JAMHURI endeleeni kupinga maovu Tanzania

Ni muda mrefu toka nimeanza kufuatilia maandishi na machapisho ya gazeti hili.Nilipata kujiuliza maswali mengi na kuhangaika kwa muda wa miezi sita kutafakari na kujiuliza nini maana ya Jamhuri na ni kwanini wahusika na bodi nzima iliamua kuliita gazeti hili kwa jina la JAMHURI.

Wakati mwingine ilinichukua muda mwingi kupata ulinganifu wa majina ya magazeti mengine yanayochapishwa hapa nchini yenye majina lukuki ila bado swali langu liliendelea kupata changamoto za uvutio, hisia, dhamira na wakati mwingine niliwaza na kushirikisha mawazo yangu kwenye Taifa hili lililopata kuitwa JAMHURI mnamo mwaka 1964.

 

Mambo yanayoandikwa kila mara kwenye gazeti hili yanazidi kunikumbusha mbali zaidi, hasa yanayohusu maendeleo ya Taifa hili yakiwamo ya kiuchumi na siasa kama mgongo unaotumika kudidimiza maendeleo ya JAMHURI kijamii na utamaduni kwa ujumla.

 

Baada ya harakati hizo, ndipo tafakari zangu zilianza kunipa majibu ya kwanini gazeti Jamhuri. Maana yake ni Tanzania iliyoandaliwa vyema na waasisi wetu, waliojenga misingi ya umoja, amani, mshikamano na uhuru wa kujitawala kifikra au mawazo, Jamhuri yenye kujitegemea kwa kutumia nguvu za Watanzania wanaotokana na JAMHURI.

 

Ni dhahiri sasa gazeti hili limekuja kwa wakati mwafaka kuikumbusha jamii ya Watanzania na pia kutenda kazi ya kuonesha mambo ya msingi yenye kulitoa Taifa hili hapa tulipo na kusogea kwenye hatua nyingine kama Mwalimu alivyosema, “Tukitaka kuendelela lazima kupiga tathmini ya tulikotoka, tulipo na wapi tunakotaka kwenda.”

 

Ni ishara tosha kwa Serikali hii kwamba mambo ya msingi ya kuliendeleza Taifa yamesahaulika kutokana na baadhi ya watu wachache wenye nafasi na mamlaka, yaani viongozi au watu waliojengeka na hisia mbaya kutokana na ushawishi au fedha kuhujumu maslahi ya umma wa Watanzania.

 

Watanzania wenye tumaini la maendeleo tokea ukombozi wa nchi yetu na harakati zilizojaa vipaumbele vya misingi vya kujitawala na kutambulika kama Taifa huru kama ilivyokuwa kwa mataifa mengine duniani yaliyokuwa na kauli isemayo: “MAENDELEO HULETWA NA TAIFA LILILOKUWA HURU.”

 

Ni kutokana na msukumo wa viongozi wetu waasisi kutambua umuhimu wa kujitawala na kuitwa Jamhuri, utawala wao ulizingatia maadili ya uongozi, nidhamu ya kazi, haki na wajibu wa kila aliyepewa fursa ya kuongoza wengine kwa lengo kubwa la kuharakisha maendeleo ya wananchi, hasa katika huduma muhimu zinazogusa maisha yao ya kila siku kama vile afya, elimu na maji. Maendeleo yoyote hubainishwa na afya bora, elimu bora na huduma nzuri ya maji.

 

Kwa kuzingatia hayo nchi yetu sasa sio jamhuri tena ya Watanzania bali ni Jamhuri ya WATUNZANIA. Maana yake ni kwamba wapo viongozi waliosahau kuwa nchi hii ni ya Watanzania na kuifanya kuwa mikononi mwao na wanaweza kufanya au kuamua lolote bila ya kuogopa na kutambua uwepo wa wamiliki, yaani WATANZANIA.

Hili limechukua sehemu kubwa katika siasa ya utawala ndani ya nchi yetu na kuligharimu Taifa kuwa na umaskini ambao kwa sasa umegeuka ukoma, yaani ugonjwa usiokuwa na tiba!

 

Ni ushuhuda uliodhahiri kwa safu ya uongozi wa Serikali yetu kwa sasa ambao umeandamana na tamaa za mali, tena mali ya wengi, ila wamesahaulika na hawana nafasi ya kuhoji popote. Wakati mwingine tumeshuhudia wachache waliojitosa kutetea umma wakipewa adhabu kama watuhumiwa na wengine kubambikwa kesi zisizokuwa na hukumu na mpaka sasa nyingine zipo mahakamani.

 

Jambo la msingi la kujiuliza kwa viongozi wetu ni kwamba kila kitu kina awali na hatima yake. Rai kwa viongozi wa nchi hii, miaka hamsini ya uvumilivu ni sawa na kuonja matunda ya mti uliooteshwa, ukazaa matunda, yakaiva na hatimaye hakuna aliyeyafaidi kama ilivyotegemewa na wengi.

 

Nguvu iliyotumiwa na Watanzania kutafuta uhuru wao kwa malengo ya kufurahia matunda yametoweka na wengi wamekata tamaa kabisa. Matarajio yalikuwa ni kuona rasilimali za nchi hii zikitumiwa kwa uangalifu na udhibiti ili kuwanufaisha kama tegemeo kuu na azimio lao lililopewa misingi na mwasisi wetu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

 

Badala yake rasilimali zimegeuka kuwa mtaji wa viongozi wachache wasiokuwa na huruma, uoga na wamezidi kudidimiza maisha ya Watanzania kuwa magumu kupindukia, elimu isiyokidhi haja ya Watanzania, huduma mbovu za afya, ukosefu wa maji na hali ya usafiri usiojali muda kutokana na kuchelewesha ubunifu wa miundombinu ya barabara. Tunajiuliza kama wazalendo kwamba mambo haya mpaka lini?

 

Haya yamejenga Tanzania mpya iliyojaa chuki, hasira, lawama, mikakati tofauti tofauti yenye kuengua wingu lililotanda kwenye sura ya Tanzania ya miaka hamsini ijayo. Wengi husikika wakisema rushwa, uongozi mbovu, sera uchwara, ubinafsi, fursa za kidugu kwa maslahi na tamaa ndivyo vilivyotufikisha hapa. Swali linakuja kwamba hili ndilo wingu?

 

Gazeti Jamhuri kama mdau wenu sina mengi ya kuongelea na kufanya uchambuzi zaidi ila endeleeni kupiga vita maisha yaliyojaa dhuluma, ufisadi, mateso na utetezi wa haki kwa wenye kustahili kwani Mungu ameazimia kuipata Tanzania mpya yenye neema, furaha, uzalendo na tunu ya amani iliyokomaa kwa muda wa miaka hamsini iliyopita japo haifurahishi kutokana na shida na taabu walizonazo Watanzania wa leo.

 

Nikinukuu maoni ya Mhariri wa gazeti Jamhuri la Septemba 10-16, 2013 amesema, “SOTE TUKIWA WAOGA NCHI ITAYUMBA.” Ni kweli kwamba tumefika hapa kwa sasbabu ya uoga na ni wazi hakuna maendeleo iwapo watu wataogopa kutafuta haki zao. Hata Nyerere alisema uoga ni umaskini wa milele hivyo, ogopa woga!

 

wa Tanzania kwa mara nyingine upo njiani kama ilivyotabiriwa na watu wengi wenye hekima na mawazo ya mabadiliko kulingana na mifumo iliyopo, iliyodumu kwa muda wa nusu karne bila mafanikio. Wahenga walisema, “Kila neno lililonenwa litatimia.”

MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU IBARIKI JAMHURI, Tanzania itajengwa na Watanzania.

 

Wako,

 

Narcis Silvester

Simu: 0712 143 126

P. O. Box 4700, DSM