Wiki iliyopita makala hii iliishia pale ambapo Barnaba Classic anasimulia jinsi alivyokutana na Ruge Mutahaba Tanzania House of Talents (THT) alipokwenda kufanyiwa majaribio ya kufuzu kuingia katika jumba la kukuza vipaji.

Barnaba ni mmoja wa wasanii wachache wanaopenda kuongea huku wakicheka hasa pale wanapokumbuka walipotoka na mikasa iliyowahi kuwakumba katika harakati za kimuziki, ni mwanamuziki asiye na mbwembwe, mwenye sauti ya kubembeleza hasa pale anapoimba nyimbo za mahaba.

Anasema kwamba THT ni familia yake isiyo na mwisho kwani ilianzisha upya safari yake ya mafanikio ikiwa ni pamoja na kuongeza familia nyingine ya kimuziki kwa kushirikiana na wanamuziki chipukizi waliozalishwa katika nyumba hiyo.

“Haikuwa rahisi kuweza kusimama mimi bila Ruge, alikuwa sawa na mzazi wangu, kwani alikuwa ni kiongozi wangu, kaka yangu na familia yangu hapa mjini. Mimi ni mwanamuziki niliyetoka mtaani na kuanza kuishi na Ruge nyumbani kwake nikilala ukumbini.

Ulifika wakati mimi na Ruge tulikuwa tunakuwa wote tangu asubuhi mpaka usiku, maana hata soda tulikuwa tunakunywa chupa moja kwa kupokezana,” amesema.

Barnaba Classic amesema aliweza kukutana na walimu wa muziki waliokuwa wakitoa mafunzo THT na kuingia darasani katika mtindo ambao haukuwa rasmi, aliweza kuonyesha kipaji chake kiasi cha Ruge kutojutia chaguo lake.

“Nilipata malezi tofauti na niliyoyatarajia kutoka kwa walimu wa THT, walining’arisha mpaka kufikia hapa nilipo, kwani bila wao nisingekuwa Barnaba huyu mnayemuona na kupendezwa naye.

“Mimi ninatunga na kuimba ila nikiwa studio nimekuwa nikifanya muziki wangu mwenyewe kisha nitakuja kuwasikilizisha wengine baada ya kuuimba.

“Nilikuwa na kawaida ya kutotoa muziki bila kuidhinishwa Ruge. Ruge ndiye alikuwa mtu wa kwanza kusikiliza wimbo wangu kabla sijauachia, akiupitisha kwamba sasa unafaa ndipo ninauachia.

Kuna wakati nilikuwa naandaa wimbo nikimpatia ananiambia kabisa wimbo huo ni mbaya, hivyo ninaufanyia marekebisho mpaka atakaporidhika nao ndipo ninauachia.

Kulala kwa Ruge kumeniumiza, kwani alikuwa na mchango mkubwa kwenye maisha na muziki wangu. Naamini kuwa  Ruge hajafa bali amelala, amelala huku falsafa zake zikiendendea kuishi miongoni mwetu. Ninayaishi yale yote aliyonifundisha na kunielekeza.

“Safari yangu ya muziki ndiyo kwanza ninaianza huku nikiwa na dhamira ya kufika kule tulikotarajia kufika na Ruge, ndoto na maono ya Ruge nitayatekeleza kwa vitendo kupitia muziki wangu na THT ambayo tumeihamishia nyumbani kwa Ruge kama alivyotuelekeza kabla ya kulala.

“Ruge kabla hajalala alisema kuwa iwapo hatakuwepo THT ihamishiwe nyumbani kwake Masaki, nasi tunatekeleza hilo, tumeshaanza kutekeleza agizo hilo pamoja na kuongeza vyumba ili kuweza kuyaenzi maono yake,” amesema Barnaba Classic.