*Meli kubwa yatia nanga
ikiwa imebeba magari 4,041
DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Maalumu
Bandari ya Dar es Salaam imevunja rekodi yake baada ya wiki iliyopita kupokea meli kubwa zaidi kuwahi kufika, pia ikiwa ni ya kwanza yenye mzigo mkubwa zaidi wa magari kupokewa tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).
Meli hiyo ya MV Frontier Ace yenye ukubwa wa GRT 52,276 na urefu wa mita 189.45 ilibeba magari 4,041 na imetia nanga bandarini hapo ikitokea moja kwa moja nchini Japan hadi Dar es Salaam bila kusimama katika bandari ya nchi yoyote kama ratiba yao ya kusafiri kwa siku 14 ilivyopangwa.
Asilimia 74 sawa na magari 2,936 yaliyobebwa yanakwenda nchi jirani (transit) na yanayobaki nchini ni asilimia 26 sawa na magari 1,105. Magari hayo yanakwenda nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Malawi, Msumbiji, Sudan, Uganda, Zambia na Zimbabwe.
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eric Hamissi, anasema huo ni mwanzo mzuri kwao kutokana na maboresho yanayoendelea kufanyika na wanatarajia kuhudumia shehena kubwa zaidi za mizigo mchanganyiko, bidhaa mbalimbali za vyakula na mafuta.
“TPA imefanya maboresho mbalimbali katika bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na nyingine ndogondogo ili
kuhakikisha kuwa inatoa huduma bora kwa wateja wake wa ndani na nje ya Tanzania.
“Maboresho ya miundombinu yamesababisha kuongezeka kwa urefu na kina cha magati (yaani gati namba 0 hadi 7). Gati namba 0 ni mahususi kwa kuhudumia shehena ya magari na gati namba 1-7 ni mahususi kwa kuhudumia shehena mchanganyiko na bidhaa mbalimbali za vyakula,” anasema.
Katika hatua nyingine, anasema hapo awali Agosti, mwaka jana imewahi kupokea Meli ya Tranquil Ace iliyobeba magari 3,743 kutoka Japan, pia ana imani rekodi hiyo haitakuwa ya mwisho na itakuja kuvunjwa siku moja kwa kuwa bandari hiyo ina uwezo wa kupokea meli yenye uwezo wa kubeba magari 8,000.
Pia anasema kati ya Aprili 5 hadi 7, mwaka huu meli nne zilitia nanga bandarini hapo na kushusha jumla ya magari 8,384 wakati kwa wastani wanapokea magari 10,000 kwa mwezi.
Vilevile anasema msongamano unasababishwa na magari kukaguliwa bandarini hapo badala ya nje ya nchi yanakotoka. Anasema agizo la Rais Samia la kutaka yakaguliwe yanakotoka litarahisisha ufanisi wa utendaji wao.
Faida za maboresho
Hamissi anasema ongezeko la ujio wa meli kubwa na nyingi kufika Bandari ya Dar es Salaam linatokana na maboresho hayo.
Pia anasema shehena ya magari iliyohudumiwa bandarini hapo katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Machi, 2021 hadi Februari, 2022 ilifikia magari 185,524 sawa na ongezeko la asilimia 2.2 ukilinganisha na lengo la kuhudumia magari 181,492.
Vilevile anasema magari yaliyohudumiwa ni ongezeko la asilimia 38.4 ya magari yaliyohudumiwa kipindi kama hiki mwaka uliopita (Machi, 2020 hadi Februari, 2021).
Anasema ongezeko la shehena iliyopita na kuhudumiwa bandarini hapo katika kipindi cha Machi, 2021 hadi Februari, 2022 ni tani milioni 19.255 sawa na ziada ya asilimia 3.8 ya lengo la kuhudumia tani milioni 18.522.
Aidha, anasema shehena iliyohudumiwa ni ongezeko la asilimia 11.4 katika kipindi kama hiki kwa mwaka uliopita (Machi, 2020 hadi Februari, 2021).
Anasema bandari hiyo imehudumia tani milioni 17.352 sawa na asilimia 90.1 ya mzigo wote uliohudumiwa na TPA na kuendelea kuvunja rekodi za kuhudumia shehena kwa ufanisi na viwango vikubwa.
Mathalani, anasema Novemba, 2021 TPA ilivunja rekodi kwa kuhudumia meli 77 na makontena (TEUs) 17,000 ikiwa ni 7,000 zaidi ya lengo la makontena 10,000 kwa mwezi na kupungua kwa muda wa kuhudumia meli kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya vifaa vya kisasa.
Katika hatua nyingine, anasema baada ya maboresho hayo kuna ongezeko la mapato ya TPA yaliyokusanywa kipindi cha kuanzia Machi, 2021 hadi Februari, 2022 kwa kufikia Sh bilioni 1,018 sawa na asilimia 95.5 ya lengo la kukusanya Sh bilioni 1,067.41.
Anasema kuna ongezeko la asilimia 18.8 ya mapato yaliyokusanywa kwa kipindi kama hiki kwa mwaka uliopita (Machi, 2020 hadi Februari, 2021).
Pia anasema maboresho hayo yanafungua na kuchagiza wigo wa biashara katika ushoroba wa kati na wa Dar es Salaam na kuongeza ajira rasmi na zisizo rasmi katika mnyororo wa usafirishaji wa shehena mbalimbali.
“Ujio wa meli hii kubwa ya magari kunaongeza pato la kodi na mapato mengine ya serikali kupitia TPA na kutoa fursa za ajira kwa mnyororo wa usafirishaji wa shehena kama vile ajira kwa mawakala wa forodha, madereva wa magari, huduma za kifedha, vyakula na kadhalika,” anasema.
Pamoja na mambo mengine, anasema mafanikio hayo yanapatikana kutokana na uhusiano wa diplomasia ya uchumi ulioimarishwa na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia ziara zake za nje ya nchi.
Pia anasema maboresho hayo yametokana na miundombinu na vifaa, hali ya ulinzi na usalama bandarini nao umechangia kuaminika kwa wateja.
“Tunaishukuru serikali chini ya uongozi wa Rais Samia ambaye ni balozi namba moja wa TPA akiinadi katika majukwa mbalimbali wakati wa safari zake nje ya nchi na kuongeza imani kwa wateja wetu,” anasema na kuongeza:
“Matokeo ya juhudi hizo za Rais Samia yamedhihirika na tunahudumia shehena kubwa ya magari, mengi yakiwa yanakwenda nchi jirani, yaani transit.
“TPA inapenda kutambua mchango wa wateja na wadau wetu ikiwamo Kampuni ya Uwakala wa Meli (Inchcape Shipping Services) kwa kutuamini na kuendelea kutumia bandari yetu na hatimaye kuleta meli hii moja kwa moja kutoka Japan kwa mara ya kwanza bila kupita bandari nyingine yoyote kushusha magari.
“TPA inayo furaha kuwafahamisha wateja wake wote duniani kwamba Tanzania kupitia bandari zake iko tayari kupokea na kuhudumia meli kwa wakati na kwa kutumia vifaa vya kisasa. Kwa niaba ya Watanzania tupo tayari kuwahudumia kupitia bandari zetu.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TPA, Balozi Ernest Mangu, anasema menejimenti ya bandari inawasiliana na mamlaka mbalimbali kwa ajili ya kutekeleza agizo la kutaka magari yakaguliwe nje ya nchi.
“Kwa sasa Bandari ya Dar es Salaam inakaa katika mstari ulionyooka na maelekezo mnayotupa ya kuongeza ufanisi tunayafanyia kazi. Tumeshaanza kuwasiliana na mamlaka husika ili kupunguza msongamano wa magari yapungue hapa na tupokee mengi zaidi na ujio wa magari haya utasaidia uchumi wa nchi na wa bandari kwa ujumla wake,” anasema.
Naye Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, ameitaka TPA kuongeza ufanisi katika kupakua magari hayo licha ya changamoto ya uhaba wa vifaa unaoikabili.
“Kama mliyapakua magari kwa siku mbili, basi myapakue kwa siku moja, na hiyo itasaidia kuitangaza Bandari ya Dar es Salaam sehemu mbalimbali ulimwenguni,” anasema.
Mbarawa anasema kufanya hivyo kutaongeza imani ya mataifa mbalimbali duniani kutumia bandari hiyo huku akionya kuongezwa uaminifu kwa mizigo ya wateja.
“Si sawa mtu ameletewa gari lake kisha anakuta halina kioo, najua tunasifika kwa uaminifu na tunapaswa kuendeleza hali hiyo,” anasema.
Anaitaka TPA kuanza utaratibu wa kuyahifadhi katika bandari kavu (ICD) magari yanayopakuliwa ili kuondoa msongamano bandarini hapo.
Kisha akamuagiza Hamissi kupima ufanisi wa bandari kwa viwango vya kimataifa kwa kulinganisha na utendaji wa nchi jirani.
“Bandari kazi yake ni kupakua magari, si kuyahifadhi ili kuondoa msongamano. Pelekeni magari yaliyopo katika ICD zilizokamilika, naagiza zote zifunguliwe na zitumike ikiwezekana na kontena zilizopo hapa bandarini zipelekwe huko,” anasema.
Pia anakazia agizo la Rais Samia la ukaguzi wa magari huko huko nje ya nchi ili yatakapofika nchini yaondolewe haraka bandarini hapo.
Anaagiza kuongezwa ufanisi wakati wa upakuaji wa mizigo kwa ajili ya kupunguza muda wa meli kukaa bandarini hapo na itasaidia kuongeza imani kwa wateja na akataka kitengo cha masoko kiboreshwe ili waitangaze ulimwenguni na waongeze maarifa licha ya changamoto ya vifaa iliyopo.
“Miaka miwili au mitatu iliyopita magari yaliyokuwa yanapokewa hapa ni kati ya 500, 600 au 700 lakini baada ya ukarabati wa gati namba moja hadi saba matokeo makubwa yameanza kuonekana bandarini hapa,” anasema.