Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amezindua Baraza jipya la Madaktari Tanganyika linalotarajia kudumu kwa muda wa miaka mitatu, huku moja ya jukumu la Baraza hilo ni kumshauri Waziri wa Afya katika masuala ya udhibiti, utoaji huduma na mafunzo kwa wataalamu wa Udaktari, Udaktari wa Meno na Afya Shirikishi.

Waziri Ummy amezindua baraza hilo leo Juni 7, 2023 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma, tukio lililohudhuriwa na Wakurugenzi wa Wizara, Wasajili wa Mabaraza, Wasajili wa bodi na Watumishi mbalimbali wa Wizara ya Afya.

Katika tukio hilo, Waziri Ummy ameelekeza Baraza kusimamia viapo na maadili ya taaluma zao yanavyoelekeza, hususan kwenye suala la kuokoa maisha ya mgonjwa kwanza kabla ya kutanguliza maslahi binafsi ikiwemo ya fedha jambo ambalo ni kinyume na viapo na maadili ya taaluma ya Udaktari.

“Lazima msimamie viapo vyenu, hasa kwenye suala la kuokoa maisha ya mgonjwa kwanza kabla ya kutanguliza maslahi ya fedha mbele, jambo ambalo ni kinyume na viapo na maadili ya Udaktari.” Amesema Waziri Ummy

Ameendelea kusema, taaluma ya Udaktari lazima kuwe na ubora elekezi (standards) kwakuwa inahusu maisha ya watu na amepongeza Baraza hilo lililomaliza muda wake kwa kazi nzuri waliofanya katika hili.

Aidha, Waziri Ummy amesema Pamoja na kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na Baraza lililomaliza muda wake, bado kuna kazi kubwa ya kufanya katika kusimamia Madaktari, huku akitaka kujua katika miaka mitatu ya Baraza ni madaktari wa ngapi wamechukuliwa hatua za kusimamishiwa sajili zao au kupewa onyo katika kipindi hicho.

Sambamba na amelitaka Baraza jipya kukaa na TCU ili kuona mahitaji ya soko la ajira katika kada za Udaktari ili kuwasaidia wanafunzi wasome kulingana na mahitaji ya soko la nchi katika fani ya Udaktari hali itayosaidia kupunguza idadi ya Wataalamu wasio ajirika nchini.

Pamoja na hayo, Waziri Ummy ametoa wito kwa Baraza kuunga mkono jitihada za Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kupeleka Madaktari kusoma nje ya nchi kwa fani mbalimbali za kibingwa katika maeneo ambayo Serikali inauhitaji wa wataalamu hao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Madaktari Tanganyika Prof. David Ngasapa amesema Baraza lina mamlaka ya Kimahakama (Quasi – Judicial) inayolipa uwezo wa kuendesha uchunguzi na kumshitaki Mwanataaluma yeyote ambaye atatuhumiwa kwenda kinyume na maadili ya taaluma ambayo imewekwa na Sheria pamoja Kanuni za Maadili ya Kitaaluma.