MAGUFULIBila ya shaka, Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, atakuwa anasuka Baraza lake la Mawaziri.

Anamteua Waziri Mkuu na kulifikisha jina lake bungeni kwa uthibitisho, kama inavyohitaji Katiba, ili amsaidie katika kazi hiyo.

Katika Awamu zote, suala la kupunguza matumizi ya uendeshaji wa Serikali, hasa kupunguza ukubwa wa Serikali, limekuwa juu katika ajenda, lakini utekelezaji wake umekuwa kitendawili kisichoteguka.

Mmoja wa viongozi angalau aliyediriki kuweka dhamira hiyo ni Waziri Mkuu, hayati Edward Moringe Sokoine, lakini alifariki dunia katika ajali ya gari Aprili 12, 1984 na hakuwahi kutekeleza dhamira yake hiyo. Kwa maono ya Sokoine, Baraza dogo, wakati huo akizungumzia mawaziri 13, litapunguza gharama za uendeshaji wa Serikali na litakuwa na ufanisi wa hali ya juu.

 Baraza la Mawaziri la Serikali ya Awamu ya Nne, wakati mmoja hivi karibuni, lilikuwa na mawaziri 31 na naibu mawaziri 25.

Kwa Awamu ya Tano, Rais Magufuli, anaweza akalipunguza Baraza hilo likawa na mawaziri 12 tu, tena bila ya naibu. Mawaziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Waziri Mkuu, kama walivyo Naibu Mawaziri, hawana kazi ya maana kwa hiyo hawana sababu ya kuwapo.

Ile dhana kuwa kila mkoa uwe unawakilishwa katika Baraza, au apatikane Waziri au Naibu kutoka kila kabila, kati ya makabila takriban 120 nchini, haifai. Mbona Rais tunampata kutoka kabila moja tu?

Baraza la Mawaziri la Serikali ya Awamu ya Tano lisilokuwa na Mawaziri wa Nchi wala Naibu Mawaziri.

   Mpangilio wa uongozi wa Serikali na Baraza la Mawaziri, kwa maoni yangu, unaweza kuwa kama ifuatavyo:

 

Rais:

Makamu wa Rais (atashughulikia pia Muungano, yeye mwenyewe);

Waziri Mkuu (atashughulikia yeye mwenyewe Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa – TAMISEMI na atakuwa na Idara kadhaa zitakazoongozwa na Makamishna kusimamia masuala mbalimbali, chini yake, kama vile Uratibu, Sheria na Katiba, Utawala Bora, Jinsia – Wazee, Kinamama na Watoto);

 

Waziri wa Ulinzi, Usalama, Mambo ya Ndani: (atashughulikia pia JKT, Uhamiaji, Maafa);

Waziri wa Fedha Uchumi na Mipango: (atashughulikia pia Uwekezaji na Uwezeshaji);

Waziri Kilimo na Chakula: (pia Mifugo, Uvuvi);

Waziri wa Elimu, Sayansi, Utamaduni: (kama lilivyo Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) – atashughulikia pia  Utafiti, R&D (Research & Development);

Waziri wa Nishati, Madini na Maji;

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi;

Waziri wa Ardhi, Maliasili na Misitu (na Mazingira);

Waziri wa Viwanda, Biashara na Utalii (pia Ushirika, ambao ni Umoja wa Biashara na Huduma. Utalii ni Biashara tu);

Waziri wa Utumishi, Kazi na Vijana (pamoja na Masuala ya Ajira);

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii;

Waziri wa Mambo ya Nje: (ushirikiano wa Afrika Mashariki utakuwa humo pia);

Waziri wa Habari na Mawasiliano.

 

Katika mpangilio huu, Wizara nyingi zimeondolewa na baadhi ya shughuli, badala kuwa na Wizara kamili au Waziri wa Nchi, zinaweza zikafanywa na Idara tu ya Serikali, chini ya Kamishna au Mkurugenzi. Mwanasheria Mkuu atashughulikia masuala ya Katiba na Sheria, naye ni kama Waziri tu. Bunge ni kama idara inayojitegemea na hivyo, masuala yake kiserikali yanaweza kushughulikiwa na Waziri Mkuu mwenyewe, ambaye pia ni Mkuu wa Shughuli za Serikali katika Bunge, akisaidiwa na Mwanasheria Mkuu.

Naibu Mawaziri nao, huwa hata hawahudhurii vikao vya Baraza la Mawaziri. Ikibdi wahuhudhurie, kama Waziri hayupo, basi lazima apate kibali maalum. Kwanza hakuna Waziri anayemuamini Naibu wake na kumpa majukumu ya maana. Wizara ikiboronga, anawajibishwa Waziri, siyo Naibu. Kwa kukosa shughuli, wamebakia kujibu maswali ya Bunge tu, tena yale myepesi myepesi, mazito anajibu Waziri mwenyewe. Acha Mawaziri wafanye kazi hiyo wenyewe.

Habari ni Habari tu iwe kwa Elektroniki au Gazeti, hivyo isimamiwe na Wizara moja, siyo mbili kama ilivyo sasa

   Shughuli za Mawasiliano, kama vile Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasliano (TCRA), ziwe chini ya Wizara ya Habari. Kwa hiyo tozo za kampuni za simu na vyombo vya utangazaji, zitasaidia kuendesha masuala ya habari, ambayo siku zote yanakosa fedha, kuimarisha TV ya Taifa, Radio ya Taifa n.k. na kuendeleza taaluma ya Habari na Mawasiliano.

Hata jengo la TBC, lililoanza miaka ya 1990, sasa litamalizika. Katika Baraza lililopita, shughuli za vyombo vya habari vya elektroniki, zilikuwa zikisimamiwa na Wizara inayohusika na Sayansi na Teknolojia!

Lakini teknolojia au Teknohama, ni njia tu ya kufanikisha, kuharakisha na kuleta ufanisi katika masuala ya Habari. Habari ni habari tu, kama ikitolewa na TV, Radio, Mtandao wa Kijamii au Magazeti. Sasa ni mkanganyiko tu, masuala ya Habari yanasimamiwa na Wizara mbili tofauti – ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo na ya Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano.

Nafasi ya Waziri wa Nchi, kwa kweli haina maana na inaleta vurugu katika namna ya kuwajibika. Kwa utaratibu tuliouzoea, kwa mfano, Waziri Mkuu ndiye mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Lakini Tamisemi hii, ina Waziri wake, Waziri wa Nchi. Je, mambo yakiharibika, nani sasa ashikwe shati au blauzi? Waziri Mkuu au Waziri wa TAMISEMI?

Hata katika Ofisi ya Rais, kuna mambo kibao. Kwa utaratibu wa Awamu ya Nne, kwa mfano: Ofisi ya Rais ina Mawaziri wa Nchi, Ofisi ya Rais: (1) Menejimenti ya Utumishi wa Umma; (2) Utawala Bora; (3) Uhusiano; (4) Kazi Maalum. Wote hawa? Hii ni kupeana ulaji tu. Kwa Makamu wa Rais nako, kuna Mawaziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais: (1) Muungano (2) Mazingira! Na kwa Waziri Mkuu, kama ilivyo, Mawaziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu: (1) Tamisemi; (2) Sera, Uratibu na Bunge na (3) Uwezeshaji na Uwekezaji! Au ndiyo utamaduni wa kila kabila liwe na angalau Waziri, Naibu Waziri au Mkuu wa Mkoa au Wilaya?

Tusijielekeze katika kugawana vyeo, tujielekeze katika ufanisi wa hali ya juu wa Serikali, ambayo kila kabila, hata kama halina kabila lake ndani ya Baraza la Mawaziri, basi liione kuwa Serikali hiyo inalihusu vilivyo. Inaonekana tumezama zaidi katika kupeana ulaji wa bure.

Ndiyo maana, wataalamu wengi, maprofesa, wahandisi waliobobea; madaktari, wanakimbilia kwenye siasa na kuacha kutoa mchango wa kitaaluma kwenye taaluma zao.

Wakuu wa mikoa wasimamie pia wilaya zao, hawana haja ya wasaidizi kama Wakuu wa Wilaya.

Hata Wakuu wa Mikoa nao sasa wamulikwe. Watu hao wawe magavana wa kweli wenye uwezo wa kutenda na siyo makada wa vyama vya siasa, na kwa mfumo wa sasa, makada wa chama tawala. Hawa. Kwa kweli, wanamwakilisha Rais, kiutendaji, katika mikoa. Wawe wasimamizi wa shughuli zote za utawala katika mkoa na waangalizi wa shughuli za maendeleo, zilizokasimiwa kwa Halmashauri. Wasiingize mikono yao kwenye Halmashauri, lakini watupie jicho kali katika Halmashauri hizo, wakiwa Mhimili wa Halmashauri.

Wawajibike moja kwa moja kwa Waziri Mkuu na kila mwezi watoe taarifa kwa Waziri Mkuu, itakayofikishwa kwa Rais, kuhusu mambo yanavyokwenda kwenye mikoa yao.

Hivi sasa Wakuu wa Mikoa wanaonekana kama vile wapo wapo tu, na shughuli zao ni kuhudhuria sherehe na tafrija au kuwapokea mikoani viongozi wa ngazi ya juu wa Serikali, kama vile Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu au mawaziri.

Kwa mfano, Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa ana kazi gani zaidi ya kumsindikiza Rais, Makamu au Waziri Mkuu au kuwapokea uwanja wa ndege wakati wakirudi safari zao! Pakitokea mkutano wa hadhara, yeye ndiye mkaribishaji.

Je, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, anafanya nini kuzibana Halmashauri kuhusu uchafu wa jiji, usafi wa mazingira, kukitokomeza kipindupindu, kuwahamisha watu wa mabondeni n.k.?

   Ili Wakuu wa Mikoa, wafanye kazi zao kwa ufanisi, wasiwepo Wakuu wa Wilaya. Hawa Wakuu wa Wilaya, hawana kazi, wala hawakutajwa kwenye Katiba. Tumekuwa nao kwa mazoea tu  kuwa wasaidizi wa Wakuu wa Mikoa. Ndiyo maana wanapoteuliwa, hawaapishwi na Rais, bali wanaapishwa na Wakuu wa Mikoa!

Wakuu wa Wilaya wanawasaidia kazi gani Wakuu wa Mikoa, ambao kwa kweli Wakuu wa Mikoa wenyewe wapo wapo tu? Kama ni suala la Ulinzi wa Amani katika Wilaya, kazi hiyo ifanywe na Kamanda wa Polisi wa Wilaya, mwenye taaluma hiyo ya usalama. Wakuu wa Mikoa, wasimamie wilaya zao.

Kuwaondoa Wakuu wa Wilaya zaidi ya 130, kutapunguza sana gharama za kuendesha Serikali. Kumbuka, kila Mkuu wa Wilaya, ana gari la kifahari, “shangingi”, mshahara mnono, nyumba ya kuishi na ofisi kubwa. Mabilioni yatanusurika na shughuli za Serikali zitakwenda kama kawaida. Haya ndiyo maoni yangu.

 

Kwa ushauri unaweza kuufikisha kwa mwandishi wa makala hii kupitia simu 0759 488 955