Kwa miaka mingi mikoa ya Kusini ilikuwa imesahaulika. Katika makala hii tutawaelezea nafasi ya Bandari ya Kyela katika kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa Nyanda za Juu Kusini na nchi jirani za Malawi na Msumbiji.
Bandari ya Kyela ambayo ipo katika mwambao wa Ziwa Nyasa ni miongoni mwa bandari ambazo zipo chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).
Bandari hii ina jukumu la kusimamia bandari zote zilizopo katika Ziwa Nyasa kwa upande wa Tanzania. Miongoni mwa bandari zilizo chini ya Bandari ya Kyela ni; Itungi, Kiwira (wilayani Kyela, Mkoa wa Mbeya), Mbamba Bay, Liuli na Ndumbi (wilayani Nyasa, Mkoa wa Ruvuma), Manda na Lupingu (wilayani Ludewa, Mkoa wa Njombe).
Uwezo wa Bandari ya Kyela na bandari zake katika kuhudumia shehena ni tani 500,000 na abiria 20,000 kwa mwaka. Mipango ya TPA ni kuifanya Bandari ya Itungi kuhudumia abiria na mizigo midogo (passenger terminal) na Bandari ya Kiwira kuhudumia mizigo mikubwa (cargo terminal).
Bandari ya Kyela na bandari zake katika Ziwa Nyasa zina umuhimu wa kipekee katika uchumi na ustawi wa nchi yetu. Jamii kubwa ya mwambao wa Ziwa Nyasa hutegemea njia ya maji kusafiri na kusafirisha bidhaa mbalimbali.
Mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe na Ruvuma imekuwa ikinufaika kwa namna moja au nyingine kupitia Bandari ya Kyela na bandari zake katika Ziwa Nyasa.
Bandari za Dar es Salaam na Mtwara zinasaidiwa na bandari zilipo katika Ziwa Nyasa kuyafikia baadhi ya masoko yaliyo katika nchi za Malawi na Msumbiji. Mradi wa Mtwara Corridor unahusisha bandari za Ziwa Nyasa ambapo utakapokuwa tayari shehena ya mizigo kupitia Bandari ya Mtwara itaongezeka, hivyo kuinua pato kwa Mamlaka na taifa kwa ujumla.
Bandari ya Kyela inatoa fursa kwa wafanyabiashara kusafirisha kiasi kikubwa cha mizigo kwa wakati mmoja na kwa gharama nafuu, kwenda umbali mfupi tofauti na usafiri wa barabara ambapo mzunguko wake unakuwa mrefu kulingana na jiografia ya maeneo yanayozunguka Ziwa Nyasa. Urahisi wa usafiri kwa watu na usafirishaji wa bidhaa unaoletwa na bandari umesaidia kukua kwa shughuli nyingi za kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wa ulinzi wa meli, abiria na mizigo katika Bandari ya Kyela ni imara na TPA imeendelea kuimarisha ulinzi kuhakikisha kuna usalama wakati wote kwa mizigo, meli, abiria na mali za Mamlaka kwa kutumia mbinu za kisasa.
Bandari ya Kyela imekuwa na ushirikiano mkubwa na wadau wake kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wateja wake kwa kukutana na watumiaji wa bandari kusikiliza changamoto na kero wanazokutana nazo na kuzitatua.
Ili kuhakikisha Bandari ya Kyela inaendelea kutoa huduma bora kwa wateja wake, TPA imewekeza katika miradi ya maendeleo. Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa meli mbili za mizigo Mv Njombe na Mv Ruvuma ambazo zimekamilika tangu katikati ya mwaka 2017 na zilizinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa. Meli hizi ambazo zimeshaanza kufanya kazi kila moja ina uwezo wa kubeba tani 1,000.
Meli hizi zimefungua fursa zaidi na kuboresha shughuli za kiuchumi, kibiashara na kijamii katika ukanda wa Ziwa Nyasa, hasa katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe na Ruvuma. Pia meli hizi zimekuwa kiunganishi kikubwa kibiashara na nchi jirani za Malawi, Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Zambia, hivyo kuongeza mapato kwa TPA na taifa kwa ujumla.
Mkandarasi MS Songoro Marine ameunda meli ya abiria na mizigo. Meli hiyo ina uwezo wa kuchukua abiria 200 na tani 350 za mizigo. Mradi mwingine uliokamilika ni wa kuweka sakafu ya matofali magumu (paving blocks) katika Bandari ya Itungi sambasamba na kuweka zege katika njia ya kuingia kwenye Bandari ya Kiwira.
Mradi mwingine ambao TPA imewekeza ni ujenzi na uendelezwaji wa Bandari ya Ndumbi kwa ajili ya kuhudumia shehena ya makaa ya mawe kutoka mgodi wa Ngaka na migodi mingine katika wilaya za Nyasa na Mbinga. Mradi mwingine unahusu ujenzi wa eneo la kuhifadhi mizigo ya wateja.
Mradi mwingine uliokamilika ni wa uchimbaji njia ya kuingilia Bandari ya Itungi (creek entrance channel) na sehemu ya gati la Itungi ulifanyika kati ya mwezi Januari na Mei 2017. Uchimbaji huo umesaidia kuongeza kina kutoka 0.5m iliyokuwepo kwa wakati huo hadi kufikia mita 5.
Katika kukabiliana na ushindani na bandari za nchi jirani, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania, inaendelea na mchakato wa kuanzisha Bandari Kavu katika eneo la Inyala lililo katika Mkoa wa Mbeya. Lengo la kuanzisha Bandari Kavu hiyo ni kuwapunguzia umbali wateja wa nchi za Malawi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
TPA kwa kumjali mteja ina kituo cha huduma kwa mteja ambacho kina simu ambazo mteja anaweza kupiga simu au kutuma ujumbe mfupi (SMS) bure kuuliza swali lolote au kupata ufafanuzi juu ya meli na mizigo ya wateja bandarini kwa saa 24. Namba hizo ni 0800110032 au 0800110047. TPA imejipanga kutoa huduma bora kwa wateja wake.