Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Ruvuma
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ametangaza bei elekezi ya kununua mahindi Mkoani Ruvuma, kuwa kilo moja ya mahindi itauzwa kwa bei isiyo pungua shilingi 550 kwa kilo moja.
Waziri Bashe amesema hayo alipokuwa anazungumza na maafisa kilimo, wafanya biashara ya mazao,mbegu na mbolea, maafisa ugani na wadau wengine wa kilimo; wilayani Songea.
Katika mkutano huo, Waziri Bashe alisisitiza umuhimu wa kufuata bei elekezi na kwamba wataalamu wa wizara watapita vijijini na wilayani kusajili mawakala ili kuhakikisha biashara ya mahindi inafanyika kwa ufanisi.
Waziri Bashe alisisitiza kuwa serikali inapotoa bei elekezi, inazingatia uhalisia wa soko, gharama za uzalishaji na gharama nyinginezo.
Aliongeza kuwa wafanyabiashara kutoka nje ya nchi wanaotaka kununua mazao lazima wapitie kwa wafanyabiashara wa ndani.
“Tenengenezeni umoja wenu wenye nguvu na serikali ipo tayari kufanya kazi na nyie,”alisema Bashe.
Alifafanua kuwa wafanyabiashara wanaonunua mahindi kwa niaba ya WFP walikuwa wakinunua kwa bei ya Shilingi 400 kwa kilo wakati serikali ilikuwa ikinunua kwa Shilingi 1000, lengo likiwa kuwasaidia wakulima kwa kupandisha bei ya ununuzi wa mahindi.
“Serikali imetoa muongozo kuwa itaendelea kununua mahindi mpaka yaishe na vituo havitafungwa.
“Pia Mahindi ambayo ni mabovu yaliyokuwa yakitupwa yatatumika kama chakula cha mifugo.,”alisema.
Aidha serikali itatoa kibali kwa wafanyabiashara watakaokuwa tayari kujenga maghala ya kuhifadhia chakula.
Waziri Bashe alieleza kuwa mkakati wa kuboresha mifumo ya utoaji wa mbolea na mbegu unaendelea na mifumo hiyo itasimamiwa kikamilifu ili kuvutia wauzaji na wanunuzi.
Alisemaa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewekeza zaidi katika kilimo ikilinganishwa na awamu zilizopita, ikiwemo kuajiri wataalamu, ununuzi wa vifaa, na ujenzi wa miundombinu. Alisema serikali itaendelea kukabiliana na changamoto kadiri zitakavyojitokeza.
Kwa upande wa viwatilifu, Waziri Bashe alieleza kuwa kila aina ya kiuatilifu kitakachouzwa kwa mkulima kiwekewe alama ili serikali iweze kufuatilia changamoto zitakazojitokeza.
Aliongeza kuwa mamlaka husika zifanye uchunguzi na ufuatiliaji wa viuatilifu vinavyoingia kutoka nchi jirani ili kuthibiti ubora wake.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Songea, William Ndile, ameomba wizara kutekeleza mpango wa kituo cha ambacho kitawakutanisha wataalam wa kilimo katika eneo moja, ili kuepusha adha kwa wakulima na kurahisisha utekelezaji wa mipango, malengo, sheria, kanuni na taratibu za wizara hiyo.