Baada ya kuelezea njia za kutoa gari bandarini katika makala zilizotangulia kwa nia ya kuepuka usumbufu na kupata uhalali wa gari lako, leo tunakueleza kuhusu nyaraka muhimu unazopaswa kupewa na wakala wako anapokukabidhi gari uliloagiza nje ya nchi na likapitia bandarini.

Kuna umuhimu wa fomu za Vehicle Discharge Inspection Transfer Tally (VDITT) na ile ya makabidhiano ya gari (Vehicle Hand Over Form) wakati mteja anapopokea gari lake kutoka kwa wakala wa forodha aliyempatia kazi ya kutoa gari bandarini.

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ilianza kutoa fomu hizi kuhakikisha wateja wanachukua au wanapata magari yao kutoka bandarini yakiwa katika hali ileile kama yalivyoshushwa na kupokewa kutoka melini. Hatua hii ilichukuliwa na TPA dhidi ya vitendo vya wizi wa vipuri vya magari ya wateja yakiwa katika hatua mbalimbali ya kusafirishwa, kuanzia bandari ambako gari linapakiwa melini mpaka mteja anavyopokea gari lake.

Vehicle Discharge Inspection Transfer Tally (VDITT)

 

Vehicle Discharge Inspection Transfer Tally (VDITT) ni fomu inayotumika kuonyesha hali halisi ya gari lilivyopokewa bandarini baada ya kuteremshwa kutoka melini. Fomu ya VDITT imeainisha vipuri mbalimbali vinavyopaswa kuwemo katika gari na sehemu ya kutoa maelezo ya hali ya mwonekano wa gari.

Baada ya gari kuteremshwa kutoka melini, karani wa TPA hulikagua gari na kujaza fomu hiyo kulingana na hali aliyoona kwa kuweka alama ya vema (√) kwa kipuri ambacho kipo kwenye gari na alama ya kosa (X) kwa kipuri kinachokosekana. Karani akishakamilisha kujaza fomu hiyo ya VDITT ataiweka ndani ya gari husika mpaka mteja anapokuja kuchukua gari lake.

Fomu ya VDITT ina umuhimu mkubwa kwa mteja na kwa TPA, kwani fomu hiyo inaonyesha hali halisi ya gari lilivyopokewa bandarini baada ya kuteremshwa kutoka melini na kuthibitishwa na Afisa Mkuu wa Meli husika kwa kusainiwa na kugongwa muhuri. Matumizi ya fomu hii yameondoa malalamiko kutoka kwa wateja na kulinda heshima ya TPA, hivyo kuongeza uaminifu wa wateja kwa kuendelea kutumia Bandari ya Dar es Salaam na bandari nyingine za TPA.

Wakati wa utoaji au uchukuaji wa gari (delivery) mteja akikuta gari lake lina tatizo lolote anatakiwa kuikagua fomu ya VDITT iliyotumika kukagulia gari lake kama inaonyesha vipuri husika vipo au hapana. Kama vipuri havipo fomu itaonyesha na kama vipuri husika vilikuwepo, lakini wakati anapokea gari havipo, anashauriwa ajiridhishe kwa kuangalia fomu ya pili ambayo ni ya makabidhiano (Hand Over Form).

Matumizi ya stika za rangi ya kijani na nyekundu

 

Pamoja na fomu ya VDITT katika ukaguzi wa magari, TPA iliamua kuanzisha matumizi ya stika za kijani na nyekundu. Baada ya ukaguzi endapo gari litakuwa na vipuri vyote, karani ataweka stika ya rangi ya kijani yenye alama ya vema (√) juu ya kioo cha mbele ya gari. Umuhimu wa stika ya kijani ni kuonyesha kwamba gari hilo halina tatizo la kukosekana kwa kipuri chochote.

Aidha, kama gari lililokaguliwa likaonekana lina upungufu wa baadhi ya vipuri, karani ataweka stika ya rangi nyekundu yenye alama ya kosa (X) juu ya kioo cha mbele ya gari husika. Matumizi ya stika hiyo nyekundu yatathibitisha kwamba gari husika limepokewa bandarini likiwa na dosari za kukosekana kwa baadhi ya vipuri kama fomu ya VDITT iliyotumika kukagulia gari husika itakavyokuwa inaonyesha.

Fomu ya Makabidhiano ya Gari (Vehicle Hand Over Form)

Fomu ya makabidhiano ya gari ni nyaraka ambayo hutumiwa na TPA kwa ajili ya kukabidhiana gari na mteja wakati anapochukua gari lake kutoka bandarini. Wakati wa utoaji au uchukuaji wa magari bandarini ni lazima kila gari liandikiwe vehicle hand over form.

Lengo la fomu hii ni kutaka kuonyesha hali halisi ya gari mteja anapochukua gari lake bandarini na fomu ya VDITT ni fomu ambayo inaonyesha hali halisi ya gari lilivyopokelewa bandarini baada ya kuteremshwa kutoka melini.

Baada ya gari kuteremshwa kutoka melini linahifadhiwa bandarini mpaka mteja aje kuchukua gari lake. Katika kipindi hicho kunaweza kutokea tatizo lolote wakati gari likiwa bandarini, hivyo TPA iliona kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na aina ya nyaraka hii ya vehicle hand over form.

Nyaraka hii ni ya muhimu sana kwa mteja kwani itamuonyesha hali halisi ya gari lake wakati wakala wake wa forodha alivyolichukua kutoka bandarini. Kama gari husika litakuwa na tatizo lolote itamsaidia mteja kudai fidia kwa gari lake.

Ni muhimu kwa mteja anapopokea gari lake kutoka kwa wakala wake wa forodha akabidhiwe fomu hizi za Vehicle Discharge Inspection Transfer Tally (VDITT) na ile ya makabidhiano ya gari (Vehicle Hand Over Form).

Endapo mteja hatapatiwa fomu hizo na wakala wake, basi mteja anatakiwa kutoa taarifa TPA kwa kutuma ujumbe au kupiga simu za bure za TPA kutoa taarifa ili wakala husika achukuliwe hatua stahiki. Wasiliana nasi bure kwa namba 0800110032 au 0800110047.