Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
BARAZA la Mitihani la Tanzania limefuta matokeo yote kwa jumla ya wanafunzi 105 wa darasa la nne na 46 wa kidato cha pili kwa kufanya udanganyifu na kuandika matusi.
Aidha Baraza hilo limefungia kituo cha Upimaji na Mitihani ya Taifa GoodWill kilichopo mkoani Arusha kutokana na Mkuu wa Shule na baadhi ya walimu kuthibitika kufanya udanganyifu kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi.
Akizungumza na waandishi wa habari, leo Januari 4, 2025 Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania, Dkt. Said Mohamed amesema matokeo hayo yamefutwa kwa mujibu wa kifungu cha 5(2)(j) cha Sheria ya Baraza la Mitihani sura ya 107 kikisomwa pamoja kifungu cha 30(2) (b) cha Kanuni za Mitihani za Mwaka 2016.
Amesema katika wanafunzi hao 100 wa darasa la nne walifanya udanganyifu na watano waliandika matusi huku kwa kidato cha pili waliofanya udanganyifu ni 41 na watano waliandika matusi katika karatasi zao za majibu katika Upimaji wa kitaifa wa kidato cha pili.
“Kati ya hao wanafunzi 100 waliofutiwa matokeo, 98 ni watoto wa muda mrefu hivyo walimu wakuu waliwapanga wanafunzi wenzao wa darasa la tatu, tano na sita kuwafanyia Mitihani kwa maslahi yao binafsi,” amesema.
Akizungumzia kuhusu Kituo cha GoodWill kufungiwa amesema kilijaribu kuwarubuni wasimamizi na askari Oktoba 28 na 29, 2024 bila mafanikio.
“Walipoona hivyo wakaamua kutumia mbinu mbadala wakati Mtihani ukiendelea kwa kuwapanga wanafunzi kupata majibu kupitia chooni. Pamoja na kufungiwa, Baraza litawasilisha mapendekezo kwa Kamishna wa Elimu ili kufutiwa usajili wa moja kwa moja kwani kinakosa sifa ya kuendelea kuwa Shule,” amesema.
Kuhusu waliofaulu darasa la nne, Dkt. Mohamed amesema kuwa jumla ya wanafunzi 1,320,227 kati ya 1,530,805 wenye matokeo sawa na asilimia 86.24 wamefaulu kuendelea na darasa la tano mwaka 2025 kwa kupata daraja A, B, C na D.
“Mwaka 2023 wanafunzi waliofaulu walikuwa 1,287,934 sawa na asilimia 83.34, hivyo kumekuwa na ongezeko la ufaulu kwa asilimia 2.90 kwa wanafunzi waliopata fursa ya kuendelea na Darasa la Tano ikilinganishwa na mwaka 2023,” amesema.
Akizungumzia waliofaulu kidato cha pili, amesema jumla ya wanafunzi wa Shule 680,574 kati ya 796,825 wenye matokeo ambao sawa na asilimia 85.41 wamefaulu kuendelea na kidato cha Tatu ambapo wamepata Madaraja ya I, II, III na IV.
“Mwaka 2023 wanafunzi waliofaulu walikuwa 592,741 sawa na asilimia 85.31. Ufaulu umeongezeka kwa asilimia 0.10. Kati ya wanafunzi 680,574 waliofaulu kuendelea na kidato cha Tatu. Wasichana ni 367,457 sawa na asilimia 83.99 na wavulana ni 313,117 sawa na asilimia 87.13. Hivyo, wavulana wamekuwa na ufaulu bora kuliko wasichana,” amesema.