Rais mteule wa Gambia, Adama Barrow, alizaliwa Februari 1965 katika kijiji kidogo cha Jimara, Mankamang Kunda. Historia inaeleza kuwa Barrow alipata elimu yake ya msingi katika shule ya Kunda pamoja na elimu yake ya sekondari nchini Gambia.
Baadaye alikwenda nchini Uingereza mwanzoni mwa miaka ya 2000 kusomea shahada ya Real Estate ambako pia alifanya kazi kama mlinzi ili aweze kumudu gharama ya masomo yake.
Katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni nchini Gambia, ushindi wa Barrow unaweza kufananishwa na ule wa Donald Trump nchini Marekani, kwa misingi kuwa alikuwa hapewi nafasi kabisa ya kushinda katika uchaguzi huo kama vile tu hakuwa na historia yoyote katika siasa.
Duru za kisiasa nchini Gambia zinaripoti kuwa miezi sita kabla ya uchaguzi, jina la Adama Barrow halikuwa likipigiwa chapuo katika medani ya ushindani wa urais nchini Gambia, na wala halikuwa mdomoni mwa wananchi wa Gambia – kuanzia viunga vya mji mkuu Banjul au Mankamang Kunda, eneo ambako alizaliwa.
Barrow amekata ngebe na tambo za dikteta Jammeh ambaye alijinasibu kuwa endapo Mungu atapendezwa naye basi ataongoza taifa hilo kwa miaka bilioni. Hata hivyo, ushindi wa barrow unadhihirisha kuwa hata Mungu pia hakupendezwa na utawala wa Jammeh na ndiyo maana kupitia sanduku la kura, wananchi wa Gambia wameukataa utawala wake wa kiimla.
Kabla ya kuchaguliwa mwezi septemba, 2016 kuwakilisha vyama saba vya upinzani katika uchaguzi wa rais, ambavyo vilikubaliana kumsimamisha mgombea mmoja, Barrow alikuwa ni mfanyabiashara maarufu kupitia kampuni yake aliyoianzisha mwaka 2006, baada ya kurejea kutoka masomoni nchini Uingereza akiwa na uzoefu wa miaka 10 katika biashara.
Rais huyu mteule, kipenzi cha vijana, ameishangaza Afrika na dunia nzima kwa kushinda nafasi ya kisiasa bila kuwa na historia ndefu ya kisiasa kama ilivyokuwa kwa mfanyabiashara Donald Trump aliyeshinda uchaguzi wa Marekani.
Rais huyu mteule ambaye amebeba matumaini ya maelfu ya wananchi wa Gambia kupitia ahadi zake wakati wa kampeni, kama vile kuhakikisha dawa zinapatikana katika hospitali, kuboresha shule ambazo zina vifaa duni, pamoja na miundombinu mibovu.
Anatajwa kuwa ni mtu mstahimilivu, muumini wa dini ya Kiislamu, lakini pia mtu wa kujishusha na kujichanganya zaidi na watu wa kawaida, na ndiyo maana haikuwa taabu kwa yeye kukubali kufanya kazi ya ulinzi wa duka nchini Uingereza mwanzoni mwa miaka ya 2000 alipokuwa akisoma masomo yake ya shahada ya kwanza. Jambo hilo si la kawaida sana kufanywa na watu wanaojiita wasomi.
Licha ya kuwa mpenzi wa kandanda, na mshabiki kindakindaki wa timu ya Arsenal ya nchini Uingereza, Barrow alijinasibu kuwa endapo atashinda uchaguzi atahakikisha Gambia haijiondoi katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC), ambapo rais anayemaliza muda wake aliweka azimio la kuiondoa nchi yake katika Mahakama hiyo, kwa kile kinachodaiwa ni ukandamizaji kwa nchi za Afrika unaofanywa na Mahakama hiyo.
Rais aliyemaliza muda wake, Jammeh, katika mahojiano yake na kituo cha utangazaji cha BBC Uingereza mwaka 2011, aliweka wazi kuwa hatima ya uongozi wake ipo mikononi mwa Mwenyezi Mungu, na pia alisema hashtushwi na shutuma anazopewa na wakosoaji juu ya ukiukwaji wa misingi ya haki za binadamu, pamoja na ukandamizaji wa demokrasia.
Kati ya vitimbi ambavyo vitamfanya akumbukwe ni pamoja na kauli yake ya mwaka 2007 kuwa ana uwezo wa kutibu ugonjwa wa ukimwi kwa kutumia dawa za asili, na uwezo wa kutibu ugumba kwa wanawake, kitu ambacho kilipingwa vikali na wataalamu wa afya nchini Gambia.
Jammeh atakumbukwa kwa hotuba yake kali aliyoitoa mwaka 2014 katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambapo alishutumu vikali nchi za Ulaya kwa kile kinachoitwa kushinikiza ndoa za jinsia moja, ambapo Jammeh alisema kuwa suala hilo ni kinyume na utamaduni wa Kiafrika, kinyume na amri za Mungu lakini pia si kitendo cha kibinadamu.
Kupitia chama cha United Democratic (UDP), Adama Barrow, ambaye kwa mujibu wa katiba ya nchi yao anapaswa kuapishwa tarehe 19 January, 2017 anaandika historia mpya katika uga wa demokrasia Afrika kwa kuwa mmoja ya marais walioshinda uchaguzi kupitia vyama vya upinzani Afrika Magharibi.
Rais huyu mteule ambaye ana familia ya wake wawili na watoto watano, anakabiliwa na changamoto nyingi zilizopo nchini Gambia lakini hasa ni ile ya ukosefu wa ajira kwa vijana, kitendo kinachowalazimu vijana wengi kukimbilia Ulaya kwa ajili ya kutafuta ajira.
+255 712 438307.