Na Zulfa Mfinanga, Jamhuri Media, Arusha

Watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Arusha wametakiwa kuwa wazalendo katika matumizi sahihi ya mitambo mipya iliyonunuliwa kwa lengo la matengenezo ya barabara za ndani ya jiji ambazo hazina viwango vya TARURA.

Akizindua mitambo hiyo iliyogharimu kiasi cha zaidi shilingi bilioni 1.7, Meya wa Jiji la Arusha Maxmillian Iranqhe amewataka watendaji hao kuhakikisha lengo linatimizwa la kuwa na barabara za ndani zenye ubora ili wananchi wafanye majukumu yao ya kulijenga Taifa katika mazingira rafiki.

Hata hivyo amesisitiza suala la Madiwani na Watendaji wa mitaa kusimamia usafi wa mitaa unaofanyika kila siku ya jumamosi ili kufanya Jiji kuwa safi na kuvutia zaidi Wageni.

“Pesa iliyonunua mitambo hii imetokana na kodi za wananchi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, kupitia usimamizi wa Madiwani hivyo nategemea mitambo hii kutunzwa vyema, pia nitoe rai kwa yeyote kuwa mlinzi wa mitambo hii,” amesema na kuongeza:

“Kipekee nawapongeza Waheshimiwa Madiwani kwa kuwa mafanikio haya yote yametokana na mawazo yenu chanya na namna mnavyoibua hoja za kujenga Jiji letu, sambamba na hayo niwahamasishe kuimarisha usafi ili kuendana na hadhi ya Jiji la Utalii ambapo kwa mwaka huu tunategemea kupata wageni wapatao milioni tano hivyo kila mmoja kwa nafasi yake ahamasishe usafi kwenye eneo lake” Amefafanua Iranqhe.

Mkurugenzi wa Jiji la Arusha John Kayombo amepongeza hatua hiyo iliyofikiwa ambayo imefanikisha manunuzi ya malori mawili na mtambo 1 kwa gharama ya shilingi bilioni 1.7, hatua iliyofanikisha kufikia lengo lililowekwa na Baraza la Madiwani.

“Licha ya manunuzi ya mitambo hii na kulipa mapato serikali kuu, bado tumebaki na salio ambalo tutahakikisha Kata zote 25 za Jiji pamoja na Mitaa yake yote 154 inanufaika kwa kiasi cha shilingi milioni 4 kwa kila Kata, lengo ni kununulia vifusi ili barabara zote za mitaa ziweze kuwa imara” amefafanua Kayombo.

Diwani wa Kata ya Sokoni 1 Saruni Olodi, amepongeza jitihada za Baraza la Madiwani kwa kuokoa gharama za kukodisha mitambo, hadi kufikia hatua ya kumiliki mitambo yao wenyewe.

“Niwatoe wasiwasi wananchi wetu wawe na subira, mambo yatakaa sawa kwa kata zote ambazo zimekuwa na changamoto ya ubovu wa barabara kwa kipindi kirefu” amesema Olodi.

“Nimefurahishwa na hatua hiyo maana itatuondolea adha ya kuharibika kwa vyombo vyetu kila wakati kutokana na ubovu wa miundombinu katika kata zetu, ninaomba wakabidhiwe watu makini watakaotunza mitambo hiyo” amesema Samwel Bulima dereva wa bodaboda anayepaki stand ya Kilombero.