Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), limesema halijaufungia wimbo wa Parapanda ulioimbwa na wasanii wa kundi la Rostam, Roma Mkatoliki na Stamina na kusema kuwa labda wameamua kujifungia wenyewe kwa lengo la kutafuta ‘kiki’.
Kauli hiyo inakuja ikiwa ni siku moja baada ya Roma kupitia ukurasa wake wa Instagram kuandika maneno ya kuilaumu Basata kwamba inaua vipaji na ubunifu wa wasanii na kuhoji wimbo wao huo una tatizo gani.
Mbali na kuandika hayo pia alizungumza na baadhi ya vyombo vya habari na kudai kuwa amepewa wito wa kufika Basata.
Akilizungumzia hilo, Katibu wa Baraza la Sanaa, Godfrey Mngereza, amesema hawajaufungia wimbo huo na haujapitishwa mikononi mwao hadi sasa kwa ajili ya kuhaririwa.
“Labda kama wameamua kujifungia wenyewe ili kuufanya wimbo wao ujulikane na watu, lakini sisi hata hatujauona na kuupitia kama taratibu zetu zinavyotaka na mnajua tukifungia wimbo huwa tunatangaza sasa labda Roma awaonyeshe wapi tumesema hivyo,” amesema Mngereza.
Wasanii hao, Agosti 2 waliachia wimbo huo Parapanda, unaoelezea masuala mbalimbali yanayoendelea nchini yakiwemo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Wimbo huo ambao umeachiwa sauti tu (audio) katika mtandao wa YouTube, umesindikizwa na picha za hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na aliyekuwa mwanasiasa mkongwe marehemu Kingunge Ngombare Mwiru.
Hata hivyo, katibu huyo alikiri kuwa juzi wasanii hao wawili kufika katika ofisi za Basata kwa ajili ya kushiriki jukwaa la wasanii ambalo hufanyika kila siku ya Jumatatu katika ukumbi wao uliopo Ilala Gereji huku mada kuu kwa siku hiyo ilikuwa kuhusu kanuni mpya za sanaa zilizoanza kutumika Julai mwaka huu.
Pia Basata limesema iliwaita Roma na Stamina kwa kuwa walikiuka taratibu za kufikisha wimbo kwenye baraza ili ukaguliwe kabla kuutoa rasmi
Katika jukwaa hilo anasema mmoja wa waandishi aliuliza swali kuhusu matumizi ya picha za waasisi wa mbalimbali wa nchi hii katika sanaa, ambapo Mngereza anadai alimjibu kuwa msanii anapaswa kupata kibali kutoka kwa familia au Serikali.
“Huenda majibu haya labda ndiyo yalimfanya Roma akaondoka pale na tafsiri yake na kuandika hicho alichokiandika, lakini kiukweli hatujamfungia wala kumuita kumuhoji kuhusiana na wimbo hiyo,” amesema Katibu huyo.