Na Happy Lazaro, JamhuriMedia, Arusha

Baraza la madiwani Halmashauri y Wilaya ya Meru mkoani Arusha limeridhia na kupitisha bajeti ya zaidi ya shs 60 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa mwaka 2025/2026.

Akipitisha bajeti hiyo leo mkoani Arusha Mwenyekiti wa halmashauri hiyo ,Jeremiah Kishili amesema kuwa bajeti hiyo ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri hiyo.

Kishili amewapongeza wataalamu wa halmashauri hiyo kwa kuiangalia bajeti hiyo na kuipitia kwani imekaa vizuri na sasa ni utekelezaji tu wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Wananchi wanataka kuona mabadiliko hivyo ni wajibu wetu kuendelea kushirikiana ili mapato yaendelee kuongezeka zaidi na kuendelea kupata sifa nzuri kuhusu kuongezeka kwa kiwango cha mapato “amesema Kishili.

Aidha amewataka wataalamu hao kuendelea kushirikiana katika kutatua changamoto mbalimbali katika halmashauri hiyo na kuhakikisha hakuna malalamiko yoyote.

Kwa upande wake Meneja wa TARURA Arumeru,Injinia Julius Kaaya amesema kuwa Baraza la madiwani limepitisha bajeti ya shs 2,653,000 bilioni kwa mwaka 2025/2026 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya barabara katika halmashauri hiyo.

Kaaya amesema kuwa,fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya barabara katika halmashauri ambapo ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha pindi miradi hiyo inapofika katika maeneo yao.

Aidha baada ya kusomwa kwa bajeti hiyo madiwani wa halmashauri hiyo waliomba kuongezewa bajeti zaidi ili iweze kutosheleza mahitaji ya barabara zao .

Kwa upande wake Mratibu wa TASAF halmashauri ya Meru , Edwin Mathias amesema kuwa wameweza kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa nyumba za watumishi,vyumba vya madarasa pamoja na kufikia wananchi mbalimbali wenye mahitaji .

Aidha ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana nao zaidi katika kipindi hiki ambacho wanaendelea kutekeleza miradi mbalimbali kwani miradi hiyo imeletwa kwa lengo lao.

Naye Diwani wa kata ya Seela -Sing’isi ,Elisa Nassari amesema kuwa bajeti hiyo itasaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya elimu,afya,maji pamoja na ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya halmashauri hiyo kwani miundombinu mingi ni mibovu.

Aidha ametoa wito kwa madiwani wengine kuendelea kuhamasisha wananchi wao katika kushiriki kikamilifu katika miradi mbalimbali ya maendeleo na wasiwe wakwamishaji bali waendelee kuwaunga wadau mkono.