Wiki iliyopita makala hii iliishia pale ambapo Barnaba Classic anakumbuka kwamba baba yake hakuwahi kumkubali katika kazi yake ya muziki hadi siku alipopata mwaliko wa kwenda Ikulu na kwenda na baba yake, hapo mambo yakaanza kubadilika ndani ya familia. Endelea kufuatilia.
“Ninakumbuka niliponunua gari la kwanza, nikalipeleka nyumbani (Moshi) ili lipate baraka za wazee, baba alikataa kabisa hata kuligusa huku akinibeza kwamba nimeanza kuwa na tabia kama za matapeli wa mjini.
“Baba aliniambia kwamba nimekodi hilo gari ili kwenda kuwakoga nyumbani, wakati ukweli ni kwamba nilikuwa nimenunua gari hilo kwa fedha zangu zilizotokana na muziki. Niliondoka nyumbani nikiwa mnyonge kabisa.
Asimulia alivyokutana na Ruge
Barnaba Classic ameliambia Gazeti la JAMHURI kwamba hakuwa akifahamiana na Ruge Mutahaba awali, isipokuwa alipokwenda Tanzania House of Talents (THT) kufanyiwa majaribio ya kufuzu kuingia katika jumba la kukuza vipaji.
Barnaba anakumbuka wakati huo makao makuu ya THT yalikuwa Mtaa wa Morocco, jijini Dar es Salaam. Baada ya kukabidhiwa kipaza sauti ili aimbe na majaji wafanye uamuzi, hakuweza kuwashawishi hata kidogo.
Wakati anaondoka jukwaani huku akiwa amepoteza matumani ya kujiunga na THT, lakini kuna vitu vitatu vilikuwa vinabamiza kichwa chake, kwani tayari alikacha shule, kitu cha kwanza alichokuwa anafikiria ni kurudi mtaani akawe fundi wa kutengeneza redio; kitu cha pili arudi mtaani akaokote vyuma, maarufu kama siso, au arudi nyumbani akauze genge la mama yake.
Lakini kabla hajapata jibu la nini atakwenda kufanya mtaani, ndipo Ruge Mutahaba akamsimamisha na kumuuliza: “Wewe ndiye ulikuwa unaimba?” Barnaba akamjibu: “Ndiyo.” Ruge akampa nafasi nyingine ya kwenda kuimba kwa mara nyingine, lakini bado alionekana hana kipaji.
Barnaba Classic amesema pamoja na kuimba vibaya bado Ruge Mutahaba aligundua kipaji chake, akawaomba viongozi wa THT wamwache Barnaba aendelee kuingia darasani katika mtindo ambao haukuwa rasmi sana. “Ruge aliwaambia waniache nizugezuge pale, lakini nikaonyesha uwezo wangu na baadaye nikaanza kuingia darasani,” amesema.
Amesema malezi aliyoyapata akiwa THT kutoka kwa walimu waliompatia mafunzo kwa njia ya vitendo na nadharia yamemng’arisha na kumfanya kuwa Barnaba Classic mwenye mashabiki ndani na nje ya nchi kutokana na tungo zake zenye kugusa hisia za watu wengi.
“Kwangu THT ni baba kwenye muziki wangu, sambamba na hilo nikitaja THT linakuja jina la mzee wangu Ruge,” amesema Barnaba Classic.