Na NIRC Dodoma
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amehimiza ushirikiano kati ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri, katika kusimamia miradi ya Umwagiliaji nchini.
Amesema Tume inatekeleza mradi wa Mifumo Himilivu ya Chakula nchini(TFSRP) lengo ni kuongeza uzalishaji wa chakula kutosheleza ndani ya nchi na kuilisha dunia,hivyo kuwapo na ushirikiano na Halmashauri.
Aidha amesisitiza kuwa katika utekelezaji wa mradi huo Tume imenunua zaidi ya Magari 17 na mitambo kwaajili ya uchimbaji wa Visima 56,000 vya Umwagiliaji na kuboresha miundombinu ya Umwagiliaji kwa lengo la kufikia adhina ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuongeza uzalishaji wa chakula.
“Magari hayo yanatarajiwa kuwasili kuanzia Machi mwaka huu, ambapo mawili kati ya hayo yatakuwa na uwezo kuchimba visima virefu zaidi”, amesema Bashe
Waziri Bashe amesema Tayari serikali imeshatangaza kandarasi ya kuchimba visima hivyo na tumepata wakandarasi kwa ajili ya kuanza kufanya kazi.
“Na tumesema kila kisima kimoja kiwe na uwezo wa kuhudumia ekari 40 za kilimo,”alisema
Amesema hayo katika hafla ya Makubaliano na Wakurugenzi wa Halmashauri 19 nchini, juu ya Usimamizi, Uendeshaji na Matunzo ya Skimu za Umwagiliaji kati ya Tume na Vyama vya Umaagiliaji kupitia Mradi huo.
Alihimiza Wakurugenzi hao kuhakikisha kuwa wanatembelea wakulima mashambani na kufanya Maafisa Kilimo wafanye kazi yao ya kuhudumia wakulima.
“Ili kuinua kilimo, lazima awepo Afisa Kilimo anayemhudumia Mkulima kuongeza uzalishaji,” alisema Bashe.
Aliongeza kuwa:”Kupitia mradi huu tunaendelea kufanya usanifu katika mikoa mbalimbali na tunampango wa kununua pampu 2,000 ambazo zitasambazwa maeneo ambayo yanavyanzo vya maji ambayo haviitaji kujengwa ili kuhakikisha maji hayo yanawafikia wakulima.
Waziri Bashe alisema ili kufanikisha hali hiyo na adhima ya Rais Dkt Samia ya kuongeza uzalishaji Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ihakikishe inawashirikisha wakurugenzi kwani ndio wanaishi na miradi pamoja na wakulima
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Tume ya Umwagiliaji Raymond Mndolwa alisema serikali ilipata fedha za mkopo nafuu dola milioni 300 kwa ajili ya kutekeleza mradi katika kipindi cha miaka mitano.
Alisema mradi huo utaenda kurekebisha maneo ya kilimo ili kuhakikisha skimu za wakulima zinawekewa mifumo sahihi kwa ajili ya uzalishaji.
“Katika kutekeleza mradi huu tuliona ni muhimu kushirikiana na wakurugenzi wa halmashauri kwasababu wao ndio wapo kwa wananchi,”alisema
Aliongeza kuwa ;”Mradi huu utaenda kuchimba visima nchi nzima kupitia magari ambayo yameagizwa na yataanza kuwasili hivi karibuni lengo ni kuhakikisha sera ya serikali ya kuongeza tija katika Kilimo cha Umwagiliaji ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi inafikiwa,”alisema
Akifunga Hafla hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Mweli alisema kuwa halmashauri nyingi nchini zinategemea kilimo kwa zaidi ya 80% ya mapato yake hivyo ushirikiano wa kisekta katika kusimamia miradi ya Umwagiliaji ni muhimu.
“ Wizara imeandaa mwongozo wa namna ya kuongeza mapato kupitia kilimo na halmashauri kutenga ekari 1,000, kwa akili ya miundombinu ya Umwagiliaji, lengo ni kuzalisha ajira,kuongeza uzalishaji na kupunguza tatizo la njaa na kufikia maono ya serikali kuilisha dunia,”alisema.
Naye Mratibu wa Mradi huo Mhandisi Naomi Mcharo alisema mradi huo utatekelezwa nchi nzima ambapo kupitia sekta ya umwagiliaji mradi huo utagharamiwa kwa dola za kimarekani milioni 70 na Tume imeanza na Wakurugenzi wa halmashauri 19 kutoka katika mikoa sita ambayo inalima zaidi kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji ili kuwajengea uwezo.