· TARURA yasema mkandarasi yupo kazini
· Mbunge asema bado mkandarasi hajapatikana
· Mkandarasi agoma kuzungumza
ARUSHA
NA ZULFA MFINANGA
Ubovu wa barabara inayounganisha Kata ya Shighatini na Ngujini wilayani Mwanga katika Mkoa wa Kilimanjaro umeendelea kuwa kero kwa wakazi wa maeneo hayo, hali inayosababisha kushindwa kuzifikia huduma za kijamii kwa haraka na kwa wakati muafaka kutokana na kukosekana kwa usafiri wa uhakika.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 25.9 ipo chini ya Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA), inategemewa na wakazi wa kata hizo kwa uzalishaji mali na njia ya kufika Hospitali ya Wilaya Usangi, Soko la Kikweni, Soko la Ugweno na kwa wakazi wa Kata ya Shingatini hutegemea barabara hiyo kufika katika Soko Kuu la Mwanga.
Licha ya unyeti wa barabara hiyo, bado imekuwa kero kubwa huku wananchi wa maeneo hayo wakidai kuwa tatizo hilo ni la kihistoria, kwani tangu Uhuru barabara hiyo haijawahi kutengenezwa.
Wananchi wanasema wamekuwa wakitumia muda mwingi kujitolea nguvu kazi kwa mikono kwa ajili ya kufanya matengenezo madogo madogo kila mara, jambo ambalo wanaona halipatiwi ufumbuzi wa kudumu.
Mkazi wa Kijiji cha Ibaya anasema: “Viongozi wetu wamekuwa wakituhamasisha kujitolea ili tuiboreshe angalau tuweze kupita, lakini tunaona tunapoteza muda, kwa sababu kila mwaka kazi ni hii hii. Kwa nini serikali isije na suluhisho la kudumu, hapa hata usafiri ni shida kubwa, usafiri wa uhakika ni pikipiki za kukodisha.”
Anaongeza: “Lakini nazo ni gharama kubwa, pia si rafiki kwa watu wote kama vile wagonjwa na wazee. Mfano, ukiwa na mgonjwa gharama ya teksi kutoka hapa hadi Mwanga mjini ni Sh 40,000, hii yote inatokana na ubovu wa barabara.”
JAMHURI limetembelea maeneo hayo na kushuhudia ubovu mkubwa wa barabara hiyo iliyopo maeneo ya mlimani, yenye mawe na utelezi. Aidha, barabara hiyo ni nyembamba isiyoruhusu magari mawili kupishana, pia haina mifereji ya kupitisha maji kipindi cha mvua.
Kwa mujibu wa wakazi wa maeneo hayo, awali kulikuwa na usafiri wa mara moja moja kwa wiki hasa siku za masoko, lakini kadiri siku zinavyozidi kwenda na barabara hiyo kuzidi kuharibika wenye magari wameacha kutoa huduma hiyo kabisa.
Mmoja wa wananchi kutoka Kijiji cha Vuchama Ndambwe anasema kutokana na ubovu wa barabara hiyo wamekuwa wakitumia gharama kubwa sana kusafirisha malighafi kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya serikali kama vile Shule ya Sekondari Kamwala pamoja na zahanati ya kijiji hicho.
“Hapa tunategemea Kituo cha Afya Shighatini au Hospitali ya Wilaya Usangi, wewe mwenyewe umeona, hivi ikitokea mgonjwa hapa anafikaje huko? Hata ukikodisha gari, kwanza gharama ni kubwa sana, kutoka hapa hadi Mwanga kwa teksi ni shilingi 40,000, huwezi kuamini kuwa huwa tunatembea kwa miguu kwenda Mwanga mjini au Usangi, kwa sababu kutumia usafiri ni gharama kubwa,” anasema.
Wakazi wa Kijiji cha Vuchama Ndambwe wanasema kijiji hicho hakijawahi kutembelewa na kiongozi yeyote kutoka ngazi ya juu serikalini ambaye angeweza kujionea hali halisi na kuwasaidia.
“Tungetembelewa na viongozi wa juu ingesaidia, kwa sababu hata hayo matengenezo unayoambiwa ni aibu ukiona, wanachukua udongo kutoka eneo la pembeni wanaweka barabarani, mvua ikinyesha kunakuwa na tope la hatari, na kibaya zaidi hilo katapila likipita hatuambiwi, hata viongozi hawaambiwi, tunaona limekuja tu ghafla,” anasema mmoja wa wananchi na kuongeza:
“Tunasikia wakisema bajeti ni ndogo, basi kama ni hivyo hayo maeneo wanayotengeneza yangekuwa imara ili ikipatikana bajeti nyingine iweze kuendeleza sehemu nyingine, isiwe sehemu hizo hizo zinarudiwa kila mara, ndiyo sababu mabadiliko hayaonekani.”
Taarifa kutoka chanzo cha ndani kwenye kikao cha Maendeleo cha Kata ya Shighatini (WDC) kinasema ubovu wa barabara hiyo imekuwa ajenda yao kila mara na majibu yake ni kwamba TARURA watakuja kulifanyia kazi licha ya kukiri kuona marekebisho madogo yakifanywa lakini hayana tija, kwani tatizo bado lipo palepale.
Chanzo hicho kimedokeza pia kuwa hivi karibuni Mbunge wa jimbo hilo, Prof. Jumanne Maghembe, alifanya kikao na viongozi wa chama akatoa ahadi ya kutafuta fedha nje ya TARURA kwa ajili ya kuboresha barabara hiyo lakini hadi sasa hawajui kinachoendelea.
Mbunge ‘apishana’ na TARURA
Akizungumza na JAMHURI kwa njia ya simu, Prof. Maghembe amekiri kuwepo kwa changamoto ya barabara hiyo na kuongeza kuwa kutokana na umuhimu wake imepewa kipaumbele kwenye matengenezo na kwamba matengenezo hayo yatafanyika mara baada ya mvua kukatika.
Wakati TARURA wakisema tayari mkandarasi ameshapatikana na yupo eneo la kazi licha ya kuwa kwa sasa amesimama kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, mbunge huyo amesema bado hawajapata mkandarasi kwa sababu ya mvua, na kwamba wanasubiri mvua zikipungua au kukatika ndipo watatafuta mkandarasi.
“Ni kweli hayo maeneo unayoyataja nimepita, najua changamoto zake, ukweli ni kwamba fedha zipo kutoka mfuko wa dharura ingawa kwa sasa siwezi kujua ni kiasi gani, kwa hiyo fedha hizo pamoja na zile za TARURA zitasaidia kutatua sehemu kubwa ya changamoto. Kuhusu mkandarasi bado hajatafutwa kwa sababu huwezi kumtafuta kipindi hiki cha mvua, kwani atatudai pesa za ucheleweshaji, kumtafuta sasa hivi ni kutaka kumlipa malipo ambayo hakuna kazi iliyofanywa,” anasema.
TARURA yamuita mwandishi ofisini
JAMHURI lilipowasiliana na Meneja wa TARURA Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Meleck Silaa, ili kupata maelezo juu ya barabara hiyo, alimuelekeza Meneje wa TARURA Wilaya ya Mwanga, Emmanuel Yohana, kutoa maelezo hayo kwa mwandishi.
Lakini alipotafutwa kwa simu, Meneja wa TARURA Wilaya ya Mwanga, alimtaka mwandishi kufika ofisini kwa maelezo kwamba ni muhimu kufika eneo la tukio (kwenye barabara husika) ili kujionea kwa macho kile kinachosemwa ili kulinganisha na hali halisi.
Baada ya mwandishi kufika Ofisi ya TARURA Mwanga na kukubaliana kufika katika barabara hiyo lakini bado suala hilo halikuwezekana, kwa madai kwamba kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha haitawezekana kufika, hivyo itafutwe siku nyingine ambayo hakutakuwa na mvua.
Katika maelezo yake, Yohana amesema barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 25.9 kutoka Kisangara hadi Shighatini ingawa ni kweli ina ubovu, lakini bado haiwezi kuitwa mbaya, bali ipo kwenye kundi la ubovu wa wastani kwa mujibu kwa vipimo vya kitaalamu.
Aliendelea kufafanua kuwa barabara hiyo imekuwa ikifanyiwa matengenezo kila mwaka na kwamba kutokana na ufinyu wa bajeti wamekuwa wakiangalia maeneo yenye changamoto kubwa, kwani wamekuwa wakipokea bajeti pungufu ya ile waliyoomba.
Amesema mkandarasi Kampuni ya Asjel Construction Limited kutoka jijini Mwanza ndiye aliyepewa kazi ya kutengeneza na wameingia makubaliano naye Disemba 4, mwaka jana na tayari ameshaanza kazi, licha ya kusimama kwa muda kutokana na mvua huku akitarajiwa kumaliza kazi hiyo ndani ya miezi minne.
“Changamoto kubwa hapa ni bajeti. Kwa mfano, wilaya nzima tuliomba Sh bilioni saba lakini tumepewa Sh milioni 800.43. Hiyo barabara tunayozungumzia yenyewe tuliiombea Sh milioni 800 lakini kutokana na bajeti tuliyopata mwaka huu tumeitengea Sh milioni 17 ambazo zitatengeneza kilometa nane tu, na hii barabara kitaalamu tunaiita ‘collector’, kwa maana kuwa ni barabara kuu inayounganisha wilaya na kata.
“Kutokana na ufinyu wa bajeti, tulikubaliana na madiwani kwamba tutengeneza sehemu korofi ili watu waweze kupita, na nilipita tukaandikishiana muhtasari ni maeneo gani yaanze kufanyiwa matengenezo na mengine yasubiri, na kwenye hiyo barabara unayoitaja kuna sehemu tutaweka kifusi, sehemu nyingine zitafanywa kwa mikono na wananchi na nyingine zitawekwa mawe,” anaeleza.
Anasema changamoto iliyopo kwa sasa ni mvua zinazoendelea kunyesha, jambo ambalo limesababisha mkandarasi kusimamisha kazi licha ya kuwa aliingia mkataba mwezi Disemba mwaka jana lakini alianza kazi Januari mwaka huu baada ya mvua kupungua, lakini kwa sasa amesimama kwa mara nyingine.
Anasema wilaya hiyo ina mtandao wa barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 579.64, ambapo kati ya hizo kilometa 212.98 sawa na asilimia 36.74 zipo katika hali nzuri, kilometa 151.04 sawa na asilimia 26.06 ni za wastani na kilometa 215.62 sawa na asilimia 37.2 zipo kwenye hali mbaya.
Anasema asilimia kubwa ya mtandao wa barabara katika wilaya hiyo zipo kwenye hali mbaya na kwamba juhudi za kusaidia zinahitajika, ikizingatiwa kuwa maeneo mengi ya wilaya hiyo yapo milimani.
JAMHURI limemtafuta mkandarasi wa Kampuni ya Asjel Construction Limited aliyetajwa na TARURA lakini baada ya mwandishi kujitambulisha na kueleza lengo la kumpigia simu alisema hawezi kuzungumza bila ruhusa kutoka kwa wakubwa wake wa kazi aliowataja kuwa ni TARURA.
Akaomba apewe muda kidogo ili awasiliane na wakubwa wake wa kazi lakini alipopigiwa kwa mara nyingine alisema hawezi kuzungumza chochote na kumtaka mwandishi awasiliane na meneja wa TARURA.
Kwa mujibu wa sensa ya idadi ya watu ya mwaka 2012, Kata ya Shighatini ina wakazi 7,765 na Kata ya Ngujini ina wakazi 3,314 huku wengi wao wakijishughulisha na kilimo na ufugaji.