Na Victor Masangu, JamhuriMedia, Kibaha

Baraza la Madiwani katika  Halmashauri ya mji Kibaha limemuomba Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuwapatia baadhi ya eneo la ardhi ambayo inamilikiwa na shirika la elimu Kibaha ili waweze kuiendeleza katika shughuli mbali mbali za kiuchumi na kimaendeleo.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji Kibaha Mussa Ndomba  wakati wa  kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya nne ya mwaka wa fedha kwa kipindi cha mwaka 2023/2024.

Ndomba akizungumza kwa niaba ya madiwani wenzake amesema kwamba kwa kipindi kirefu eneo kubwa la ardhi limekuwa likimilikiwa  na shirika la Elimu Kibaha limeshindwa kuendelezwa na kusababisha kuwa sehemu kubwa ya vichaka na  pori hali ambayo inahatarisha usalama.

Alibainisha kwamba lengo lao kubwa la Halmashauri ya Kibaha mji ni kuwa Manispaa hivyo wakipata  eneo hilo la ardhi  wataweza kuliendeleza katika shughuli mbali mbali za kimaendeleo kuliko lilivyo kwa sasa halitumiki katika shughuli yoyote ile.

“Kwa kweli sisi kama Baraza la Madiwani ombi letu kubwa kwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ni kupata baadhi ya  eneo la ardhi ambalo linamilikiwa na Shirika la elimu Kibaha na nia yetu ni nzuri ya kuweka mipango ya kuendesha shughuli mbali mbali za maendeleo,”alisema Ndomba.

Aidha Ndomba alitumia kikao hicho kukumbushia ahadi ya Waziri wa Maji Juma Aweso ya kupeleka mradi wa maji kwa baadhi ya kata ikiwemo kata ya Pangani na viziwaziwa.

 Alibainisha kwamba kuna baadhi ya kata bado zinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama hivyo ana imani ahadi ya Waziri ikitekelezwa kutaweza kusaidia wananchi kupata huduma ya maji safi na salama.

Katika hatua nyingine Ndomba alimpongeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kutenga fedha kwa ajili ya kuweza kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule mpya.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Tangini Mfaume Kabuga hakusita kuunga mkono hoja ya kupewa baadhi ya  eneo la Shirika la elimu Kibaha kutokana na kugeuka kuwa mashamba pori na sehemu ya kujificha waharifu.

Pia baraza hilo limeiomba serikali kuweka mipango madhubuti ya kufanya upanuzi katika barabara kuu ya morogoro  road kwa lengo kwa lengo la kuweza kupunguza foleni na ajali.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya mji Kibaha Dkt.Rogers Shemweleka amesema lengo lake kubwa ni kuhakikisha analinda na kuzitunza rasilimali zote kwa maslahi.

Kadhalika Mkurugenzi huyo aliwaomba madiwani na wataalamu kuwa na ubunifu na kuwa na vyanzo vipya vya mapato ambavyo ni vikubwa kuliko kutegemea vyanzo vile vile.

“Lengo langu ni kuwahudumia wananchi wote na mimi kiukweli tangu nianze kazi hii nimejitahidi kwa hali mali kushirikiana na timu yangu ya wataalamu na tumefanikiwa kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mapato,”alisema Dkt Rogers.

Pia katika baraza hilo pia kulienda sambamba na  kufanyika uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji.

Katika uchaguzi huo Diwani wa kata ya picha ya ndege Karim  Mtambo ameweza kuibuka kidedea baada ya kuibuka na ushindi kwa kuweza kupata kura 18 za ndio.

Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa kushika nafasi ya  Makamu Mwenyeki alisema aliwataka madiwani kuwa.na umoja na mshikamano ili kuwaletea wananchi maendeleo.

Nao baadhi ya madiwani akiwemo diwani wa viti maalumu  Aziza Mruma amehimiza suala la kuwa na uwazi katika utekezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo ili kuondokana na sintofahamu baina ya watendaji,wananchi na madiwani.

Kikao cha baraza la madiwani Halmashauri ya mji kibaha robo ya nne imeweza kujadili mambo mbali mbali ya kimaendeleo,kufanya uchaguzi wa kamati tofauti na kupanga mipango ya kimaendeleo.