Mheshimiwa John Pombe Magufuli,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ikulu, Dar Es Salaam
Agosti 30, 2018
UTANGULIZI
Mheshimiwa Rais,
Nakusalimu kutoka Leuven, Ubelgiji ninakoendelea na matibabu. Naomba pia upokee salamu zangu za rambi rambi na pole kwako wewe binafsi, mama yako mzazi, ndugu, jamaa, marafiki na majirani zenu wa Chato, kwa kufiwa na mpendwa dada yako hivi karibuni.
Mheshimiwa Rais,
Nimewiwa kukuandikia barua hii ya wazi baada ya kusikiliza kipande cha hotuba yako ya leo tarehe 30 Agosti, 2018, wakati ukizungumza na viongozi wa ngazi mbalimbali wa Wilaya yako ya Chato, Mkoa wa Geita. Aidha, nimepitia taarifa rasmi kuhusu hotuba yako iliyotolewa na Mkurugenzi wako wa Mawasiliano, Gerson Msigwa.
Ni barua ya wazi kwa sababu masuala uliyoyazungumzia kwenye hotuba yako, na nitakayoyajadili hapa, ni masuala yenye umuhimu mkubwa kwa umma wa Watanzania, hasa katika kipindi hiki katika historia ya nchi yetu. Kwa umuhimu wake, na kwa njia uliyoitumia kuyazungumza, haya ni masuala ya umma yasiyohitaji kufungwa kwa viapo vya siri vya Ikulu.
Mheshimiwa Rais,
Umezungumza vizuri sana, na kwa upole ambao wengi wetu hatujauzoea kutoka kwako. Kwa mujibu wa taarifa ya maandishi ya Mkurugenzi wako wa Mawasiliano, umewataka viongozi wote nchini kutekeleza majukumu yao “kwa kuzingatia sheria sambamba na kuhakikisha wanasimamia ipasavyo matumizi ya rasilimali za umma kwa maslahi ya wananchi.”
Kwa kifupi, Mheshimiwa Rais, umezungumzia umuhimu wa viongozi wote kuheshimu Katiba na Sheria za nchi yetu katika utekelezaji wa mamlaka yao ya umma. Hiki ndicho kinachoitwa, kwa lugha ya kitaalamu, Utawala wa Sheria. Yaani kila mtu, bila kujali cheo, nasaba au nafasi yake ya kiuchumi au kijamii, anapaswa kuheshimu Katiba na Sheria za nchi.
Mheshimiwa Rais,
Ijapokuwa imekuchukua karibu miaka mitatu kutambua umuhimu wa Utawala wa Sheria kwa nchi yetu, hasa kwa “viongozi wote”, kwenye suala hili mimi ninakuunga mkono.
Sina shaka, Mheshimiwa Rais, kwamba kwa matendo ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambayo leo umelazimika kuyakiri hadharani, umeanza kutambua hatari ya viongozi wetu wa umma kuendesha shughuli za umma kwa amri, matamko na utashi wao binafsi, badala ya kuongozwa na utashi wa Katiba na Sheria za nchi yetu.
Kwa uzoefu wetu wenyewe wa miaka mingi kama Taifa, viongozi wa aina hii huwa hawachelei kugeuza ofisi na dhamana zao za umma kuwa ‘pango la walanguzi’, kwa kauli maarufu ya Baba wa Taifa.
Aidha, kwa uzoefu wetu huo, viongozi wa aina hii hutumia mamlaka yao hayo kuonea wananchi, kuwadhulumu haki zao na kuwanyanyasa ama kudhalilisha utu wao. Haya yote, Mheshimiwa Rais, tumeyashuhudia sana katika awamu hii ya utawala wa nchi yetu.
YA MKUU WA MKOA PAUL MAKONDA
Mheshimiwa Rais,
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ni kielelezo sahihi na cha wazi cha viongozi wasiozingatia, na ya wanaopuuza Utawala wa Sheria. Naomba na hili la makontena yaliyoko bandarini ambalo umelizungumzia wewe mwenyewe.
Umesema kwamba kama Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam anadaiwa kodi kutokana na yaliyomo kwenye makontena yale basi ailipe kodi hiyo.
Lakini papo hapo, Mheshimiwa Rais, umeibua maswali kadhaa. Je, kilichopo ndani ya makontena yale ni madawati ya shule tu au kuna masofa ya kupelekwa kwenye shopping malls!
Je, ni marafiki au watu gani waliomtumia Mkuu wa Mkoa makontena yale!
Je, kama ni zawadi kwa Mkuu wa Mkoa, kiongozi wa Serikali, kwanini zawadi hizo kwa Serikali hazijapelekwa Waziri wa Fedha ambaye, umetuelimisha, ndiye mwenye mamlaka kisheria ya kupokea zawadi zote za Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Misaada, Mikopo na Dhamana za Serikali ya mwaka 1974.
Mheshimiwa Rais,
Maswali uliyoyaibua yanaonyesha dhahiri kwamba hata wewe mwenyewe huamini hii hadithi ya makontena ya vifaa vya elimu kwa ajili ya shule za Dar es Salaam.
Na kwa sababu wewe ni Mkuu wa Nchi na Kiongozi Mkuu wa Serikali pia, sisi wananchi wako wa kawaida hatuwezi kutilia shaka msingi wa mashaka yako juu ya makontena haya na mwenendo wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuhusiana nayo.
Ninachotaka kuelezea ni kile ambacho wewe hujakisema kuhusiana na maswali uliyoyaibua juu ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Moja, kama ni kweli kwamba makontena ya Makonda yana mizigo mingine ambayo hajaitangaza bandarini, basi Mkuu huyo wa Mkoa atakuwa ametenda kosa la jinai la kutoa taarifa ya uongo (false declaration) kwa mujibu wa Sheria mbalimbali za kodi za nchi yetu.
Hilo ni kosa la jinai pia kwa mujibu wa Sheria yetu kuu ya jinai, yaani Kanuni ya Adhabu, na kwa Sheria yetu ya TAKUKURU.
Pili, kama Mkuu wa Mkoa Makonda hajawataja hao marafiki au wafanya biashara anaodai wamempa zawadi ya makontena hayo, hilo ni kosa la jinai kwa mujibu wa Sheria ya TAKUKURU na Sheria ya Mapato ya Udhalimu (Proceeds of Crime Act).
Tatu, kama Mkuu wa Mkoa Makonda amepokea zawadi zinazodaiwa kuwa kwenye makontena kinyume na Sheria ya Misaada, Mikopo na Dhamana za Serikali uliyoitaja wewe mwenyewe, basi sio tu amekiuka masharti ya lazima ya Sheria hiyo, atakuwa pia amekiuka masharti ya lazima ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuhusu zawadi kwa viongozi wa umma.
Mheshimiwa Rais,
Kwa makosa yote haya, haitoshelezi na haitatosheleza kwa Mkuu wa Mkoa Makonda kuambiwa alipe kodi anayodaiwa tu halafu yaishe.
Kama wasi wasi wako ni wa kweli, na hatuna sababu za kukukanusha juu ya hilo, basi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ni mhalifu anayetakiwa kufukuzwa kazi mara moja, kuchunguzwa kijinai na kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria kulingana na makosa yake.
Sisi raia wako wa kawaida tunatarajia kwamba, kwa vile na wewe mwenyewe umeanza kutambua hatari ya viongozi wa aina hii kwa maslahi ya umma, hutafumbia macho vitendo vya kihalifu ambavyo inaelekea vimefanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Vinginevyo, Mheshimiwa Rais, sisi wananchi wako wa kawaida tutakuwa na sababu halali ya kuamini hii minong’ono tunayoisikia chini kwamba Mkuu wa Mkoa Makonda ana ubia mkubwa katika Urais wako.
RAIS KAMA MFANO WA UONGOZI
Mheshimiwa Rais,
Kama Rais, Mkuu wa Nchi na Kiongozi Mkuu wa Serikali, wewe ni ‘First Citizen’ (Raia Nambari Moja), kama Wamarekani wanavyopenda kusema. Kwa sababu hiyo, unatakiwa kuongoza kwa kuonyesha mfano.
Kwa hoja ya kuzingatia sheria uliyoizungumza kwenye hotuba yako, wewe mwenyewe ndiye unayetakiwa kuonyesha mfano wa kuheshimu Utawala wa Sheria.
Viongozi wengine wote hufuata kwanza mfano na msimamo unaowekwa na Kiongozi Mkuu wa Nchi. Kama Mkuu wa Nchi anaendesha nchi kama mali yake binafsi na anaona wananchi wake kama watwana wake wa kutii amri na maagizo yake bila mjadala, basi viongozi wote wa chini yake nao wataendesha ofisi au idara zao kama mali zao binafsi, na watawaona walio chini yao kama punda wa kubebea mizigo yao.
Nchi inayotawaliwa namna hii haiwezi kuwa tofauti na Zaire ya Mobutu Sese Seko, na haiwezi kuchukua muda mrefu bila kuingia kwenye machafuko na hata kuparaganyika.
GHARAMA ZA KUTOZINGATIA SHERIA
Mheshimiwa Rais,
Madhara ya viongozi wetu wa umma kutokuzingatia Utawala wa Sheria yamekuwa, na yanaendelea kuwa, na gharama kubwa kwa nchi yetu. Ni wiki hii tu, kwa mfano, tumepata taarifa ya Serikali ya Tanzania, kupitia Shirika letu la Ugavi wa Umeme (TANESCO), kushindwa kesi katika Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID).
Sasa, kwa sababu ya kushindwa kesi hiyo, Serikali yako inatakiwa kuilipa Standard Chartered Bank Hong Kong, dola za Marekani milioni 170 au takriban shilingi za Tanzania bilioni 425.
Na wala sihitaji kukukumbusha madhara ya kupuuza kulipa deni hili jipya na kwa wakati muafaka. Serikali yako isipolipa deni hilo sio tu kwamba litaongezeka kwa sababu ya riba na faini nyinginezo, bali pia mali za Serikali yako zitakuwa halali kukamatwa popote zitakapokutwa nje ya nchi yetu.
Yaliyotokea Canada kwa Bombardier yetu mwaka jana, yanaweza kutokea tena kwa Dreamliner ya sasa endapo itafanya safari nje ya Tanzania, na jitihada zako za kufufua ATCL zitakuwa ni kazi ya bure.
Mheshimiwa Rais,
Hasara hii kwa Taifa letu ilikuwa inajulikana na tungeweza kuiepuka, kama viongozi wetu wa Serikali ya Awamu ya Nne wasingekula njama za kuiba na kulipana zaidi ya shilingi bilioni 309, zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow ya Benki Kuu ya Tanzania.
Mimi mwenyewe, na Wabunge wengine, tulitoa tahadhari bungeni Dodoma kwamba Serikali na TANESCO ilikuwa inakabiliwa na kesi ICSID kuhusu fedha hizo za Tegeta Escrow Account, na kwamba tukishindwa kesi hiyo tutatakiwa kuzilipa kwa wanaotudai. Tulijibiwa kwa kejeli na viongozi wa serikali kwamba sisi ni nchi huru na hatuwezi kuogopa kushtakiwa na taasisi au mtu yeyote. Matokeo ya kiburi hicho ndio haya ambayo yametokea wiki hii.
Katika suala hili, na kama sehemu ya utekelezaji wa kauli yako ya leo, tunatarajia, Mheshimiwa Rais, kwamba utaelekeza kuwa faili la Kesi ya Tegeta Escrow Account liangaliwe upya na mamlaka zenye wajibu huo, ili wale wote waliohusika kuliingizia Taifa letu hasara hii wachukuliwe hatua stahiki za kijinai.
Haiwezekani, na itakuwa ni doa kubwa kwako na kwa Serikali yako, kwamba watu pekee ambao wamechukuliwa hatua kutokana na ‘kuchotwa’ kwa mabilioni ya Tegeta Escrow Account hadi sasa ni Mzee James Rugemalila na Harbinder Singh Sethi peke yao.
Viongozi wa umma wa ngazi zote walioruhusu pesa hizo kutolewa Benki Kuu, au ‘waliochotewa’ mabilioni hayo, wameepukaje mkono mrefu wa sheria? Tafadhali tuonyeshe kwa vitendo sisi wananchi wako kwamba kauli yako ya leo sio maneno ya bure.
HAKI ZA VYAMA VYA SIASA
Mheshimiwa Rais,
Kwa vile sasa umetambua umuhimu wa viongozi wote kuheshimu Utawala wa Sheria, sisi raia wako wa kawaida tunatarajia kwamba utatembelea kwenye utambuzi huu kwa kutengua makatazo yako kwa vyama vya siasa vya upinzani kuendesha shughuli zao kwa mujibu wa Katiba na Sheria na Kanuni husika.
Katiba yetu inatamka wazi kwamba “Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia… yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.”
Aidha, “mambo yote yahusuyo uandikishaji na uendeshaji wa vyama vya siasa nchini yatasimamiwa kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii na ya sheria iliyotungwa na Bunge kwa ajili hiyo.”
Kwa kuzingatia masharti haya ya Katiba, Bunge lilitunga Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992. Sheria hiyo imevipa vyama vya siasa haki ya kufanya mikutano ya hadhara na maandamano, baada ya kutoa taarifa ya maandishi kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD).
Na, kwa mujibu wa Sheria hiyo, ni OCD peke yake ndiye mwenye mamlaka ya kuratibu na kudhibiti mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya siasa na wafuasi wao.
Aidha, Sheria hiyo imeweka utaratibu na masharti ya vyama vya siasa kupatiwa ruzuku kutoka kwa Serikali ili kuendeshea shughuli zao za kisiasa, ikiwapo mikutano ya hadhara na maandamano.
Sasa, Mheshimiwa Rais, ni karibu mwaka wa tatu tangu upige marufuku mikutano halali ya vyama vya siasa. Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, mamlaka yako kama Rais yanaishia kwenye kuteua Msajili wa Vyama vya Siasa.
Huna mamlaka yoyote juu ya uendeshaji wa vyama vya siasa kama vile kufanya mikutano ya hadhara na maandamano. Umepoka mamlaka ya kisheria ya ma-OCD wakati wewe sio OCD.
Sasa kwa vile umetambua makosa ya kutozingatia sheria zetu, tunatarajia utatengua na kufuta makatazo ya mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya siasa vya upinzani.
Kama ilivyowahi kusema Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora katika mojawapo ya taarifa zake za uchunguzi, sio haki na ni ukiukaji wa sheria za nchi na misingi ya utawala bora, kwa Jeshi la Polisi kutumika kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya siasa vya upinzani wakati mikutano ya hadhara na maandamano ya CCM hayazuiliwi.
HAKI ZA BINADAMU
Mheshimiwa Rais,
Tangu mwaka 1984, Katiba yetu imeweka hifadhi ya Haki za Binadamu kama sehemu muhimu ya Katiba. Sehemu ya Tatu ya Sura ya Kwanza ya Katiba imefafanua haki na wajibu wetu kwa kirefu.
Kwa takriban miaka mitatu sasa, Serikali ya Awamu ya Tano imeleta janga kubwa sana la kukithiri kwa vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu katika nchi yetu.
Kwa mfano, wakati Katiba inapiga “… marufuku mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu ya kumtweza au kumdhalilisha”, Watanzania kadhaa wameteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu za kuwatweza au kuwadhalilisha katika vituo vya polisi au sehemu nyingine.
Wengi wameumizwa vibaya kimwili na kisaikolojia, wengine wamepata vilema vya maisha. Mambo haya yamefanywa na vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo wewe ndiye Amiri Jeshi Mkuu wake.
Wakati Katiba imeweka haki ya kila mtu “kuishi na kupata kutoka kwa jamii hifadhi ya maisha yake…”, watu wengi wameuawa na vyombo vya ulinzi na usalama na makundi ya wahalifu wanaoelekea kupata ulinzi wa vyombo vya dola.
Alfons Mawazo aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Geita hayuko peke yake; wala aliyekuwa diwani wa CHADEMA katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero; au Katibu wa CHADEMA Kata ya Hananasif, Dar es Salaam, au mwanafunzi Aquilina Aquiline wa Chuo cha Usafirishaji Dar es Salaam.
Wapo pia mamia ya wananchi wa maeneo mbalimbali ya wilaya za Mkuranga, Kibiti, Rufiji na Kilwa, ambao wanadaiwa kukamatwa kwenye makazi, mashamba au hata nyumba za ibada na kupotezwa na vyombo vya dola, na baadaye miili yao kuokotwa kwenye fukwe za bahari au ikielea kwenye Mto Rufiji.
Wakosoaji wa Serikali nao wamekiona cha mtema kuni, kama alivyowahi kusema Mwalimu Nyerere. Sio Ben Saanane wa CHADEMA au mwandishi Azori Gwanda tu ambao wamepotea kwa zaidi ya mwaka sasa.
Ni pamoja na Roma Mkatoliki aliyeponea chupu chupu baada ya Watanzania wengi kupiga kelele; na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko ambaye naye amepotezwa na vyombo vya ulinzi na usalama.
Ni pamoja na mimi mwenyewe ambaye wiki ijayo nitamaliza mwaka nikiwa kitandani, baada ya kumiminiwa risasi 16 na wanaoitwa ‘watu wasiojulikana’, ndani ya eneo la nyumba za viongozi wa umma linalolindwa muda wote.
Ninaamini unafahamu kwamba siku ya tukio hilo walinzi wote waliondolewa kwenye maeneo hayo na ‘watu wasiojulikana’ pia.
Mheshimiwa Rais,
Vitendo hivi vimeacha wajane na watoto yatima wengi sana. Kilio cha wajane na yatima hawa; na cha wazazi au ndugu, jamaa na majirani wa wote ambao wamepotezewa uhai wao, au wamefanywa vilema wa maisha, ni kikubwa.
Wote hawa wanastahili kufutwa machozi. Njia mojawapo bora ya kuwafuta machozi yao ni kuweka ukweli wote wa mateso yao hadharani. Ukweli utatuweka huru, kama yanavyosema maandiko matakatifu. Ninakushauri uunde Tume huru na thabiti ya kijaji (Judicial Commission of Inquiry) kuchunguza matukio yote haya na kuweka ukweli wote hadharani.
Njia nyingine bora ya kufuta machozi ya wote ambao sasa wanalia, ni kuhakikisha kwamba vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu vinakomeshwa kabisa; au endapo vitatokea, kuhakikisha vinachunguzwa kwa ukamilifu na mamlaka huru za kiuchunguzi na wahusika wanaadhibiwa kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.
Ukimya wako mwenyewe na wa Serikali yako kuhusu matukio haya umekuwa na kishindo kikubwa. Watu wengi wanaamini, kwa halali kabisa, kwamba Serikali yako inahusika na mambo haya mabaya. Ndio maana umekuwa kimya sana, na matukio haya hayachunguzwi wala wahusika kujulikana na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria zetu.
Baada ya hotuba yako ya leo, huu sasa ni muda muafaka kwa wewe kuchukua hatua stahiki na za wazi wazi kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa kama ilivyoamriwa na Katiba.
HITIMISHO
Mheshimiwa Rais,
Mambo yanayohitaji kufanyiwa kazi ili kurejesha Utawala wa Sheria katika nchi yetu ni mengi sana. Niliyoyasema ni baadhi tu.
Kuheshimu Uhuru wa Mahakama na wa wanasheria; kutokuingilia uhuru na uendeshaji bora wa shughuli za Bunge; kuacha utamaduni wa sasa wa kuwarubuni wabunge, madiwani na viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani kwa kuwapa vyeo vya kiserikali ili wahame vyama vyao; kurekebisha mfumo mzima wa kikatiba, kisheria na kiutendaji kuhusu usimamizi wa chaguzi zetu, n.k., ni maeneo mengine yanayohitaji kufanyiwa kazi ili kujenga Utawala wa Sheria na kuliepusha Taifa letu na hatari ya kuwa ‘a failed state.’
Yote haya, Mheshimiwa Rais, yanahitaji uongozi wako. Ukiwa jasiri na kuyarekebisha historia itakukumbuka na utasifiwa na sisi wote tuliopo sasa, pamoja na vizazi vyetu vijavyo.
Ukiyanyamazia au kuyaendeleza, kwa ukimya au kwa matendo yako, historia pia itakuhukumu vikali na kukuweka katika kundi moja na watesi wengine wa Bara letu na wa kwingineko duniani.
Uamuzi ni wa kwako. Ninatarajia utachagua upande sahihi wa historia.
Nakutakia kila la kheri.
Tundu AM Lissu, MB
Leuven, UBELGIJI