Na Mwandishi Maalum
Baada ya kuona jinsi Bandari ya Kyela inavyoing’arisha kiuchumi na kijamii Kanda ya Juu Kusini na nchi jirani za Malawi, Msumbiji na Zambia wiki iliyopita, katika makala haya tutaona jinsi Bandari ya Mwanza ilivyo kiungo muhimu cha uchumi na biashara kati ya mikoa ya Kanda ya Ziwa, nchi za Afrika Mashariki na maeneo mengine.
Bandari zilizo chini ya Bandari ya Mwanza
Bandari ya Mwanza ni miongoni mwa bandari zilizo chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA). Bandari hii inasimamia bandari zote zinazopatikana katika ukanda wa Ziwa Victoria kwa upande wa Tanzania ambazo ni Mwanza, Bukoba, Kemondo Bay, Nansio na Musoma.
Bandari nyingine za Mamlaka katika Ziwa Victoria ni Kinesi, Shirati (Sota) mkoani Mara, Nyamirembe, Chato, Nkome, Bukondo (mkoani Geita), Kyamkwikwi, Magarini mkoani Kagera, Buchenzi, Nungwe Bay, Kahunda, Maisome, Ukara, Nyakalilo, Mgambo, Kome Ntama, Kome Mchangani, Lushamba, Irigamba, Luhama, Mharamba, Itabagumba, Karumo (mkoani Mwanza), Solima mkoani Simiyu.
Historia ya Bandari Mwanza
Bandari ya Mwanza na bandari zake kila moja ina historia yake na historia ya baadhi ya bandari inaanzia tangu kipindi cha ukoloni na nyingine zilijengwa baada ya uhuru. Bandari ya Mwanza Kaskazini ilijengwa mwaka 1939 ikiunganisha wasafiri wa reli waliokuwa wakielekea mikoa ya Kagera na Mara pamoja na nchi jirani – Kenya na Uganda.
Bandari ya Bukoba ilijengwa mwaka 1945 wakati bandari ya Mwanza Kusini ilijengwa mwaka 1960 na kujengewa Daraja la Mabehewa mwaka 1966. Bandari ya Kemondo Bay ilijengwa mwaka 1971 – 1973 maalum kwa ajili ya mizigo ya biashara kwenda na kutoka nje ya nchi ikitokea nchi jirani za Uganda na Burundi pamoja na Mkoa wa Kagera; vile vile bandari hizi zimekuwa kiunganishi muhimu kati ya bandari ya Mwanza na bandari kuu ya Dar es Salaam.
Awali, Bandari hizi zilikuwa zinasimamiwa na Shirika la Reli na Bandari la Afrika Mashariki (EAR & H), baadaye mwaka 1974 zikawa chini ya Shirika la Reli la Afrika Mashariki (EAR) na hatimaye mwaka 1978 zikawa chini ya umiliki na uendeshaji wa Shirika la Reli (TRC).
Mwaka 1999 Kitengo cha Meli cha Shirika la Reli (TRC) kilifanywa kuwa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) na kukabidhiwa majukumu ya uendeshaji wa meli na bandari katika Ziwa Viktoria (pamoja na Nyasa na Tanganyika).
Mnamo Julai, 2006 bandari zilihamishiwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA). Hii ni kwa mujibu wa utekelezaji wa Sheria ya Bandari Na.17 ya Mwaka 2004. Tangu wakati huo Bandari ziko chini ya usimamizi na uendeshaji wa TPA.
Uwezo na Umuhimu wa Bandari ya Mwanza
Bandari za Mwanza na bandari zake zina uwezo wa kuhudumia wastani wa tani za mizigo 1,000,000 (milioni moja) kwa mwaka pamoja na abiria 1,000,000 (milioni moja) kwa mwaka.
Aidha Bandari ya Mwanza ina umuhimu sana kwa maendeleo ya nchi na kwa watumiaji wa bandari. Bandari ya Mwanza ni kiungo muhimu cha kiuchumi na biashara kati ya mikoa ya Kanda ya Ziwa, nchi za Afrika Mashariki na maeneo jirani.
Bandari zinarahisisha huduma za kijamii kama vile usafirishaji wa abiria na mizigo kutoka na kwenda sehemu mbalimbali vikiwemo visiwa vilivyomo Ziwa Victoria kama vile Ukerewe na Goziba.
Kupitia shughuli za kibandari ambazo kimsingi ni huduma na biashara, nchi inajipatia mapato na wananchi kupata ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
Jamii pia inafaidika kwa kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na bandari kwa dhana/sera ya uwajibikaji kwa jamii (CSR); mfano utoaji wa madawati kwa Shule na uchimbaji visima vya maji.
Ulinzi na Usalama wa bandari
TPA ina ulinzi madhubuti katika bandari zake zote kwa lengo la kuhakikisha ulinzi wa mizigo katika bandari ya Mwanza ni wa kiwango cha juu. Huduma hii ya ulinzi wa mizigo inatolewa na askari wa TPA kwa kushirikiana na askari wa SUMA JKT Guard Ltd.
Aidha ulinzi na usalama wa mizigo unafanywa pia na vyombo vingine vya usalama sambamba na hilo bandari pia ina kikosi madhubuti cha zimamoto ambacho usimamia usalama mahali pa kazi pamoja na mazingira.
Uhusiano wa Bandari na Wadau wake
Bandari ya Mwanza ina uhusiano mzuri na wadau wake na bandari imekuwa na utaratibu wa kukutana mara kwa mara na wadau mbalimbali wa bandari wakiwamo wateja na taasisi za serikali, kujadili mambo mbalimbali yahusuyo bandari, uendeshaji wake na kuzipatia ufumbuzi au majibu kwa kadri changamoto zinavyojitokeza.
Miradi katika Bandari ya Mwanza
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ili kuboresha utoaji wa huduma katika bandari ya Mwanza imeamua kuwekeza katika miradi mbalimbali ya maendeleo. Miradi inayotekelezwa katika Bandari ya Mwanza Kusini ni pamoja na kuongeza kina katika gati za kuegeshea meli, ukarabati wa Daraja la Mabehewa (link span) na ununuzi wa kreni yenye uwezo wa tani 50.
Pia TPA inatekeleza miradi ya maendeleo katika bandari za Ntama na Lushamba wilayani Sengerema kwa kujenga gati kwa kila bandari. Kwa upande wa Wilaya ya Ukerewe TPA inafanya ukarabati wa gati ya bandari ya Nansio kwa kubadilisha mbao zilizokuwa zimechakaa pamoja na mradi wa kuongeza kina katika gati ya kuegeshea meli.
Miradi mingine katika bandari zilizo chini ya bandari ya Mwanza ambayo TPA inatekeleza ni ujenzi wa gati katika mwalo wa Mwigobero mkoani Mara katika wilaya ya Musoma. Kwa upande wa Mkoa wa Geita TPA ina ujenzi wa Bandari ya Nyamirembe katika Wilaya ya Chato.
Aidha kwa bandari zilizo mkoani Kagera wilayani Muleba TPA ina miradi ya ujenzi wa gati katika bandari ya Magarini na Kyamkwikwi pamoja utwaaji wa ardhi pamoja na ujenzi wa ghala la kuhifadhia mizigo na jengo la abiria.
TPA imeanza utekelezaji wa ujenzi wa bandari kavu katika eneo la Fela wilayani Misungwi katika mkoa wa Mwanza ambapo imefanikiwa kutwaa ekari 1,178 kwa kulipa fidia ya Sh bilioni 5.6 kwa kaya 144. Ujenzi wa bandari kavu hiyo ni utekelezaji wa makubaliano na maelekezo ya Marais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na wa Jamhuri ya Uganda, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni.
Lengo la bandari kavu hiyo ni kuwapunguzia umbali wafanyabiashara wa Uganda ili wasisumbuke kwenda hadi Bandari ya Dar es Salaam badala yake mizigo yao wawe wanachukulia Mwanza ikiwa ni njia ya uhakikia na nafuu ya kusafirisha mizigo yao na hivyo kuifanya Bandari ya Mwanza kuwa kiunganishi cha uhakika katika ukanda wa maziwa makuu.
TPA kwa kumjali mteja ina kituo cha huduma kwa mteja ambacho kina simu ambazo mteja anaweza kupiga simu au kutuma ujumbe mfupi (SMS) bure kuuliza swali lolote au kupata ufafanuzi juu ya meli na mizigo ya wateja bandarini kwa saa 24. Namba hizo ni 0800110032 au 0800110047. TPA imejipanga kutoa huduma bora kwa wateja wake.