magufuli88Wiki iliyopita mwandishi wa makala hii ndugu Kalisti Mjuni, alizungumzia umuhimu na mbinu bora za kuandaa walimu. Katika sehemu ya pili, leo Mjuni anazungumzia mahitaji ya msingi kwa utoaji wa elimu bora. Endelea…

Mazingira bora. Ili kazi yoyote iweze kufanyika kwa ufanisi, hatuna budi kuweka vizuri mazingira ya kufanyia kazi hiyo, hali kadhalika, ili tuweze kutoa elimu bora, hatuna budi kuboresha mazingira ya kutolea elimu. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu, inapaswa ifanye mambo yafuatayo katika kuboresha mazingira ya kutolea elimu:

1. Kujenga madarasa ya kutosha kusomea wanafunzi kuepuka wanafunzi kusomea chini ya miti kama ilivyo katika shule ya msingi Majimatitu iliyopo Mbagala Wilaya ya Temeke mkoa wa Dar es Salaam; 2. Kuongeza idadi ya madawati ili kila mwanafunzi akae kwenye dawati tofauti na ilivyo sasa, ambapo baadhi ya shule za msingi wanafunzi bado wanakaa chini;

3. Kuongeza idadi ya matundu ya vyoo kwa shule ambazo zina upungufu wa matundu ya vyoo; 4. Kujenga maktaba katika kila shule ya msingi ili kuweka vitabu vya kutosha vitakavyowajengea wanafunzi utamaduni wa kusoma na kuwafanya wapate maarifa stahiki. Asilimia kubwa ya maarifa tunayopata hutokana na kusoma vitabu na asilimia ndogo iliyobaki hutokana na kuona na kusikiliza;

5. Kupunguza idadi ya wanafunzi katika chumba kimoja cha darasa. Kwa kawaida chumba cha darasa kinapaswa kiwe na wanafunzi arobaini na tano (45) ili mwalimu aweze kuwamudu vizuri wanafunzi, hali ilivyo katika shule zetu nyingi za msingi na sekondari ni tofauti, ambapo chumba kimoja utakuta kina zaidi ya wanafunzi hamsini (50).

Kwa mfano katika Shule ya Msingi Buhongwa A iliyopo wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza, darasa la kwanza chumba kimoja kina wanafunzi 188 na katika Shule ya Sekondari Ula iliyopo Halmashauri ya Mji wa Kondoa, Mkoa wa Dodoma chumba kimoja cha kidato cha kwanza kina wanafunzi 102.

6. Kuwaandikisha na kuwapangia wanafunzi shule ambazo zipo karibu na makazi yao. Hii itasaidia kuondoa usumbufu wa kugombania magari kwa wanafunzi na hivyo kujikuta wakifika shuleni wakiwa wamechelewa  na kukosa baadhi ya vipindi. Pia wanafunzi wanaosomea mbali na makazi yao hufika nyumbani wakiwa wamechoka na kushindwa kujisomea. Hali hiyo huchangia kutofanya vizuri katika masomo yao.

Mheshimiwa Rais nakupongeza kwa kuanza kushughulikia baadhi ya changamoto za kuboresha mazingira ya shule kwa kuwaagiza wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuhakikisha kwamba kila shule inapata madawati ya kutosha. Nina imani kwamba hilo litafanikiwa, tunapaswa kuendelea kushughulikia changamoto nyingine.

Vitabu bora. Hizi ni nyenzo muhimu katika kutolea maarifa. Ili tuandae taifa lenye watu wenye maarifa sahihi, hatuna budi kuwa na vitabu bora vya kiada na ziada. Utaratibu wa kupata vitabu bora vya kiada, unapaswa uwe wa kiushindani na ufanywe kwa umakini mkubwa na usimamizi mzuri.

Unapotaka kupata kitu chenye ubora, huna budi kuweka ushindani. Mfano mzuri ni pale mwajiri anapotafuta mfanyakazi mwenye taaluma Fulani. Mwajiri hulazimika kuwafanyia usahili watu wengi wenye taaluma hiyo ili apate mfanyakazi mmoja mwenye sifa na uwezo mkubwa wa kiutendaji kuliko wengine.

Suala la uandishi wa vitabu vya kiada limekuwa likiiyumbisha sekta ya elimu kutokana na kutokuwa na mfumo maalumu wa kupata vitabu hivyo. Kwa mfano, kabla ya mwaka 1991, jukumu la kuandika vitabu lilikuwa la serikali kupitia Taasisi ya Elimu, ambapo kitabu kimoja cha kiada kilitumika kwa kila somo kwa shule zote za Tanzania Bara.

Matokeo yake hayakuwa mazuri kutokana na kutokuwa na vitabu vya kutosha na vilivyokuwa chini ya kiwango. Kwa kuliona hilo, mnamo mwaka 1991, Wizara ya Elimu ilipitisha utaratibu mpya wa uzalishaji na usambazaji wa vitabu vya kiada shuleni na vyuo vya ualimu, ambapo jukumu hilo walipewa wachapishaji binafsi na serikali ilishirikiana na kampuni hizo kwa kuleta kampuni iliyobobea katika mambo ya vitabu kutoka Swiden kwa lengo la kuzimarisha kampuni.

Matokeo yake yalikuwa mazuri, kwani tulifanikiwa kupata vitabu vya kiada vilivyokuwa na ubora unaotakiwa, ambavyo tunavitumia hadi leo. Rejea vitabu vya kiada vinavyotumika katika shule za msingi. Mnamo mwaka 2014, serikali ilibadilisha tena utaratibu wa kuandaa vitabu vya kiada kwa kuitaka Taasisi ya Elimu Tanzania iandae vitabu hivyo. Wasiwasi wangu ni kwamba, je, tutapata vitabu bora vya kiada?

Ikumbukwe kwamba, kazi ya Taasisi ya Elimu ni kufanya tafiti mbalimbali zinazohusiana na mambo ya elimu, kutunga mitaala na mihitasari, kutoa semina kwa wadau wa elimu kuhusu namna ya kuitumia mitaala na mihitasari, kutoa ushauri kwa wadau wa elimu kuhusu mambo yanayohusiana na elimu na kuthibiti ubora wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Majukumu haya ni makubwa kama yatafanywa kikamilifu. Kazi ya kuandaa vitabu inahitaji wataalamu wenye vipaji na elimu hiyo, wahariri, wachoraji waliosomea taaluma hiyo, wapangaji wa vitabu, watu wa masoko kwa ajili ya kusambaza vitabu nchi nzima, mtaji wa kutosha kuzalisha na kusambaza vitabu idadi yoyote ya vitabu itakayohitajika.

Tukitaka kupata vitabu vya kiada vyenye ubora unaotakiwa, jukumu la kuandaa vitabu tuliache kwa kampuni binafsi ya vitabu yenye wataalamu wa idara zote za uandishi wa vitabu, kisha Kamati ya Ithibati ya Vifaa vya Kielimu nchini (EMAC) ivipitie na kuona ni vipi vinafaa kupewa muhuri wa ithibati na mwisho TAMISEMI kupitia wataalamu wake, ichague vitabu vya kiada miongoni mwa vitabu vilivyopitishwa na EMAC. Tukifanya hivyo tutapata vitabu bora vitakavyowapa maarifa sahihi wanafunzi wetu. Tujifunze kutoka mataifa ya wenzetu yaliyofanikiwa katika sekta ya elimu.

 Mfumo wa Elimu. Mheshimiwa Rais, baada ya kuelezea namna ya kuboresha elimu yetu, naomba nielezee kwa ufupi kuhusu mfumo wetu wa elimu. Mfumo wa elimu ni utaratibu ambao nchi inajiwekea katika kutoa elimu kwa wananchi wake. Mfumo wa elimu unaweza kubadilika kulingana na mahitaji ya wakati husika.

 Ikumbukwe kwamba msingi mkuu wa mabadiliko ya mfumo wa elimu ni utafiti uliofanywa kwa umakini mkubwa katika shule zetu kwa kushirikisha wadau wote wa elimu na kubaini upungufu uliopo. Mabadiliko yanayofanywa katika mfumo wa elimu yanapaswa yaboreshe na si kuharibu mfumo uliopo. Nina mashaka kama mabadiliko yaliyofanywa katika mtaala na mihitasari yataboresha elimu yetu.

 Sikatai kufanya mabadiliko lakini, tunapaswa tujiulize, “mabadiliko tunayofanya yana faida gani kwetu?” Tusije tukafanya mabadiliko kwa kisingizio cha kwenda na wakati. Tunaweza kubadili mfumo wa elimu, lakini kama hatujaboresha mafiga matatu ya elimu bora, hali inaweza kuwa ileile au ikawa mbaya zaidi ya ilivyokuwa mwanzo.

 Tatizo la wanafunzi wetu wa shule za serikali kutofanya vizuri katika masomo yao sio mfumo wa elimu tulionao bali ni usimamizi mbovu wa mfumo. Nasema hili nikiwa na ushahidi wa kutosha. Tukitaka kujua kuwa mfumo wa elimu tulionao ni mzuri, tuangalie shule binafsi. Shule hizi zinatumia mfumo huo huo unaotumiwa na shule za serikali, lakini wanafunzi wake wanafanya vizuri katika masomo yao ya ngazi ya msingi na sekondari.

 Mfano mzuri angalia matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne wa mwaka 2015, shule zilizoingia kumi bora zote ni shule binafsi. Naomba nizitaje kwa mtiririko wa ya kwanza hadi ya 10. Kaizirege (Kagera), Mwanza  Allience (Mwanza), Marian Boys (Pwani), St. Francis Girls (Mbeya), Abbey (Mtwara), Feza Girls (Dar es Salaam), Canossa (Dar es Salaam), Bethel Sabs Girls (Iringa),  Marian Girls (Pwani) na Feza Boys (Dar es Salaam).

 Sio mwaka huo tu ambapo shule binafsi zilifanya vizuri, tukiangalia miaka miwili ya nyuma bado shule binafsi ziliongoza. Wanafunzi wengi waliosoma katika shule hizo za sekondari, walisoma shule za msingi binafsi. Iweje leo tuseme mfumo wetu wa elimu ni mbovu?

 Ni mambo gani yanafanya shule binafsi zifanye vizuri? Moja, msingi mzuri wanaowapatia watoto katika elimu ya awali. Watoto wanapomaliza elimu ya awali katika shule binafsi wanakuwa na uwezo mzuri wa kusoma na kuandika, pia wanakuwa na hali ya kuipenda shule kutokana na msingi mzuri wa elimu walioupata.

 Pili, mfumo mzuri wa kuendesha shule. Walimu wengi wanaofundisha shule binafsi wamesoma shule na vyuo vya aina moja na walimu wanaofundisha shule za serikali. Kinachowafanya wafanye kazi kwa bidii ni mfumo waliowekewa shuleni; mafao yao.

Tatu, upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kijifunzia. Katika shule binafsi, wanafunzi wanatakiwa wawe na vitabu vyao vya kiada na ziada kwa masomo yote, hii inawasaidia kujisomea wenyewe hata wanapokuwa nyumbani.

Nne, mazingira mazuri yenye mahitaji yanayotakiwa kwa walimu na wanafunzi; tano, walimu wa kutosha; sita, uongozi mzuri wa shule wenye uwezo wa kusimamia vizuri mfumo uliowekwa na utoaji wa motisha kwa walimu ambao wanfanya vizuri katika kazi yao.

Mheshimiwa Rais, mambo haya yanaonekana kuwa mengi, lakini yanaweza kufanikiwa endapo serikali itashirikiana na wananchi wake. Kama serikali iliyopita ilishirikiana na wananchi kujenga maabara, kwa nini serikali hii ishindwe kuyapatia ufumbuzi hayo niliyoyataja?

 

Wasalaam,

Kalisti Mjuni

Mdau wa elimu

0762488763

Email: [email protected]

 

Kalisti Mjuni ni msomaji mzuri wa Gazeti la JAMHURI. Anaamini kupitia makala hii na kupitia gazeti la JAMHURI ujumbe huu utamfikia Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magudfuli na wenye dhamana na elimu watayafanyia kazi. Mhariri.