MAGUFULIRais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, amekwepa kihunzi cha wasaka nafasi ya uwaziri waliokuwa  wakihaha kuomba nafasi hizo.

Habari za uhakika zilizoifikia JAMHURI zinaeleza kuwa kumekuwa na msururu wa wanasiasa nchini ambao wamekuwa wakihaha kukutana naye ili kumshawishi awateua katika nafasi za ubunge na wengine katika Baraza la Mawaziri.

Habari hizo zinaeleza kuwa juhudi hizo zimekuwa zikifanywa na baadhi ya wanasiasa wakongwe, ambao wengine hawakufanikiwa kupata ubunge katika Uchaguzi Mkuu uliomalizika hivi karibuni.

Imeelezwa kuwa tangu Dk. Magufuli atangazwe kuwa Rais, kumekuwa na idadi kubwa ya baadhi ya wanasiasa na wapambe wao wanaotaka kumuona, lakini amekuwa mgumu kukutana nao.

Rais Dk. Magufuli alibainisha tangu awali kuwa anataka kufanya kazi na watu wapya na suala la uteuzi wa Spika aliliacha kwa chama hasa Mwenyekiti, Dk. Jakaya Kikwete, Makamu Mwenyekiti (Bara), Philip Mangula, pamoja na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana.

“Dk. Magufuli kajifungia, hataki mchezo, watu wanahaha kumuona ili awateue wakati wengine wamekaa kwenye nafasi hizo na hakuna walichofanya, na sasa hawapi hata fursa ya kukutana nao,” anasema mtoa taarifa.

Anasema kuwa baadhi ya wanasiasa wamejikuta wakishindwa kukutana na Dk. Magufuli kutokana na kutokuwa tayari kukutana nao ili kutimiza wajibu wake bila msukumo wao, jambo ambalo limekuwa likisifiwa na wasaidizi wake.

“Tulizoea kuona watu wakikutana na Rais kirahisi-rahisi huku wengine wakija kumuomba nafasi za uteuzi, hapa wamegonga mwamba, hataki kukutana nao maana anawajua,” anasema.

Inaelezwa kuwa Rais amekuwa mgumu kukutana na watu katika kipindi hiki anachotaraji kufanya uteuzi wa Baraza la Mawaziri wiki hii.

Ili kuthibitisha hilo, Dk. Magufuli mwenyewe alibainisha Ijumaa iliyopita kuwa anatarajia kuwa na Baraza dogo la Mawaziri litakalofanya kazi kwa zaidi ya saa 18 kwa siku ili kwenda sambamba na kasi anayotaka kuwaletea maendeleo Watanzania. 

Mtoa habari anakwenda mbali akisema mbali na Spika wa Bunge la 10, Anne Makinda, kutangaza kwamba ameamua kupumzika baada ya kufanya kazi bungeni kwa miaka 40, lakini taarifa zinasema kuwa sababu nyingine ni kikwazo cha kutoonana na Magufuli.

Taarifa kutoka kwa watu wa karibu zinasema kwamba Makinda alijiandaa kutetea nafasi yake ila alishindwa kuingia rasmi katika kinyang’anyiro cha Uspika wa Bunge la 11 baada ya juhudi zake kukwama.

Imeelezwa kuwa kabla ya Makinda kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo, alitaka kukutana na Rais Dk. Magufuli lakini alijikuta akikosa fursa hiyo, jambo lililomlazimu kuachana na Uspika.

“Madam Speaker (Mheshimiwa Spika) alitaka kukutana kwanza na Rais ili aweze kuwa na uhakika na kile anachokwenda kukifanya, ni vigumu kupata nafasi hiyo kama Rais hajatoa baraka,” anasema.

Anaeleza kuwa Makinda alifanya juhudi za kuweza kukutana na Rais lakini hakuweza kufanikiwa, hivyo kuamua kutogombea nafasi hiyo kukwepa kujisikia vibaya ingetokea jina lake kukatwa.

Kutokana na msimamo huo hakuwa tayari kuchukua fomu kisha jina lake likatwe, jambo ambalo lingemletea aibu  kama ilivyopata kuwatokea watangulizi wake – Samwel Sitta wa Bunge la Tisa na Pius Msekwa wa Bunge la Saba na Nane.

Hata hivyo, anasema kuwa wakati wa mchakato huo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kulikuwa na tetesi kuwa Dk. Magufuli anataka sura mpya katika uongozi wake, hivyo wanasiasa waliokuwa serikalini kwa muda mrefu hawezi kuwapa nafasi ili kutoa fursa kwa watu wapya.

 

Baraza la Mawaziri

Kumekuwa na taarifa za Dk. Magufuli kutokutoa fursa kwa wanasiasa wakongwe kuingia kwenye Baraza lake la Mawaziri kutokana na kuwapo serikalini kwa muda mrefu.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa Baraza la Mawaziri litakuwa na sura mpya ambazo zinatarajiwa kuwa na tija itakayoendana na kasi ya utendaji wake.

“Kuna watu wamekuwa kwenye nyadhifa kubwa tangu Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere, wamekuwapo katika awamu zote za uongozi, hawa hawatapewa nafasi katika Awamu hii ya Tano,” anasema mtoa habari.

Baadhi ya wanasiasa waliotajwa hawakuweza kupatikana ili kutoa ufafanuzi kuhusiana na taarifa zao hadi gazeti hili linakwenda mtamboni, ingawa gazeti hili lina uhakika juu ya makada hao wa chama.