Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Tandahimba
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amevitaja vyama vya ushirika nchini kubadilika ili wakulima wazidi kunufaika na ushirika huo.
Bashe ametoa kauli hiyo leo Oktoba 2, mara baada ya kuzindua kiwanda cha kubangua korosho kinachosimamiwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (TANECU LIMITED) kilichogharimu Sh bilioni 3.4.
Kiwanda hicho kimejengwa katika kijiji cha Mmovo kata ya Kitangari kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Newala mkoani Mtwara.
“Nataka niwaambie wakulima kama vyama vyetu vya ushirika havitakubali kubadilika ni heri kutokuwa na ushirika unaonyonya wakulima kuliko kulea ushirika unaonyonya wakulima ni lazima vyama vya ushirika vibadilike,” amesema Bashe.
Hata hivyo amewahakikishia na kuwatoa wasiwasi wakulima wa zao hilo kuhusu swala la bei kuwa na kwamba bei itakuwa mzuri katika msimu wa kilimo mwaka 2024/2025.
“Naomba niwahakikishie wakulima tuna korosho mzuri, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tutapata bei mzuri,”amesema Bashe.
Meneja wa Tanecu Mohamed Nassoro amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kubangua tani 3,500 kwa mwaka baada ya kukamilika kwa kiwanda hicho wataanza ujenzi mwingine wa viwanda vingine 19 vilivyobaki katika wilaya za Tandahimba na Newala hivyo kufanya jumla ya viwanda 20 kwenye wilaya hizo vyenye uwezo wa kubangua tani 70,000 kwa mwaka.
Mrajisi na Mtendaji Mkuu kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) Dk Benson Ndiege amesema ujenzi wa kiwanda hicho ni utekelezaji wa adhima ya serikali kwani inapotoa maelekezo inatakiwa vyombo vya chini vifanyie kazi na waliyafanya hayo kwasababu takribani miaka miwili hadi mitatu iliyopita bei za korosho ghafi ilikuwa zimepungua.
‘’Tukaona kwamba tuna wajibu wa kujenga viwanda ili tuongeze thamani mazao ya wakulima wa Tandahimba na Newala ili mwisho wa siku kuleta tija na kunufaisha ili kuboresha maisha ya wakulima hawa’’
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Maalum ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Newala Mjini, George Mkuchika amesema wilaya ya Newala wanapenda ushirika kwasababu awali wilaya hiyo ilikuwa na vyama vya ushirika 21 ikilinganishwa na sasa.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala amesema mkoa huo umekuwa ukinufaika na sekta hiyo ya kilimo ambapo sasa wanajiona uwekezaji huo mkubwa wa kiwanda hicho lakini pia serikali inavyoendelea kuwapatia wakulima pembejeo za korosho bure.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas alisema uzinduzi wa kiwanda hicho amekuja kujifunza na kujionea hatua hiyo mzuri kilipofika kiwanda baada ya ile hatua aliyoachia yeye wakati akiwa mkuu wa mkoa wa Mtwara.