Baada ya kukamilisha zoezi la kuimiliki Kampuni ya Acacia Mining, Barrick Gold Corporation ya Canada imeanza kutekeleza mikakati mipya ya kuiendesha migodi iliyokuwa ikisimamiwa na kampuni hiyo, ukiwemo ule wa North Mara uliopo wilayani Tarime.

Mikakati hiyo inayolenga kuongeza ufanisi katika uzalishaji na uendeshaji wa migodi hiyo ya dhahabu hapa nchini ni pamoja na kupunguza wafanyakazi.

Mwanzoni mwa wiki hii Kampuni ya Barrick North Mara inayosimamia mgodi wa dhahabu wa North Mara kwa sasa iliwatangazia wafanyakazi wake kuwepo kwa zoezi hilo litakalohusisha wafanyakazi 110.

Kupitia waraka wa ndani wa tarehe 13/01/2020, kampuni hiyo ilisema tayari imewasiliana na chama cha wafanyakazi katika mgodi huo kwa ajili ya kuanza kutekeleza shughuli hiyo. Kwa mujibu wake, wafanyakazi watakaohusika kwenye zoezi hilo watatoka katika vitengo saba vikiwemo vile vya rasilimali watu, uchimbaji pamoja na ugavi.

“Tangu Barrick ichukue umiliki wa Acacia, tumefanya mapitio ya kina jinsi tunavyofanya kazi ili kubaini kama tuna watu sahihi wenye ujuzi unaotakiwa kwenye nafasi zao za kazi. Haya ni mabadiliko ya kiidara ili kukabiliana na changamoto za uendeshaji na kuongeza ufanisi,” Barrick North Mara inasema kwenye waraka huo uliosainiwa na Meneja Mkuu wa mgodi wa dhahabu wa North Mara,  Luiz Correia.

Barrick ilikamilisha zoezi la kuimiliki Acacia Mining kwa asilimia 100 pamoja na migodi yake yote nchini mwezi Septemba mwaka jana kama sehemu ya kukamilisha mazungumzo na makubaliano yake na serikali kuhusu usimamizi na uendeshaji wa migodi hiyo.

Migodi mingine ambayo sasa iko chini ya Barrick ni ile ya Buzwagi na Bulyanhulu ambayo yote ni miongoni mwa migodi mikubwa ya dhahabu hapa nchini. Acacia ilikuwa kampuni tanzu ya Barrick iliyokuwa ikisimamia na kuendesha migodi hiyo.

Mwaka 2017, Acacia iliingia katika mgogoro na serikali baada ya kubainika kuendesha shughuli zake kinyume cha taratibu ikiwemo ukwepaji wa kodi, vilivyoikosesha nchi mapato makubwa. Baada ya kampuni hiyo kupigwa faini ya dola bilioni 190 za Marekani, Barrick ilianzisha mazungumzo na serikali ili kunusuru biashara zake nchini.

Mazungumzo hayo yalikamilika mwishoni mwa mwaka jana huku pande mbili hizo zikikubaliana pamoja na mambo mengine kuunda kampuni ya pamoja ya kusimamia na kuendesha migodi hiyo mitatu iliyopewa jina la Twiga Minerals Company Limited, ambayo makao makuu yake yatakuwa Mwanza, tofauti na Acacia iliyokuwa ikiendesha shughuli zake kutoka London, Uingereza.

Kwenye kampuni hiyo ambayo inasemekana bado haijaanza kufanya kazi rasmi, Barrick itamiliki asilimia 84 ya hisa zote huku zinazobaki zikiwa mikononi mwa serikali.

Utaratibu huo wa hisa za kampuni hiyo mpya ni utekelezaji wa sheria mpya ya madini iliyopitishwa mwaka 2017 ambayo utekelezaji wake umechangia sana kuongeza uzalishaji wa dhahabu na mapato yake.

Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), fedha za kigeni zilizotokana na mauzo ya dhahabu nje ya nchi katika mwaka ulioishia Novemba 2019 ziliongezeka kwa karibu asilimia 42 na kufika dola milioni 2,139.9 za Marekani ikilinganishwa na dola milioni 1,507.6 kipindi kama hicho mwaka 2018.

BoT inasema ongezeko hilo la mapato ya dhahabu lilitokana pia na kuongezeka kwa bei yake kwenye soko la dunia. Wastani wa bei ya dhahabu kwenye mwaka unaoishia Novemba 2019 ilikuwa dola 1,373.44 kwa kila wakia moja, ambalo ni ongezeko la asilimia 8.1 ikilinganishwa na bei ya kipindi kama hicho mwaka 2018.

Mwishoni mwa mwaka jana wakia moja iliuzwa kwa dola 1,523 na Ijumaa iliyopita bei yake ilikuwa imepanda hadi dola 1,558.8.