Jina Barnaba Classic pengine si geni masikioni mwako! Huyu ni mwanamuziki na si msanii kama wanavyoitwa wengine, maana ameenea kila idara inayokidhi mwanamuziki kuitwa hivyo.

Unaweza kusema Barnaba Classic ni almasi iliyong’arishwa na Tanzania House of Talents (THT), maana yeye anasema alizaliwa na kipaji cha muziki lakini hakuwa anafahamu afanye nini, THT walisaidia kuhakikisha Barnaba Class anatoka kuwa Elias Barnaba a.k.a Dogo Pizzo.

Pengine unaweza kushangaa Dogo Pizzo ni nani? Naam! Huyo ndiye Barnaba Classic leo, jina ambalo kwa hakika halikuwa chaguo lake isipokuwa Ruge Mutahaba baada ya kusikiliza vionjo na muziki uliopangiliwa kutoka kwa kijana huyo kutoka Mkoa wa Kilimanjaro.

Kwa upekee huo pamoja na ala zilizopangika kwenye muziki, Gazeti la JAMHURI limezungumza na Barnaba Classic ambaye pamoja na mambo mengine amezungumza kuhusu alikotoka, alipo na mipango yake katika maisha ya muziki.

“Kwanza kabisa kwangu muziki si kazi ya ziada…niliacha kufanya mtihani wa kidato cha nne kwa sababu ya muziki, hivyo kwangu hii ni kazi. Bila muziki hakuna Barnaba…mimi ni Mchaga, sikufungua genge wala kuendeleza genge la mama isipokuwa nilichagua kufanya muziki.

“Ilitokea siku niliyotakiwa kufanya mtihani wa kidato cha nne, siku hiyo hiyo kukawa na usaili wa wanamuziki wanaotakiwa kusajiliwa na THT, sikufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne, tena sikufaulu usaili kuingia pale THT.

“Nakumbuka wakati ninaondoka pale kwenye audition, Ruge aliniona na kuniita, akanihoji kuhusu usaili wangu…nikamwambia kwamba sikufanikiwa, kwa kweli sikuimba vizuri. Akaniambia niimbe tena, akanisikiliza na kuwaambia wale majaji kwamba anaona kama nina kitu, akawaomba waniache ili niwe ‘ninazuga’ pale THT.

“Baada ya kupewa hiyo nafasi na baba (Ruge Mutahaba), mengine leo ni historia. Leo mimi ni mwanamuziki niliyeiva, kipaji changu kinaendelea kuthibitika,” amesema Barnaba.

Wazazi walifahamu?

Barnaba amesema hakuwashirikisha wazazi wake pale alipoacha kufanya mtihani wa kidato cha nne na kuamua kwenda kufanya usaili wa kujiunga na Tanzania House of Talents.

“Nilifanya siri kubwa sana, lakini baadaye wazazi walijua na bila shaka unafahamu hali anayokuwa nayo mzazi baada ya kuona mtoto wake amekatisha ndoto, tangu hapo sikuwa na furaha maana taswira ya muziki machoni pa wazazi wangu, hasa baba lilikuwa ni jambo la kihuni tu.

“Mama yangu (sasa marehemu) alikuwa ni shabiki mkubwa wa muziki wangu, ninakumbuka hata ule wimbo wangu wa kwanza niliomshirikisha Pipi, kwa kweli akiwa pale kwenye genge lake na akasikia unapigwa unamwona namna alivyokuwa akiburudika nafsini mwake.

“Baba yangu hakuwahi kunikubali kimuziki hadi pale tulipoalikwa Ikulu na kutakiwa kwenda na watu wetu wa karibu. Nakumbuka ilikuwa wakati wa Rais Jakaya Kikwete, nilikwenda na baba yangu na akamwona rais kwa sababu ya muziki wangu.

Itaendelea wiki ijayo…