Bukoba kulikoni?
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meya, Balozi Kagasheki tuambieni kulikoni Bukoba? Tuambieni wakweli ni wapi kati ya madiwani waliofukuzwa, meya na madiwani waliobaki. Tuambieni tatizo ni nini hasa? Kimefichika nini hasa?
Mangula, Nape na Rais Kikwete wamefika Bukoba lakini hatuambiwi kiini cha tatizo ila tunaambiwa tu kwamba ni mgogoro usiokuwa na tija.
Ni tija gani hiyo ambayo imewashinda Mangula, Nape, Balozi Kagasheki na Rais Kikwete hadi madiwani wanane kufukuzwa udiwani? Kuna maslahi gani na ya nani hasa?
Mkuu wa Mkoa na Meya wa Bukoba angalieni sana mtakigharimu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa sababu ya maslahi binafsi.
Mwogopeni Mungu jamani, mnafanya rais wetu aonekane hafai. Je, amewatuma kuyafanya hayo? Acheni kumdhalilisha Rais Kikwete na Serikali yetu. Kama mmeshindwa majukumu tokeni msisumbue wananchi wa Bukoba.
Maheri Maheri, Bukoba
0785 880 350
Wavuta sigara kuweni wastaarabu
Miongoni mwa vitendo vinavyowakera wengi ni uvutaji wa sigara usiyo wa kistaarabu. Wavuta sigara wengi wanakera mno pale wanapovuta sigara katikati ya msongamano wa watu na kutema moshi ovyo.
Utakuta mtu anavuta sigara stendi, baani, hotelini na hata barabarani kwenye msongamano wa watu na kutoa moshi mwingi ambao husambaa kwa watu wengi wakiwamo wasiyovu sigara.
Kibaya zaidi wataalamu wa afya wanasema kwamba moshi unaotolewa na mvuta sigara huwaathiri zaidi watu wengine kuliko mvutaji mwenyewe. Kwa hali hiyo mbona wavuta sigara wasiyo wastaarabu watatuangamiza watu wengi kwa moshi wa sigara wanaoutema ovyo katika msongamano wa watu.
Ninajua sheria ya kuzuia watu kuvuta sigara katika msongamano wa watu ipo ila inaonekana haizingatiwi na wavuta sigara wengi, na hata vyombo vya dola havichukui hatua za kisheria dhidi ya watu wanaoikiuka sheria hiyo.
Hatuwezi kuzuia watu kuvuta sigara kuridhisha nafsi zao ila ninashauri wavuta sigara wote wajenge utamaduni wa kuvuta sigara kistaarabu bila kusababisha bughudha kwa wengine wasiyo wavutaji. Wajenge tabia ya kujitenga na watu wengine wakati wa kuvuta sigara.
Lakini pia, serikali isimamie kwa vitendo sheria iliyopo kwa kuhakikisha inawachukulia hatua za kisheria watu wanaovuta sigara hadharani kwenye misongamano ya watu. Inakera sana.
Mpenzi wa JAMHURI, Dar es Salaam