Katika mfululizo wa makala za Bandari, leo tunakuletea Bandari ya Tanga ambayo ni miongoni mwa bandari kubwa nchini zilizo chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).

Bandari hii inayopatikana Kaskazini mwa Tanzania katika pwani ya Bahari ya Hindi ni fursa kubwa na muhimu katika kuleta chachu kwa biashara na uchumi wa viwanda kwa mikoa ya Kaskazini na kwa nchi jirani za Rwanda, Uganda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sudan Kusini. 

Historia ya Bandari ya Tanga inaanzia mwaka 1888 ilipoanzishwa na wakoloni wa Kijerumani. Bandari hii ina uwezo wa kuhudumia meli zenye uzito wa zaidi ya tani 1,200. Shughuli za upakuaji na upakiaji meli hufanyika kwenye maji yenye kina kirefu (Nangani). Meli zenye uzito chini ya huo uhudumiwa gatini. Bandari hii ina gati yenye urefu wa mita 462 na kina cha maji kuanzia mita 2 hadi 3.5 wakati wa bamvua dogo na kwa asili gati hilo lilijengwa na kina cha maji cha mita 5. 

Kwa upande wa maji marefu ambako bandari inahudumia meli kubwa nangani (Deep sea vessels) kuna kina kati ya mita 8 hadi 18.  Vifaa mbalimbali hutumika kuhakikisha meli inahudumiwa nangani na gatini, ikiwemo matishari ya kati ya tani 80 hadi 600 ambayo huvutwa na ‘Tugs’. Bandari ya Tanga kama zilivyo bandari nyingine nchini Tanzania inafanya kazi saa 24, siku 7 za wiki na siku 365 za mwaka.

Katika kuhakikisha Bandari ya Tanga inaleta chachu katika sera ya taifa ya uchumi wa viwanda, serikali kupitia TPA iliamua kutekeleza miradi mbalimbali yenye lengo la kuijengea uwezo bandari hii ili iweze kuhudumia meli na shehena kubwa kwa ufanisi zaidi ili kuhaikisha bandari hii inaleta mchango mkubwa kwa taifa katika kukuza biashara na uchumi wa viwanda. 

Ili kufanikisha azima hiyo, miradi mbalimbali imekuwa inatekelezwa ikiwemo ya muda mfupi kama vile manunuzi ya vifaa, miradi ya muda mrefu kama ujenzi wa sehemu ya kuhifadhia makasha na uboreshaji wa gati namba 2 kwa ajili ya kuhudumia meli na mizigo kwa ufanisi wenye tija kubwa zaidi. 

TPA inatekeleza mradi wa kuboresha gati namba 2 ambapo maboresho yanayofanywa ni pamoja na kuongeza kuchimba kina kwa zaidi ya mita 2, kuimarisha gati na kuweka mfumo wa kuzuia kutu katika nguzo.

Mradi huu utakapokamilika utasaidia kuongeza uwezo wa kuhudumia meli na shehena zaidi. Pia mradi huu utawezesha wafanyakazi kufanya kazi katika mazingira bora na usalama wa vyombo vitakavyohudumiwa. 

Katika kuhakikisha ulinzi na usalama wa bandari na mizigo ya wateja na kudhibiti uingiaji na utokaji bandarini, TPA inatekeleza mradi wa kisasa wa ulinzi kwa kuweka kamera za CCTV na vifaa maalumu vya ukaguzi (metal detectors) na kuweka mashine ya kukagulia mizigo (scanners) inayoingia na kutoka bandarini. Mradi huu utakapokamilika utasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa bandari na utasaidia kujiridhisha usalama na uhalisia wa mizigo inayopita bandarini. 

Pia TPA inatekeleza mradi wa kusakafia maeneo yaliyo wazi, ukarabati wa Ulenge Light House, ukarabati wa jengo la abiria na mizigo (Baggage Room), ukarabati wa shedi Na. 6, 7 na 8 na kuweka uzio maeneo ya bandari.

Mradi huu upo katika hatua ya utekelezaji na umeshafikia asilimia 40. Mradi utakapokamilika utaboresha na kuongeza maeneo ya kuhifadhi mizigo, huduma za kuongoza meli kuwa rahisi, mazingira ya wafanyakazi kuwa bora zaidi, lakini pia matumizi kwa ajili ya abiria yatakuwa na mandhari ya kuvutia, kutakuwa na uhakika wa kuhifadhi mizigo bila kupata athari yoyote. Pia kuweka uzio kutasaidia kudhibiti uingiaji kiholela katika maeneo ya bandari na kuimarisha ulinzi na usalama.

Mradi mwingine ambao TPA inatekeleza katika Bandari ya Tanga ni mradi wa ujenzi wa matishari mawili (barges) ya tani 2,500 kila moja, ambapo ujenzi wa Barge Hapa Kazi Na. 1 umefikia asilimia 94 na ujenzi wa Barge Hapa Kazi Na. 2 umefikia asilimia 54. Vitendea kazi hivi vitakapokamilika vitaiwezesha bandari kutoa huduma nafuu na yenye ufanisi kwa wateja.

Kwa upande wa vifaa, TPA imeshanunua kwa ajili ya Bandari ya Tanga na tayari vimeshapokelewa, ni pamoja na Wheel loaders 3 za tani 7, Reach stackers 2 za tani 45, Harbour Mobile Cranes 2 za tani 100 kila moja na Forklift  moja ya tani 16. Vifaa hivi vitasaidia kuongeza kasi ya utendaji kazi na kuongeza ubora wa huduma kwa wateja wa Bandari ya Tanga.

TPA imo katika mchakato wa kununua vifaa vingine kwa ajili ya Bandari ya Tanga, ikiwa ni pamoja na Mooring Boat moja, Terminal Tractors 4 za tani 40 na Trailers 4, Forklift moja ya tani 25 na Pilot Boat moja.

Kupatikana kwa vifaa hivi TPA inalenga kuijengea uwezo Bandari ya Tanga ili iweze kuhudumia meli na mizigo ya wateja kwa ufanisi zaidi, kwani inajua Bandari ya Tanga ni kiungo muhimu kwa ajili ya kuleta chachu katika uchumi kwa mikoa ya ukanda wa Kaskazini mwa Tanzania na nchi jirani.

Aidha, katika Bandari ya Tanga kuna mradi mkubwa wa kimataifa wa bomba la mafuta ambao upo katika hatua za awali za utekelezaji wake na inatarajiwa kuwa utakamilika mwaka 2020 na kuanza kazi katikati ya mwaka 2021. 

Bomba hili lenye urefu wa kilomita 1,444 na upana wa inchi 54 litaanzia Hoima, Kabaale nchini Uganda na litaishia Bandari ya Tanga kwa kupitia mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Simiyu, Singida, Manyara hadi Tanga kupitia wilaya za Handeni na Muheza.  

Mradi wa bomba hili utakapokamilika inakadiriwa litakuwa na uwezo wa kusafirisha mapipa 200,000 kwa siku. Inatarajiwa kwamba meli zenye uwezo wa mpaka tani 250,000 (Suezmax) zitakuwa zinaingia katika Bandari ya Tanga. TPA tayari imeshaainisha eneo lenye mita za mraba 2,400 ambalo litatumika kuhifadhia kwa muda vifaa vya ujenzi kabla ya Pongwe katika eneo mahususi lililotengwa na Jiji la Tanga kwa ajili ya mradi wa bomba la mafuta.

Bandari ya Tanga ilichaguliwa kuwa lango la kupitishia mafuta ghafi kutoka Uganda kwa sababu eneo la kufunga meli lina kina kirefu hadi kufikia mita 23. Pia eneo hilo lina kingo za asili ambalo limezibwa na Kisiwa cha Pemba na mafungu kama Niuli na Fungu Nyama. Tayari eneo la Chongoleani lenye hekta 200 lililoko kilomita 6 kutoka barabara kuu ya Tanga – Mombasa limeainishwa na fidia iliyofikia kiasi cha Sh 2,979,130,838 zimeshalipwa kwa wakazi wa eneo hilo. 

Mradi huu wa bomba la mafuta utakapokamilika utakuwa na faida mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongeza ukuaji wa uchumi kwa kuchangia pato la taifa, kwa kuwa tozo zitakazokuwa zinakusanywa kwa upande wa meli zitakazokuwa zinaingia pamoja na utumikaji wa eneo bomba litakakopita (wayleave).

Wakati wa ujenzi na baada ya ujenzi idadi ya Watanzania kati ya 15,000 hadi 20,000 watapata ajira katika bomba hili. Bomba hili litachangia uchumi wa mkoa pamoja na uchumi wa mwananchi mmoja mmoja. 

Ujio wa bomba hili unatarajiwa kuchochea miradi mingine kama ujenzi wa reli kutoka Tanga kuelekea nchi za Maziwa Makuu. Mradi huu utachochea kasi ya utafutaji wa mafuta katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki.

Aidha, TPA imeshawasilisha serikalini mradi wa ujenzi wa Bandari ya Mwanmbani kumpata mwekezaji. Eneo la Mwambani liliainishwa na kuwekwa jiwe la utambuzi na serikali tangu mwaka 1975.

Eneo hilo lina ukubwa wa hekta 174.2 na fidia ya Sh bilioni 2.59 imeishalipwa kwa wakazi wote wa eneo la mradi baada ya tathmini kutoka Halmashauri ya Jiji la Tanga. Mradi wa Bandari ya Mwambani baada ya kukamilika utaondoa changamoto za bandari kuhudumia meli nangani na kuiwezesha bandari kuhudumia shehena inayokadiriwa kuwa tani milioni 2.5 kwa mwaka.