📌 Dkt. Kazungu asema Wizara itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya Kimkakati.
📌 Baraza lapitisha rasimu ya bajeti ya 2025/2026 .
📌 Hoja za TUGHE zajadiliwa kwa kina na kupatiwa ufumbuzi
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. Khatibu Kazungu leo Machi 22, 2025 amefungua Baraza la saba la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati ambalo limepitia pamoja na mambo mengine Rasimu ya bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2025/2026 na kupitia hoja mbalimbali zilizowasilishwa na TUGHE.
Akifungua baraza hilo Dkt. Kazungu amesema Wizara ya Nishati itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya nishati nchini ili kuhakikisha nchi inakua na uhakika wa upatikanaji wa nishati ya umeme, mafuta na gesi.

“Wizara ya nishati itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya nishati nchini ili kuhakikisha Nchi inakuwa na uhakika wa nishati na katika kutekeleza hili wizara itahakikisha inasimamia taasisi zilizochini yake pamoja na makampuni tanzu yanayojishughulisha na nishati nchini”. Amesema Dkt. Kazungu.
Kazungu ameelza kuwa Wizara itaendelea kutekeleza miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme ikiwa ni pamoja na kufikisha Gridi ya taifa katika Mikoa iliyosalia ya Rukwa, Kagera, Lindi na Mtwara.
Aidha, Wizara itaendelea kutekeleza mpango wa taifa wa nishati wa mwaka 2025/2026 kwa lengo la kuongeza upatikanaji na uunganishaji wa umeme kwa wananchi, kuongeza mchango wa nishati jadidifu katika uzalishaji wa umeme na mashirika binafsi katika maendeleo ya sekta ya nishati na kuhakikisha upatikanaji wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Kutekeleza miradi wa Gridi ya taifa, kufanya matengenezo na ukarabati wa mitambo ya kuzalisha umeme pamoja na uboreshaji njia za kusafirishaji na usambazaji wa umeme katika vitongoji, maeneo ya migodi, viwanda pamoja na vituo vya afya.
Kwa upande wa Sekta ya mafuta na gesi, Dkt. Kazungu amesema sekta ya mafuta na gesi Wizara itaendelea kuwezesha upatikanaji wa bidhaa ya mafuta ,kupitia ujenzi wa vituo vya mafuta maeneo mbalimbali nchini.
Kazungu amesisitiza Wizara itaendelea kujikita katika kuwezesha utafutaji,uendelezaji na usambazaji wa gesi asilia na kutekeleza miradi ya kimkakati ya gesi asilia ikiwemo Mnazi bay Kasikazini,mradi wa kuchakata gesi asilia kuwa kimiminika (Lindi) ,utafutaji na uendelezaji na usambazaji wa mafuta ikiwemo ujenzi wa Bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Ohima (Uganda) hadi Chonholeani (Tanga-Tanzania).

Kwa upande wa nishati safi ya kupikia kwa mwaka wa 2025/2026 Wizara itaendelea kutekeleza mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na mpango wa Taifa wa nishati wa mwaka 2030.
Aidha, Wizara itaendelea kuhamasisha sekta binafsi katika kuimarisha upatikanaji wa malighafi na miundombinu ya nishati safi ya kupikia.
Mwenyekiti wa Balaza la Wafanya kazi Wizara ya nishati Ndugu Zuena Msuya aliweza kueleza umuhimu wa kudumisha stahiki za watumishi ili kuendeleza ufanisi wa ufanyaji kazi katika Wizara ya Nishati.




