Pongezi za dhati kwa Mzee  Halimoja

Ndugu Mhariri,

Sina budi kutoa pongezi za dhati kwa Mzee Yusufu Halimoja kwa kazi nzuri sana ya kuendelea kutetea bila kuchoka uboreshaji wa elimu nchini.

Kumbu kumbu zilizopo zinaonesha kuwa Mzee Halimoja ameanza kazi hiyo tangu miaka ya 1970, wakati huo akiwa mwalimu na pia akiandika vitabu bora kwa ajili ya masomo mbalimbali katika shule za msingi.


Hata hivyo nilifarijika mwezi uliopita baada ya kusoma makala yake, akiuponda mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika elimu ulioanzishwa na Serikali katika mwaka huu wa fedha wa 2013/2014.


Sina hoja ya kurudia alichoandika niseme tu kwamba alielezea kwa ufasaha, kina na uwazi, upungufu mkubwa sana uliopo katika mpango huo na mfumo wa elimu yetu kwa ujumla.


Lakini ili asionekane ni mtu mlalamikaji tu akatoa somo kwa Serikali nini cha kufanya.


Kwa hakika ni dhahiri sana Serikali yetu sio tu inatudharau sisi wananchi, bali pia inaonekena baada ya kufanya ufisadi katika kila sekta kwa muda mrefu imejaa kiburi cha madaraka.


Wananchi tunaelewa pasi na shaka kuwa watoto wetu wanahudhuria shuleni lakini wanamaliza hawana walichojifunza chochote darasani. Je iweje Serikali katika mazingira kama hayo itegemee muujiza wa mafanikio?

Tusubiri tuone.

Jeanster  Elizabert,

P.o.Box Private Bag,

Mwanza

PSPF fafanueni kuhusu  Fao la Ulemavu

Ndugu Mhariri,

Katika Gazeti la JAMHURI toleo Na. 103 zilikuwemo habari kuhusu Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF). Ndani ya habari hiyo iliyochapishwa chini ya safu ya makala ya mtangazaji, mwandishi maalum akielezea kila kitu muhimu kuhusu taasisi hiyo ya hifadhi ya jamii.


Eneo lililonigusa sana na kuwajibika kuandika barua hii nikiomba ufafanuzi kutoka kwa wahusika, ni la huduma zinazotolewa na PSPF hususan kuangalia upya ubora wa mafao.


Kama sote tunavyofahamu katika mwaka wa fedha wa 2008/2009 Serikali kupitia kwa Waziri wa Fedha wa wakati huo, Mustafa Mkullo, ilitangaza kuongeza kima cha chini cha pensheni na kufikia Sh 50,000 kwa mwezi.


Hadi niandikapo barua hii PSPF haijawahi kuongeza kima cha chini cha pensheni. Ushahidi wangu wa karibuni kabisa nimeshuhudia mtumishi wa umma aliyestaafu kwa mujibu wa sheria, mwanzoni kwa mwaka huu ameelezwa na mfuko huo kimaandishi kwamba atapokea Sh 41,500.00 kama pensheni  kwa mwezi.


Kwa hiyo kwa kiwango hicho cha fedha PSPF imeendelea kutoheshimu agizo la serikali lilitolewa miaka mitano iliyopita. Lakini pia inapingana  na maelezo yake yenyewe kwamba unaangalia upya ubora wa mafao.


Naelewa kuwa PSPF imekuwa ikiwalipa wastaafu kiwango kikubwa cha fedha, zaidi ya milioni moja katika kila kinachoitwa Mini Arrears mara moja kwa mwaka.


Hata hivyo hakuna maelezo bayana kutoka katika mfuko huo kuhusu fedha hizo zinapatika wapi. Vile vile haujulikani ni vigezo gani na fomula gani vinavyotumika kupata kiasi cha fedha anacholipwa mstaafu husika.


Je, kwa nini PSPF inamrundikia mstaafu mamilioni ya fedha za Mini Arrears kwa mkupuo mmoja badala ya kuzigawanya kwa miezi 12 sawa sawa ili kumsaidia kimaisha vizuri zaidi na kwa uhakika?


Naomba nimalizie maoni yangu kwa kugusia mafao ya ulemavu. PSPF ieleze ni mstaafu gani anayestahili kulipwa mafao ya uelemavu? Je, ni mtumishi wa umma aliyeumia na kupata ulemavu wa kudumu akiwa bado kazini, au ni yule mstaafu ambaye kutokana na uzee amejikuta ameugua maradhi ya kupooza mwili na kupata ulemavu?


Je, mstaafu anayestahili kulipwa mafao ya ulemavu afuate taratibu zipi ili aweze kupata haki yake hiyo?

Jeanister Elizabert,

P.o.Box Private Bag,

Mwanza