Ustaarabu wetu adhimu wa Kiafrika tuliourithi kutoka kwa wahenga wetu, unatutaka vijana kuwa na heshima na kufanya maamkizi kwa wakubwa. Shikamoo Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli.
Ninakuandikia barua hii nikifahamu pasi shaka yoyote kuwa kamwe hutaishangaa. Kama ujuavyo, uandishi wa barua za namna hii una historia ndefu tangu zama za Uyunani za mwanafalsafa Plato, na hata karne nyingi kabla yake.
Ni imani yangu kuwa barua ya Patrice Emery Lumumba, kiongozi wa iliyokuwa Kongo ya Ubelgiji, kwenda kwa mkewe, Pauline wakati Lumumba akiwa chini ya udhibiti wa waasi kabla ya uhai wake kupokwa kinyama kwa msaada wa mabeberu wa ng’ambo, ambao sasa ndiyo wahubiri wetu wakubwa wa haki za binadamu, unaifahamu.
Katika barua yake alieleza bayana siku yaja wana wa Afrika wataiandika historia yao badala ya ile feki inayoandikwa kwa kalamu feki za Washington, Brussels na London. Unadhani barua ya Lumumba yalikuwa maneno matupu na ndoto ya mchana ambayo haitotimia kamwe?
Mwandishi na mwanamapinduzi, Frantz Fanon, kwenye kitabu chake cha ‘The Wretched of the Earth’ anasema ‘Kila kizazi kina jukumu lake, ni lazima kiutambue wajibu wake halafu kiutekeleze au kiusaliti’. Ni sisi wenyewe wenye kuandika historia yetu. Kamwe hatuwezi kulikamilisha jukumu la kukikomboa kizazi chetu kiuchumi kama tutakuwa na hofu ya kupambana na maovu katika jamii. Hakuna njia rahisi ya kuufikia uhuru popote duniani.
Ndugu Mheshimiwa Rais, kwanza nikupongeze kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miaka mitano kikatiba. Niseme tu kuwa umechaguliwa kipindi ambacho Taifa linahitaji kiongozi atakayeweza ‘kufa kidogo’ ili kuweza kuwakomboa wanyonge ndani ya Taifa hili wakiwamo wakulima, wafugaji na wafanyabiashara wadogo. Ni kipindi ambacho Taifa letu linahitaji kiongozi mwenye moyo wa dhati kabisa na wa kishujaa wa kuweza kupambana na ‘ebola’ ya uozo kama wezi, uongo, ubinafsi, unafiki, upenda rushwa, ulaghai, umalaya wa kisiasa, utapeli, uvivu wa kufikiri na kufanya kazi, uonevu, uroho, ufisadi na uzembe ndani ya Serikali ili kuitoa jamii ilipo sasa katika uozo huu.
Sitanii, kama kaka yangu Deodatus Balile anavyopenda kusema, hili halihitaji wananchi wawe na digrii kulijua, hata wafugaji wa Nanga, Gibishi, Halawa, Lagangabilili, Lung’wa, Nkindwabiye, Ihusi, Mwamtani, Ng’walali, Butindi, Ng’alita na kwingineko wanaoishi machungani muda wote wanalijua.
Pili, nikupongeze kwa kazi nzuri ulizozifanya kwa muda huu mfupi baada ya kuingia madarakani ukiachilia mbali historia ya utendaji wako wa kazi wa nyuma. siwezi kuyaelezea yote ila niseme tu kuwa umeonesha imani kubwa sana kwa Watanzania kuwa wewe ni kiongozi wa Watanzania wote hasa wanyonge baada ya kufuatilia, kubaini na kujiridhisha kuwa Watanzania wachache wanakula mlungula na kufaidi rasilimali za Taifa hasa ufisadi uliokuwa ukifanyika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Wizara ya Fedha, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na baadaye kuwasimamisha kazi wakurugenzi wa taasisi hizo na taasisi nyingine pale ulipoona moshi unafuka na kushikilia mali zao kwa uchunguzi zaidi, yakiwamo mahekalu yale 73 ya jamaa yetu wa TRA ukitumia falsafa yako ya ‘kutumbua Majipu’, msemo ulioenea kila kona mitaani na vijijini.
Inahitaji uwe na roho ngumu Mh. Rais mithili ya mwendawazimu kumiliki mahekalu 73 huku zahanati za vijijini hazina dawa, wamama wanajifungulia njiani kama siyo chini ya miti, watoto wanakaa chini hawana madawati, miundombinu ni mibovu, ama haipo kabisa, kwa ajili ya usafirishaji wa mazao kutoka maeneo ya vijijini.
Umeenda mbali zaidi kwa kuzuia na kufuta safari zisizokuwa za lazima nje ya nchi kwa wakurugenzi wa wizara, taasisi na sekta mbalimbali kwa lengo la kupunguza/kudhibiti matumizi ya Serikali ili kuondokana na bajeti tegemezi ya kila mwaka maarufu ‘kwa hisani ya’.
Na hukuishia hapo, umeagiza wakuu wa mikoa kuleta taarifa za watumishi hewa ndani ya mikoa yao ili kuweza kupambana na ‘ebola ya mishahara hewa’ ndani ya Serikali na umeokoa mabilioni yaliyokuwa yakiishia mifukoni mwa waliokuwa wanajiita wajanja na hata kusababisha kutengua uteuzi wa mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anna Kilango Malecela, na Katibu Tawala wa Mkoa huo, baada ya kutoa taarifa zisizokuwa za ukweli.
Lakini, umeendelea kusisitiza Watanzania kufanya kazi kwa falsafa yako ya ‘Hapa kazi tu’ kwa lengo la kujenga uchumi imara na maendeleo dhabiti katika taifa. Hata wale wacheza ‘gologolo’ (kwa Kisukuma) kama pool table na mingine, watashiriki kikamilifu kuinua uchumi wa Taifa lao. Japo wachezaji wa pool table wanalipa kwa mmiliki, siamini kama wamiliki hawa wanalipa hata mapato na hata kama wanalipa haiwezi kulingana na kile ambacho kama vijana hawa watazalisha katika kilimo (mfano matikiti maji), ufugaji (mfano kuku wa kienyeji) au biashara ndogondogo.
Historia inatufundisha kuhusu masaibu zilizopitia nchi za Vietinam, Malaysia, Bangladesh na Pakistan. Kama ni nchi kuwa maskini basi nchi hizi zilikuwa zinafaa ziwe na siyo Tanzania.
Umeonesha falsafa nzuri sana kwa ukuaji imara na maendeleo thabiti kiuchumi, hii inatokana na ukweli kwamba ili Taifa changa liweze kuendelea kiuchumi, ni lazima litumie kile kilicho chake yaani rasilimali watu, madini, gesi, ardhi, mifugo, chakula, misitu na wanyamapori.
Pia nichukue fursa hii kukupongeza kwa jinsi unavyoitumia karama na taaluma yako kutukomboa kifikra sisi ‘wasakatonge’ tulio kwenye giza totoro. Naamini bado unazikumbuka nasaha za Mwalimu Julius Nyerere alivyowaasa wasomi kwenye kongamano la wanazuoni (Juni 27, 1966), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwamba jukumu kuu la mwanazuoni wa chuo kikuu ni kuutafuta ukweli, kuuzungumza kadiri anavyouona na kuusimamia kwa uthabiti bila kujali gharama yake. Je, na wewe upo tayari kuuzungumza na kuusimamia ukweli mpaka mwisho wa dahari mheshimiwa?
Kwa hakika nafahamu kwamba kuusimamia ukweli kuna gharama kubwa. Lakini, kama inavyofahamika tangu mwanzo wa dunia mpaka sasa, hakuna jipya linaloweza kumwandama mzalendo yeyote ambalo wasema kweli wengine duniani hawajalipitia. Wanatheolojia wanatujuza kwamba hakuna jipya chini ya jua kwa sababu yaliyokuwapo ndiyo yatakayokuwapo; na yaliyotendeka ndiyo yatakayotendeka.
Tangu dunia ya kale historia imetufunza kwamba ipo gharama ambayo kila msema kweli duniani anapaswa kuwa tayari kuilipa kwa kujiingiza kwenye jukumu la kuwa sauti ya wanyonge wasio na sauti.
Ni hatari gani inayoweza kumkabili msema kweli hapa duniani kushinda dhoruba ya mlipuko garini iliyotupokonya kipenzi chetu, Profesa Walter Rodney, na unyama wa maharamia wa Kenya uliowaangamiza Komredi Tom Mboya na Dk. Robert Ouko kwa sababu ya uchu wa madaraka na kukemea rushwa na ufisadi ndani ya serikali?
Nakumbuka wakati Profesa Issa Shivji anastaafu uhadhiri mwaka 2006, alitueleza kinagaubaga kwamba katika kipindi chote cha maisha yake, anajivunia sana kipindi kile cha harakati za ujanani. Lakini, kama walivyofafanua, makomredi wengi wa miaka ile wakiwa makinda wa chuo kikuu ambao sasa ni wakuu wa nchi, wanasiasa nguli na maulamaa wabobezi wa fani mbalimbali, hivi sasa wanauonea soni ukweli kwamba na wao walikuwa wanaharakati wakubwa wa ujamaa enzi za ujanani kwa vile sasa wameipokea dini mpya; dini ya ubeberu inayowashushia pepo, neema na ukwasi hapa hapa duniani!
Jambo pekee linalotia mshawasha mkono wangu kuandika barua hii ni kiu yangu ya kutoa maneno yenye kufaa, maneno ya kuwatia moyo na kuwahamasisha wanyonge kama zinavyofanya barua nyingi katika historia ya ulimwengu.
Kwanza; tunafurahi kuona umechagua kuwa upande wetu wanyonge. Prof. Issa Shivji amewahi kutufunda kuhusu thamani ya kalamu ya mwanazuoni (Rejea kitabu chake cha Insha za Mapambano ya Wanyonge). Alisema bila kumung’unya maneno kwamba silaha pekee ya mwanazuoni ni kalamu yake na kwamba ni lazima mwanazuoni aitumie kalamu yake kwa uthabiti kila anapopata nafasi kuwasemea wanyonge wasio na sauti hususani wakulima na wafugaji.
Binafsi sina maneno toshelezi kuipambanua thamani ya kalamu ya mwanazuoni wa wanyonge zaidi ya sifa zilizotolewa na ndugu Kajubi Mukajanga kwenye shairi lake la ‘You write’ (Rejea kitabu cha ‘Summons: Poems from Tanzania’).
Inanilazimu kuzitafsiri beti za ndugu Kajubi kwa Kiswahili kwa sababu nakala ya barua kwako nimeisambaza pia kwa umma wa wanyonge wa uswahilini na vijijini – wanyonge ambao mfumo wetu shelabela wa elimu umewafanya wengi wao kuwa wahitimu wa shule za kata wasioweza kuunganisha hata sentensi tatu za Kizungu kwa ufasaha! Ndugu Kajubi anamsifia msomi na kiongozi wa wanyonge kwa maneno yafuatayo;
You weep with them
Unalia pamoja nao (wanyonge)
You sigh with them
Unahema nao (wanyonge)
You suffer with them
Unataabika nao(wanyonge)
But you lift high
Lakini unainua juu
The banner of their struggle
Bendera ya harakati yao
With your sacred pen
Kwa peni yako takatifu!
Naam, hayo siyo maneno yangu. Hayo ni maneno ya Kajubi kuhusu msomi na kiongozi wa wanyonge. Wanyonge wakiteseka, na yeye anahisi kuteseka; wakihema na yeye anatweta; wakilia na yeye anabubujikwa na machozi ya uchungu! Ndiyo, ni kupitia kalamu yake iliyotukuka, bendera ya harakati za wanyonge inainuliwa juu zaidi na kupepea kudhihirisha ushindi wa umma wa walalahoi.
Kwa hakika beti hizi za Kajubi zinawahusu viongozi wa aina yako na waandishi sampuli ya Komredi Abdilatif Abdallah. Si unakumbuka huyu bwana alipowekwa gerezani na Mzee Jomo Kenyatta kwa kuhoji Kenya inakokwenda? Je, alitokwa na machozi kwa kadhia na misukosuko ya kuswekwa korokoroni? Upweke wa gerezani ulimkatisha tamaa? La hasha, si unakumbuka alivyoendelea kuandika kazi zake za kiukombozi akiwa jela kwa kutumia karatasi za chooni (toilet paper)?
Nikiwa sekondari, nilipata bahati ya kusoma na kusimuliwa habari kuhusu uchumi na maisha kipindi cha miaka ya 1970 na ya 1980 hasa katika kipindi ambacho nchi hii ilipokuwa na misingi ya ‘Ujamaa na Kujitegemea’, falsafa zilizokuwa ndani ya Azimio la Arusha. Tulisoma na kuelezwa kuwa Azimio liliwataja wakulima na wafanyakazi kuwa ndiyo wamiliki wake wakuu wa uchumi wa nchi hii. Hatukukurupuka kufanya hivyo, tuliweza kuandaa sera nzuri katika kilimo na ufugaji (Sera ya Kilimo na Mifugo 1977 na 1987) zilizotufanya tuzalishe malighafi zetu wenyewe kupiti mifugo yetu na kilimo. Mfugaji na mkulima walithaminiwa kwa kuwa injini ya uchumi wa taifa kwa kujengewa majosho ya kuogeshea mifugo na maeneo ya kutosha kwa ajili ya kuchungia ili wazalishe malighafi zenye ubora wa hali ya juu. Babu yangu, Mzee Nindwa Ngunda, huwa apenda kusema sasa hivi tunafuga ng’ombe ambao ni sawa na ndama wa zamani.
Kupitia misingi hiyo tuliweza kujenga viwanda vya kati sisi wenyewe, vilivyoweza kusindika mazao ya mifugo na kilimo tuliyoyazalisha sisi wenyewe huku tukitumia wataalamu wetu wachache tuliokuwa nao kipindi hicho (hapa nawaongelea akina Mzee Cheyo waliokuwa wataalamu wetu wa kuchanganya rangi kule Mwatex) kama viwanda vya kati vya pamba (Mwatex, Mutex, Sunguratex), viwanda vya kubangulia korosho Mtwara, viwanda vya katani na viwanda vya nyama na ngozi (Shinyanga na Musoma). Kutokana na ‘sera muflisi’ tulizokuja nazo kwa kusema kuwa Azimio limepitwa na wakati na kuja na sera za ubinafsishaji wa viwanda vyetu tukamtupilia mbali mkulima na mfanyakazi na kuvifanya viwanda vyetu kuwa makazi ya popo. Ukipita karibu na kilichokuwa kiwanda cha nyama Shinyanga lazima ububujikwe na machozi.
Wale tuliowapa viwanda hivi waviendeshe kwa kuwa Serikali haiwezi kufanya biashara, wako wapi hii leo? Au ubora wa ile mifugo tuliyoizalisha haipo tena? Hata kwenye Ranchi za Taifa (NARCO) mifugo ya ubora haipo? Au ndiyo zimwi la kuacha misingi ya Azimio la Arusha na kuja na Azimio la Zanzibar? Unakumbuka uliyoyasema mwaka jana ulipokuwa ukiomba ridhaa kwa Watanzania hasa maeneo ya wafugaji ili uwatumikie? Mimi nayakumbuka maneno uliyoyaongea ulipokuwa unahutubia mkutano wa hadhara Jimbo la Itilima kwa Mheshimiwa Njalu Daud Silanga tukiwa pale Kijiji cha Nangana, baadaye ahadi hiyohiyo ukaitoa kwa wananchi wa Lagangabilili baada ya msafara wako kusimamishwa ulipokuwa ukielekea Jimbo la Kisesa wilayani Meatu. Na baada ya wewe kuondoka ahadi hiyo tuliendelea kuinanga na kuinadi majukwaani kwa wananchi kwa kuikopi na kuipesti.
Ulisema kwa Kisukuma kuwa ‘unene hu Magufuli na’dume ghampagha duhu, naghunyosha unkono one aho ghugelela mghudimila’ ukimaanisha ‘Mimi ndio Magufuli nishindwe kupanua mpaka wa kuchungia tu? Nitanyoosha mkono wangu utakapokomea ndipo itakuwa mwisho wa eneo lenu la kuchungia mifugo’.
Hiyo haikuwa ahadi pekee na maneno matupu bali pia ulionesha namna gani unavyotambua mchango wa sekta ya kilimo na ufugaji katika Taifa changa kama hili kiuchumi na unavyouthamini mchango wa sekta hii katika Taifa kwa ukuaji imara na maendeleo thabiti kiuchumi.
Ni katika ahadi hiyo ‘Tanzania ya Viwanda’ inawezekana tukienda sambamba na upunguzaji wa tatizo la ajira nchini maana mwajiri mkuu duniani ni viwanda.
Sasa wafugaji wameagizwa kutochungia katika eneo la hifadhi na kuwataka kuheshimu utaratibu uliowekwa na mamlaka, jambo ambalo ni sahihi kabisa hasa kwa wale wanaochungia pembezoni mwa hifadhi kama vile Nkindwabiye, Ihusi, Mwashagata, Matongo, Ng’alita (kijiji nilichozaliwa na ninachoishi mpaka sasa), Ng’walali, Lung’wa, Gibishi, na vingine.
Kuna tofauti gani kwa wafugaji wa Nanga na Lagangabilili wale uliowapa ahadi hiyo (Jimbo la Itilima) na wafugaji wa Ihusi, Nkindwabiye, Matongo, Ng’alita, Halawa, Gibishi, Butindi na maeneo mengine ya nchi hii?
Hapa sijaongelea makundi makubwa ya mifugo yaliyopo kwenye mapori ya hifadhi Mpanda, Kigoma, Geita (Butindi) na maeneo mengine ya hifadhi na mapori tengefu.
Sasa mpaka badala ya kupanuliwa kwenda ndani ya hifadhi kama ahadi yako mheshimiwa, umewafuata wafugaji nje wakitakiwa wavuke mita 500 kutoka mpakani. Ni lini mkono wako sasa utaunyoosha mbele badala ya kurudi nyuma kwenye mipaka ya hifadhi kama wafugaji nchi nzima ulivyowaahidi? Au hatukukuelewa vizuri urefu wa mkono ni zile mita 500 kutoka nje ya hifadhi? Sera ya ‘Tanzania ya Viwanda’ tutaitekelezaje bila ya kuiangalia sekta ya ufugaji? Au viwanda vya nyama hatuvifufui tena kwa maana mifugo haina tena faida kwa ukuaji wa uchumi kwa Taifa letu? Au kuna haja gani hawa wafugaji kuendelea kumiliki idadi kubwa ya mifugo huku maeneo ya malisho ni tatizo? Huoni ni muda mwafaka sasa wafugaji hawa kupewa elimu ya ufugaji wenye tija kwao na kwa Taifa ili kuingiza kipato kitakachokuza uchumi wa Taifa letu (GDP)?
Kwa mujibu wa takwimu, nchi yetu ni ya tatu kwa idadi ya mifugo mingi barani Afrika. Idadi hii kubwa ina mchango gani kwa ukuaji wa uchumi wa Taifa letu?
Lakini kabla hatujaendelea na waraka wetu, naomba uniruhusu nikusimulie mchapo mmoja. Si unajua tena vijana tumejaa michapo! Na kwa kweli ujana bila michapo basi unapoteza maana yake!
Wakati nikiwa sekondari, tulisoma historia ya Chifu Machemba. Si unakumbuka jinsi huyu bwana alivyowakoromea Wajerumani walipomtaka kusalimisha himaya yake kwao wakati ule wa kinyang’anyiro cha mabeberu kuigombea Afrika? Nayakumbuka majibu yake kwa Gavana wa Kijerumani mwaka 1890; alisema, “Nimeyasikiliza maneno yako lakini sioni sababu ya kukunyenyekea. Bora nife kwa sababu mimi ni sultani hapa kwenye nchi yangu nawe ni sultani kwenye nchi yako. Kama una nguvu njoo mwenyewe unikamate”.
Naam, hayo yalikuwa maneno ya Chifu Machemba ambaye Wajerumani walipomvamia alipambana nao mpaka tone la mwisho na kuamua kutimkia Msumbiji pale maji yalipozidi unga!
Angekuwa mbinafsi, Chifu Machemba angeweza kuingiwa na uchu na kuiuza himaya yake kwa Wajerumani lakini akachagua maisha ya upweke ya uhamishoni. Mbona watawala wengi wa Afrika ya leo hawalikumbuki darasa hili maridhawa kutoka kwa Machemba? Kwa nini washirikiane na mababeru kutorosha vito, nyara za Serikali na utajiri wetu kwenda ng’ambo?
>>ITAENDELEA