Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ametoa rai kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kushirikiana katika uzalishaji wa chakula kwa mpango utakaonufaisha nchi zote wanachama.

Bashe ameyasema hayo leo alipowasilisha mada kuhusu kilimo cha kisasa kama njia ya kukabiliana na upungufu wa chakula katika mkutano wa 53 wa Mabunge ya SADC (SADC PF 53) unaofanyika Arusha.

Amesisitiza kila nchi inapaswa kuzalisha mazao ambayo itawauzia wengine na kuacha kutegemea uwezo wa nchi kuzalisha zao husika.

Ametoa mfano wa uwezo wa Tanzania katika kuzalisha mahindi na mchele ukilinganisha na nchi nyingine za SADC na kusema ni vema nchi nyingine zinunue chakula hicho na Tanzania inunue mazao mengine kutoka nchi za wanachama.

Waziri Bashe ameongeza kuwa kwa sasa tishio kubwa linalozikabili nchi nyingi za SADC ukiondoa Afrika Kusini ni upatikanaji wa mbegu, jambo ambalo linaweza kukwamisha jitihada za kuwa na uhakika wa chakula.

Kuhusu njia za kisasa za kuendesha kilimo, Waziri Bashe amesema Tanzania imepanga kuwa na hekta za mraba milioni 8 za kilimo cha umwagiliaji ifikapo mwaka 2030 ili kujiwekea uhakika wa kuzalisha chakula kipindi chote cha mwaka.