Mtwara imepata tuzo ya usimamizi bora wa tasnia ya korosho, na kuishukuru serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa usambazaji wa zaidi ya lita 21,000 za salfa na viuatilifu kwa Mkoa wa Mtwara.

Kanali Sawala ameongeza kuwa wakulima wa Mtwara wameanza kutambua kuwa inawezekana kulima mazao mengine mbali na korosho.

Waziri Bashe anaendelea na ziara yake mkoani Mtwara, ambapo anatarajia kukagua na kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali kupitia Wizara ya Kilimo, pamoja na kuzungumza na wananchi kwa lengo la kueleza utekelezaji, fursa, mipango, malengo na kusikiliza changamoto na kero za wakulima na wadau wa kilimo katika Mkoa wa Mtwara.

Please follow and like us:
Pin Share